Mizengwe yaendelea Misri | Matukio ya Afrika | DW | 21.06.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Mizengwe yaendelea Misri

Tume ya uchaguzi nchini Misri imeahirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi wa rais nchini humo yaliyotarajiwa Alhamis (21.06.2012), ili kushughulikia malalamiko yaliyotolewa na wagombea wa kiti hicho.

Karatasi za kupigia kura.

Karatasi za kupigia kura.

Tume hiyo ilitangaza Jumatano jioni kupitia televisheni ya taifa kuwa inangalia malalamiko karibu mia nne yaliyotolewa na Muhammed Mursi na Ahmed Shafique, lakini haikusema ni lini itatangaza mshindi. Mursi na Shafique wote walijitangazia ushindi.

Tangazo hilo limeongeza hali ya wasiwasi nchini Misri wakati ambapo Mohammed Mursi anadai kuna njama zilizoandaliwa dhidi ya chama chake cha udugu wa Kiislam ili kuvuruga uchaguzi na kumtupa nje ya kinyanganyiro hicho.

Wandamanaji wakiwa katika uwanja wa Tahrir mjini Kairo siku ya Jumatano.

Wandamanaji wakiwa katika uwanja wa Tahrir mjini Kairo siku ya Jumatano.

Shutuma hizo zinazidisha munkari na uwezekano wa kutokea sintofahamu kwa upande wa chama hicho endapo mpinzani wa Mursi, Waziri Mkuu wa mwisho wa Hosni Mubarak atatangazwa kuwa mshindi wa kiti cha urais.

Tangazo hilo linafuatia mfululizo wa mambao kadhaa yanayoweka mustakabali wa Misri mashakani ikiwa ni pamoja na hatua ya mahakama ya katiba kubatilisha bunge na kumruhusu Shafique kuendelea kushiriki uchaguzi, huku baraza la kijeshi likitumia fursa hiyo kujiongezea mamlaka. Na kama hiyo haitoshi, hali ya afya ya rais aliyepindulia Hosni Mubarak nayo ikaongeza wasiwasi kutokana na taarifa zilizokuwa zinakinzana.

Matumaini yanayofifia?
Uchaguzi wa rais nchini Misri ulipigiwa debe kama tukio la kihistoria kutokana na nchi hiyo kutokuwa na rais aliyechaguliwa kihalali kwa miongo kadhaa na rais huyo alitarajiwa kukabidhiwa madaraka na watawala wa kijeshi. Lakini sasa inaelekea mchakato huu utakuwa wa vuta nikuvute kati ya chama cha Udugu wa Kiislam (Muslim Brotherhood) kwa upande moja, na watawala wa kijeshi na masalia ya utawala wa Hosni Mubarak kwa upande wa pili.

Mamia ya wafuasi wa chama cha Udugu wa Kiislam waliweka kambi katika uwanja wa Tahrir Jumatano usiku wakipinga utawala wa kijeshi na kuapa kutoondoka hapo hadi pale bunge litakaporejeshwa. Baadhi ya malalamiko juu ya uchaguzi huo yaliwasilishwa Jumatano usiku, muda mfupi kabla tume hiyo haijatoa taarifa yake.

Mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislam, Mohammed Morsi.

Mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislam, Mohammed Morsi.

Kila upande undai kudhulumiwa'
Kambi ya Ahmed Sahfique ilidai kuwa kulikuwepo na udanganyifu katika mikoa 14 kati ya 27 ambapo karatasi za kura zilipelekwa zikiwa tayari zina alama ya ndiyo kwa Mursi, wakati mawakili wa Mursi walidai orodha ya wapiga kura ilikuwa na majina ya wanajeshi ambao hawaruhusiwi kupiga kura na pia majina ya watu waliyokufa.

Tayari wakuu watatu wa vituo vya kupigia kura wamekamatwa na wanaendelea kuhojiwa juu ya wizi wa kura, lakini wangalizi wa kimataifa wanasema ukiukaji waliouona wakati wa mchakato wa kupiga kura haukuwa mkubwa kiasi cha kuufanya utiliwe mashaka.

Wakati hayo yakitokea, naibu kiongozi wa chama cha udugu wa Kiislam, Khairat el-Shater alijitokeza katika televisheni na kukanusha uvumi kuwa alikuwa amekamatwa. Shater alisema kuna mbinu chafu zinafanywa ili kuchelewesha kuanza kwa enzi mpya kwa kutumia mizengwe kama vile kuchelewesha matokeo, kukamatwa watu, ugonjwa wa Mubarak na sheria za kijeshi. Akasisitiza kuwa Mohammed Mursi ndiye rais wa Misri wa kwanza kuchaguliwa na umma.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga\APE\DPAE
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman.