Misafara ya malori ya NATO kuelekea Afghanistan yaanza Pakistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Misafara ya malori ya NATO kuelekea Afghanistan yaanza Pakistan

Hatimaye malori yakiwa yamebeba shehena za Jumuiya ya Kujihami ya NATO yameondoka Pakistan leo katika safari ya kuelekea Afghanistan, hatua inayomaliza mkwamo uliodumu kwa miezi saba.

Magari yaliyobeba shehena za NATO yakiondoka Pakistan kuelekea Afghanistan.

Magari yaliyobeba shehena za NATO yakiondoka Pakistan kuelekea Afghanistan.

Maafisa wa forodha nchini Pakistan wanasema kuwa magari hayo yalivuka mpaka wa Chaman kuelekea kusini mwa Afghanistan, ikiwa ni hatua muhimu baada ya Marekani kumaliza mzozo uliokuwepo baina yake na nchi hiyo, kufuatia kitendo chake cha kufanya mashambulizi ya anga yaliyowauwa Wapakistan 24 mwezi Novemba mwaka jana.

Afisa Imran Raza anayeshughulika na masuala ya forodha nchini humo anasema kuwa walipokea amri ya kuruhusu magari hayo kupita hapo jana ingawa wakati huo maafisa wa usalama walikuwa bado hawajapata melekezo. Leo wamepewa maelekezo na ndio maana magari hayo yameweza kuendelea na safari.

Ruhusa ya shehena ya NATO kuendelea na safari ya Afghanistan inakuja ikiwa ni siku mbili baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Hillary Clinton, kutimiza matakwa ya Pakistan kwa kuomba radhi. Clinton alimwambia Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Pakistan Hina Rabbani Khar kuwa Marekani inaomba radhi kwa kitendo hicho cha kuuuwa watu.

Hasira za Pakistan

Msafara kutoka Pakistan ukielekea Afghanistan.

Msafara kutoka Pakistan ukielekea Afghanistan.

Pakistan ilifunga mpaka wake kwa hasiramara moja baada ya kutokea tukio hilo na hivyo kuzikwamisha safari za shehena za NATO kueleleka Afghanista. Katika kipindi chote hicho serikali ya Rais Barack Obama ilikataa kutii matakwa hayo ya Pakistan ambapo NATO ilikijutia kitendo hicho cha mauwaji.

Nchi wanachama wa Jumuiya ya NATO zililazimika kupeleka shehena zao Afghanistan kupitia njia ya kaskazini ambayo si rahisi kupitika na hivyo kusababisha mchakato huo kuwa mgumu. Gharama ziliongezeka mara mbili na nusu zaidi ya ile ambayo wanaipata wakipita katika njia iliyofungwa na Pakistan.

Makamanda wa jumuiya hiyo walisema kuwa kitendo cha Pakistan kufunga njia hakikukwamisha shughuli zao Afghanistan, ambako vikosi vya Nato vinapigana na kundi la Taliban kwa miaka 10 sasa. Lakini walikubali kuwa kitendo hicho kingeweza kuwapa tabu wakati vikosi vya kulinda amani vya nchi za NATO vitakapoanza kuondoka mwishoni mwa mwaka 2014.

Mwanzo mpya?

Malori ya bidhaa za NATO kutoka Pakistan kwenda Afghanistan.

Malori ya bidhaa za NATO kutoka Pakistan kwenda Afghanistan.

Makubaliano haya ya kufungua njia baina ya Pakistan na Marekani huenda yakaenda mbali zaidi hapo baadae na hivyo kupunguza hali ya kuhasimiana. Tatizo litabaki kwa shutuma za NATO kuwa Pakistan inawaruhusu wanamgambo wenye kambi zao nchini humo kufanya mashambulizi Afghanistan.

Wakati huohuo, Pakistan inaituhumu Marekani kuingilia uhuru wa mipaka yake kwa kufanya mashambulizi ya anga ya mara kwa mara dhidi ya wanamgambo katika eneo la kaskazini-magharibi linalokaliwa na kabila la Pashtun.

Katika makubaliano hayo, Pakistan imeombwa msamaha kama ilivyotaka, lakini pia nyao imekubali kuachana na madai ya kuongeza kiwango cha ushuru kwa magari hayo.

Mwandishi: Stumai George/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com