1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misri kutengua sheria

7 Juni 2012

Baraza la mahakama nchini Misri jana limependekeza kubatilishwa sheria mbili muhimu ili kumuwezesha waziri mkuu wa zamani wa utawala wa Mubarak kuendelea kugombania urais.

https://p.dw.com/p/15A18
Mpiga kura
Mpiga kuraPicha: picture-alliance/dpa

Katika uchaguzi na ikiwezekana kulivunja bunge lenye kuhodhiwa na mahasimu wao wa itikadi kali za Kiislamu.

Harakati hizi mpya za kisiasa nchini Misri ambapo jopo hilo la kisheria linatarajiwa kutowa uamuzi wake siku mbili kabla ya kufanyika kwa marudio ya uchaguzi wa rais.

Maamuzi kabla ya uchaguzi wa duru ya pili

Mahakama kuu inatarajiwa kutowa uamuzi wake juu ya sheria hizo hapo tarehe 14 mwezi huu wa Juni, ikiwa ni siku mbili kabla ya kufanyika kwa marudio ya uchaguzi wa rais kati ya waziri mkuu wa zamani, Ahmed Shafiq na mgombea wa chama cha Udugu wa Kiislamu, Mohamed Mursi. Wagombea hao wawili walijisombea kura nyingi katika duru ya kwanza ya uchaguzi huo wa rais hapo mwezi wa Mei.

Maamuzi hayo yatakuwa muhimu katika kuamuwa vipi Misri itatekeleza kipindi chake cha mpito kutoka utawala wa miaka 60 uliokuwa ukiungwa mkono na jeshi.

Ahmed Shafik, Waziri Mkuu wa zamani wa Misri
Ahmed Shafik,Waziri Mkuu wa zamani wa MisriPicha: picture-alliance/dpa

Maamuzi hayo yanaweza kubatilisha sheria za uchaguzi kwa msingi wa jinsi bunge linalodhibitiwa na Waislamu wa itikadi kali lilivyochaguliwa, yumkini kwa kutaka kuvunjwa kwa bunge hilo. Na mahakama hiyo pia inaweza kutengua sheria ambayo imepitishwa na bunge hapo mwezi wa April yenye kuwapiga marufuku maafisa waandamizi wa utawala wa Mubarak, kama vile Shafiq, kugombania urais.

Baraza hilo la mahakama ambalo linajulikana kuwa ni la makamishna wa Mahakama Kuu ya Katiba, ambapo maoni yao sio lazima yawe yametokana na sheria, tayari limeashiria namna itakavyotowa hukumu yake. Baraza hilo liko dhidi ya bunge linalodhibitiwa na Waislamu wa itikadi kali.

Shirika la habari la taifa, MENA, limesema kwamba repoti ya makamishna wa Mahakama Kuu ya Katiba imeeleza kwamba vifungu vya sheria ya bunge viko kinyume na katiba.

Kwa mujibu wa shirika hilo la MENA, repoti ya makamishna pia imesema kwamba sheria ya kumtenga mtu kisiasa ambayo inamuathiri Shafiq pia inakwenda kinyume na katiba, kwa vile inamuadhibu mtu binafsi kwa misingi ya kushika madaraka ya serikali na sio kwa ushahidi wa kuhusika na rushwa.

Mkuu wa Mahakama hiyo Kuu ya Katiba ni Farouk Soltan, aliyechaguliwa wakati wa enzi ya Mubarak, ambaye pia anaongoza tume ya uchaguzi wa rais yenye kusimamia uchaguzi wa urais.

Julai mosi rais mpya kukabidhiwa madaraka

Baraza la kijeshi ambalo limekuwa likiitawala Misri tokea mwaka jana linatazamiwa kukabidhi madaraka kwa rais mpya hapo tarehe Mosi Julai, na ushindani wa Shafiq na Mursi unatowa nafasi kwa wapiga kura kuchaguwa kati ya alama ya utawala wa Mubarak usiokuwa na mafungamano na dini na kundi la Wasilamu wa itikadi kali ambalo amelipiga marufuku.

Katika juhudi za kukwamisha majaribio ya kuwania nafasi ya urais kwa wasaidizi wakuu wa Mubarak ,bunge hapo tarehe 12 mwezi wa April lilidhinisha sheria ambayo iliwavua haki za kisiasa wale wote waliokuwa na nyadhifa za juu katika serikali na chama tawala wakati wa muongo wa mwisho wa utawala wa Mubarak.

Mohammed Morsi ,mgombea kutoka chama cha udugu wa Kiislamu
Mohammed Morsi, mgombea kutoka chama cha Udugu wa KiislamuPicha: picture-alliance/dpa

Wabunge wa itikadi za Kiislamu

Wabunge wa itikadi kali za Kiislamu awali walirasimu sheria hiyo kukabiliana na jaribio la makamo wa rais, Omar Suleiman, kuwania urais ambaye baadae alizuiliwa na kamati ya uchaguzi kwa sababu mbali mbali.

Kamati hiyo ya uchaguzi ilimzuwiya Shafiq, lakini baade ilimrudisha kwenye kinyan'ganyiro hicho baada ya kukata rufaa, akisubiri hukumu iwapo sheria iliopitishwa mwezi wa April ilikuwa halali. Iwapo mahakama kuu ya katiba itafuata maoni yalitolewa jana na baraza la mahakama, Shafiq ataruhusiwa kuendelea kugombea urais.

Mwandishi:Mohamed Dahman/Reuters

Mhariri: Miraji Othman