1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Michuano ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya.

Mohammed AbdulRahman22 Novemba 2006

Mashindano ya ligi ya vilabu bingwa barani Ulaya-Champions League- mashindano hayo yanaendelea leo, wakati Celtic na AC Milan zikiwa tayari zimeshajihakikishia nafasi ya kucheza duru ya timu 18 za mwisho. Mabingwa wa Ujerumani Bayern Munich wataumana punde na Spartak Mosko ya Urusi, wakati Werder Bremen ikitoana jasho na Chelsea ya Uingereza.

https://p.dw.com/p/CHcv
Oliver Kahn anatarajiwa kuwa uwanjani leo kulinda lango la Bayern Munich.
Oliver Kahn anatarajiwa kuwa uwanjani leo kulinda lango la Bayern Munich.Picha: picture-alliance / dpa

Celtic ya Scotland na AC Milan ya Itali zimejishajihakikishia nafasi ya kuingia duru ya timu 16 za mwisho baada ya matokeo ya mechi zao jana. Celtic iliwalaza mabingwa wa Uingereza Manchester United bao 1-0 mjini Glasgow katika mchezo ambao ungelimalizika sare kama si mshambuliaji wa Manchester United Saha kukosa mkawaju wa Penalty katika dakika ya 90 ya mchezo. Sasa MANU kama wanavyojulikana na mashabiki wao nyumbani watalazimika kujiepusha na izara wakati watakapoumana nyumbani na Benfica ya Ureno Desemba 6.

Celtic ndiyo inayoongoza kundi hilo kwa pointi 9 ikifuatiwa na Manchester United ikiwa na pointi 9 lakini kasoro ya magoli, na Benfica pointi 7 baada ya kuifunga jana Copehagen ya Denmark yenye pointi 4, mabao 3-1. AC Milan pamoja na kufanikiwa kusonga mbele, ilishindwa katika mchuano wake na AEK Athens ya Ugiriki bao 1-0 , bao lililopachikwa na Julio Ceasar katika dakika ya 32.

Katika mechi nyenginev za jana Hamburg iliyaaga mashindano ilipofungwa 3-1 na Arsenal huku Kocha wa timu hiyo ya Uingereza Arsene Wenger akisema licha ya nahodha Thiery Henry kupewa kadi ya tatu ya njano katika mashindano hayo na kuwa nje ya pambano lijalo dhidi ya Porto ya Ureno,ana imani timu yake itafanikiwa kusonga mbele. Arsenal ambayo itahitaji kwenda sare tu katika mechi yake ijayo na Porto inaongoza kundi hilo ambalo linaishirikisha pia CSKA Mosko ya Urusi.

Baada ya matokeo ya jana Celtic na AC Milan zinaungana na timu nyengine zilizofanikiwa tangu awali kucheza katika kundi la timu 16 za mwisho, ambazo ni Bayern Munich, Liverpool ya Uingereza, Olympic Lyon ya Ufaransa , Real Madrid na Valencia zote za Uhispania na PSV Eindhoven ya Uholanzi .

Bayern leo inaumana na Spartak ya Urusi katika kundi B, wakati kundi la kwanza ni mchuano kati ya Werder Bremen pia ya Ujerumani na Chelsea ya Uingereza, unaosubiriwa kwa hamu. Chelsea ndiyo inayoongoza kundi hilo ikifuatiwa na Bremen, Barcelona ya Uhispania na Levski Sofia ya Bulgaria.

Wakati huo huo, polisi ya Ujerumani imesema iliugundua na kuuvunja mpango wa wahuni wa soka wa Kiingereza na Kijerumani wa kuandaa mapambano na vurugu jana mjini Hamburg. Polisi ilisema kiasi ya wajerumani 100 na waingereza 150 waliowasili kwa mchuano huo wa leo kati ya Chelsea na Bremen, walitiwa nguvuni.