Migomo yaendelea Ufaransa
21 Oktoba 2010Paris.
Safari za anga , treni na barabara zimeendelea kuvurugika nchini Ufaransa jana Jumatano, ikiwa ni siku ya saba ya maandamano pamoja na hatua ya vyama vya wafanyakazi kufanya migomo dhidi ya mipango ya serikali kupandisha umri wa wastani wa kustaafu kufikia miaka 62. Baada ya tahadhari ya uharibifu wa muda mrefu wa uchumi nchini humo, rais Nicolas Sarkozy ameamuru polisi kuondoa vizuwizi vyote katika mabohari ya kuhifadhia mafuta, hatua ambayo imesababisha kufungwa kwa karibu theluthi ya vituo vya kuuzia mafuta. Waziri wa mambo ya ndani Brice Hortefeux ameidhinisha hatua kali dhidi ya watu wanaogoma. Watu waliofanya ghasia wamechoma moto magari na kupora vitu madukani katika miji kadha nchini ufaransa jana Jumatano. Polisi wameripoti kuwa wamewakamata kiasi watu 1,500 tangu maandamano kuwa ya ghasia.