1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mizinga yaripuliwa mjini Mogadishu

Oummilkheir6 Machi 2007

Mtihani wa mwanzo mara baada ya kuwasili vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika nchini Somalia

https://p.dw.com/p/CHIr
Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Alpha Omar Konare
Mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Alpha Omar KonarePicha: AP

Watu wasiopungua watatu wameuwawa kufuatia mapigano kati ya waasi na wanajeshi wa Ethiopias karibu na kambi ya kijeshi mjini Mogadischu.

Mashahidi wanasema mapigano hayo yameripuka muda mfupi baada ya wanajeshi wa mwanzo wa vikosi vya kulinda amani vya umoja wa Afrika kuwasili katika mji mkuu huo wa Somalia.

”Watu watatu wameuwawa.Raia mmoja na waasi wawili waliokua na silaha” amesema Mohammed Ismael ambae ni fundi magari mjini Mogadischu.Shahidi mwengine kwa jina Khadra Aden amethibitisha habari hizo akisema mapigano yameripuka baada ya waasi kuhujumu makao makuu ya wizara ya ulinzi yaliyojengewa boma mjini Mogadishu.Vikosi vya Ethiopia vinapiga kambi katika jingo hilo.Wanajeshi wa Ethiopia wamejibisha hujuma hizo.Mashambulio hayo yamepelekea watu sita kujeruhiwa,waasi wawili na raia wanne.

Mji mkuu wa Somalia unatikiswa tangu leo asubuhi na mashambulio yaliyoripuka mara baada ya kuwasili wanajeshji wa mwanzo wa kikosi cha AMISOM.

Mizinga isiyopungua sabaa imevurumishwa katika uwanja wa ndege wa Mogadischu,zilikotuwa ndege mbili zilizokua na wanajeshi 370 wa Uganada wanaotumikia vikosi vya kulinda amani vya AMISOM.

Muda mfupi baadae risasi zikaanza kufyetuliwa na waasi na kujibiwa na wanamgambo wanaoelemea upande wa serikali.Kwa mujibu wa mashahidi visa hivi viwili havikusababisha hasara ya maisha.

Mjini Kampala,naibu waziri wa ulinzi wa Uganda Ruth Nankabirwa amesema wanajeshi wa nchi yake wanaortumikia shughuli za amani za umoja wa Afrika nchini Somalia,wanatambua hatari ya shughuli zao.”Hatukuwapeleka wanajeshi wetu bila ya kujua hatari iliyoko” amesema bibi Nankabirwa aliyeongeza kusema tunanunkuu:

“Tutakua wa mwanzo kuhakikisha wanajeshi wetu wako salama kuweza kuendelea na shughuli nyengine pia za kulinda amani.Mwisho wa kumnukuu naibu waziri wa ulinzi wa Uganda.

Kamishna wa masuala ya amani na usalama wa umoja wa Afrika, Said Djinnit alisema wakati wanajeshi wa kulinda amani walipowasili Somalia,lengo lao ni kuwasaidia wasomali wote waishi kwa amani ambayo itawezekana tuu kupitia mazungumzo.

Rais Abdullahi Yusuf Ahmed wa Somalia wiki iliyopita alitangaza kuitishwa mazungumzo ya suluhu ya taifa yatakayofanyika mjini Mogadishu kuanzia april 16 ijayo.Mazaungumzo hayo yatadumu wiki mbili.Hakusema lakini kama wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam wataalikwa au la.