1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mishahara ziada ya wabunge ijulikane

Oummilkheir5 Julai 2007

Uamuzi wa korti kuu ya katiba kuhusu mishahara ya wabunge na kisa cha kutumiwa madege zaidi ya Tornado wakati wa mkutano wa kilele wa G8

https://p.dw.com/p/CHSV

Mada moja imehodhi magazeti ya Ujerumani hii leo:Uamuzi wa korti kuu ya katiba unaowataka wabunge wafichue mishahara ziada wanayopata.Mishahara hiyo sasa itachapishwa.Kwa namna hiyo majaji wa korti kuu ya katiba wameamua dhidi ya hoja za wabunge tisaa waliotuma mashtaka yao.Spika wa bunge la shirikisho Lammert anataka kuanzia sasa kuchapisha data alizonazo.Mbali na mada hiyo wahariri wa magazeti ya Ujerumani wamechambua pia siri zinazotokana na kutumiwa madege ya kivita ya Tornado,mkutano wa kilele wa viongozi wa mataifa tajiri kviiwanda G8 ulipoitishwa mjini Heligendamm.Kwanza lakini tuuangalie uamuzi wa korti kuu ya katiba.Na gazeti la TAGESZEITUNG la mjini Berlin linaandika:

Kiti cha bunge kinafungamana bila ya shaka na nafasi nyingi tuu ambazo raia wa kawaida hazipati.Kwa hivyo ni sawa kabisa kama mbunge atakua na wajib ambao wengine hawanao.Wapiga kura wanastahiki kuarifiwa, mbunge,mbali na mshahara wake, fedha zake nyengine anazipata vipi?Habari kama hizo zinasaidia kumulika maamuzi ya kisiasa .Kwa mfano,mbunge anapotumika kama mshauri na mwanachama wa baraza la usimamizi la shirika la nishati,hatokosa kupigania sera zinazolipendelea shirika hilo.Sio lazma imaanishe kwamba hoja zake hazina nguvu.

Gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG linaandika:

„Sio kwamba sheria inawakataza wabunge kufanya kazi ziada.Hasha.Sheria inalazimisha tuu kwamba mishahara ziada ijulikane,japo kama ni makadirio.Hiyo inamaanisha kuwepo hali ya uwazi-na huo ndio msingi wa demokrasia, kwa hivyo si uamuzi uliofurutu ada.Ni sawa kwamba mishahara ziada inaweza kudhamini hali ya kujitegemea,lakini inaweza pia kua ufunguo wa pingu kwa kundi linalohusika.Kwa hivyo suala hapa ni kiwango na lengo la shughuli ziada na muhimu zaidi ni kuhakikisha mpiga kura anaarifiwa.”

Gazeti la GENERAL ANZEIGER la mjini Bonn linajiuliza:

„Kanuni za uwazi zilizoanzishwa mwaka 2005 zinaweza kuwafanya wale wanaofanya kazi za kujitegemea,wasiwajibike ipasavyo bungeni na kwa namna hiyo kupalilia mtindo wa wabunge wachache tuu kukalia viti vya bunge ,huku mguu wa pili wa wabunge hao ukikutikana kwengineko.Wabunge, wale wanaotokea shule na kuingia bungeni,wanaweza kuachwa kando.Anaefichua anapokea kiasi gani, anasababisha mashindano na wivu sio tuu kwa milki aliyo nayo bali pia kuelekea suala kwa kiasi gani anaweza kuaminika au kwa kiasi gani watu wanaweza kushindana nae.“

Hatimae gazeti la SÜDKURIER la mjini KONSTANZ linaandika:

„Mahakimu wa mjini Karlsruhe kwa kupitisha uamuzi kuhusu mishahara ziada ya wabunge, wamejibu suala moja la kimsingi nalo ni kuhusu umuhimu wa masilahi ya kila mmoja mbele ya wananchi kwa jumla.Mbunge ambae kuanzia sasa analazimika kujieleza vipi anajipatia fedha alizo nazo,anakumbushwa na korti kuu ya katiba, jukumu alilo nalo mbele ya demokrasia.Ni sawa kabisa,tena uamuzi huo ulikua upitishwe tangu zamani.Kwasababu kwa miongo sasa mabishano yamekua yakiendelea kuhusu mada hii.Na kimsingi ni haki ya kila mmoja kujua kwamba kuna baadhi ya wanasiasa wanaishi kwa mishahara yao kama wabunge tuu na wengine ambao mishahara hiyo si chochote kwao.

Mada ya pili na ya mwisho magazetini inahusu kishindo kilichozuka hivi karibuni kuhusu kutumiwa madage chapa ya Tornado katika mkutano wa kilele wa G8.Waziri wa ulinzi Franz Joseph JUNG anataka kufafanua imekwenda kwendaje mpaka madage hayo yakatumika.Kabla ya hapo ilitajikana kwamba madege matano zaidi ya Tornado yalitumika kuchungua hali ya mambo mkutano wa viongozi wa mataifa tajiri kiviwanda G8 ulipoitishwa mjini Heiligendamm-kinyume na ilivyoruhusiwa.