Michuano ya ligi kuu mwishoni mwa wiki | Michezo | DW | 15.10.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michuano ya ligi kuu mwishoni mwa wiki

Mbali na michuano ya ligi kuu ya Ujerumani inayoingia siku yake ya 9,tutafika pia Uengereza ambako Liverpool inachuana na Manchester United-Haile Gebrselassie kutimka katika mbio za marathon za Tokyo mwakani.

default

Mlinzi wa lango la Dortmund,Roman Weidenfeller (kati) akitoa mpira hapo jana

Tuanzie lakini nchini Ujerumani ambako Dortmund wakisalia kumi uwanjani walionyesha ustadi mkubwa na kuondoka ushindi dhidi ya Werder Bremen jana usiku na kwa namna hiyo kupanda nafasi ya pili -japo kwa muda-ya matokeo jumla ya michuano ya ligi kuu ya Ujerumani Bundesliga,nyuma ya Bayern Munich inayoikaribisha Hertha Berlin,hii leo,mnamo siku ya 9 ya michuano ya ligi kuu.

Wiki mbili baada ya kuitwanga Augsburg manne kwa yai,watoto wa kocha Jürgen Klopp wameorodhesha ushindi wao wa tano kwa msimu huu na kuitangulia Werder Bremen kwa tofautri ya goli moja tu,huku kila timu ikiwa na pointi 16.Wamedhihirisha kwa mara nyengine tena watoto wa Dortmund, tamaa yao ya kutetea taji la ubingwa lililowaponyoka huku huku mwaka jana walipoondolewa kwa magoli sawa na hayo-mbili bila.

Ivan Perisic anaetokea Kroatia,mshindi wa goli la mwanzo la Dortmund mnamo dakika ya 42,alipewa kadi yake ya pili ya manjano dakika nne baadae.Kadi hiyo haikuwavunja nguvu watoto wa Dortmund.Patrick Owomoyela alilitumia vurumai lililozuka na kupachika goli lao la pili,mnamo dakika ya 72 dhidi ya timu yake ya zamani-akidhihirisha amerejea upya uwanjani baada ya kukaa nje kwasababu ya maumivu.

"Kadi ya pili nyekundu,muda mfupi baada ya mapumziko,ilitutia uchungu,lakini watoto wamecheza kwa moyo mkubwa na ushindi wetu ni wa haki:" amesema kocha Jürgen Klopp baada ya ushindi huo wa tatu mfululizo na kabla ya kufunga safari jumatano ijayo hadi Piree kwa mchuano wa kombe la vilabu bingwa Champions League dhidi ya Olympiakos.

Kijuu juu,Bayern Munich haina cha kuhofia itakapoikaribisha uwanjani jioni hii Hertha Berlin,kabla ya kufunga safari kuelekea Neaple:Ulinzi wake ni madhubuti,hakuna aliyeweza kupenya tangu dakika 1018 zilizopita na kocha Jupp Heynckes anajivunia wachezaji wake kabambe pamoja na kurejea uwanjani Frank Ribéry baada ya kujeruhiwa mguu.Cha kuzingatia ni kwamba vijana wa mji mjkuu si wa kudharauliwa seuze tena wameshawaondoa patupu watoto wa Cologne walipowachapa tatu bila.Na zaidi ya hayo kocha wa Hertha Berlin Markus Babbel atataka kuranda nyumbani alikotokea.

Markus Babbel amewatolea mwito wachezaji wake na kusema:

"Tunabidi tuonyeshe utayarifu wa kwenda mbio,tushambulie na zaidi kuliko yote tusiwe na woga.Na kila mmoja wetu anabidi ajitolee zaidi,baadae tutaona matokeo yake yatakuwa ya aina gani."

Hawana cha kupoteza,lakini pia hakuna asiyeweza kushindwa anahoji Markus Babbel huku mchezaji wake Christian Lell akiongezea "anazijua mbinu zote za Ribery,aliyewahi kucheza pamoja nae hadai msimu wa kiangazi mwaka jana.

Bayer Leverkusen,inayoshikilia nafasi ya tisa inajiandaa kwa michuano ya Ulaya itakapoikaribisha Valence jumatano ijayo,kwa kufunga safari hadi Mönchengladbach,timu iliyofanikiwa -kwa mshangao wa wengi-kupanda hadi daraja ya tatu ya matokeo jumla ya ligi kuu.

Stuttgart na Hoffenheim zitajaribu kujitenganisha,-kila moja ina pointi 13 huku Schalke inayoshikilia nafasi ya nne kwa pointi 15 ikiwategemea wapachika magoli wake Raul na Klaas-Jan Huntelaar kuishinda Kaiserslautern na kupanda pengine nafasi ya pili pindi Mönchengladbach wakishindwa.l

Lengo hilo hilo wamejiwekea Hannover inayokamata nafasi ya tano na ambayo kesho ijumapili itateremka uwanjani mjini Cologne katika wakati ambapo miongoni mwa timu zinazoburura mkia,Freiburg inayokamata nafasi ya 15 itawakaribisha watoto wa Hambourg jumapili,waliojipatia kocha mpya Thorsten Fink.

England Fußball Fans Liverpool

Mashabiki wa Liverpool

Na sasa tueleke Uengereza ambako michuano ya kuania ubingwa wa ligi kuu inaingia siku yake ya nane hii leo.Pambano linalosubiriwa kwa hamu likiwa lile kati ya Liverpool na Manchester United.

Mabingwa watetezi, wanaoshikilia rekodi ya kuvikwa mataji 19 dhidi ya 18 ya wapinzani wao, wanakabiliwa na hatari ya kutetereka kileleni mwa ligi guu na kuwaachia usukani Manchester City,watakapoteremka uwanjani jioni hii dhidi ya Liverpool wanaozidi kupanda.

Manchester United ilivunja moyo hapo awali ilipomaliza sare dhidi ya Stoke City inayoshikilia nafasi ya nane ya matokeo jumla ya ligi kuu ya Uengereza na pia Bale ya Uswisi katika michuano ya Champions League na baadae kushinda chupu chupu ddhidi ya timu iliyopanda daraja Norwich.

Kinyume chake Liverpool inajivunia ushindi mara mbili mfululizo-mmojawapo ukitokana na pambano dhidi ya Everton iliyokandikwa mawili kwa bila na Liverpool.

Wakikamata nafasi ya tano,The Reds pindi wakiwashinda Manchester United watakuwa na pointi tatu tu nyuma ya majirani zao.

Wayne Rooney atawashughulisha wengi,hasa baada ya kuzuwiliwa na UEFA asicheze michuano mitatu baada ya kumpiga teke mchezaji wa Montenegro alipokuwa akicheza na timu ya taifa.

Adhabu hiyo itamzuwia mchezaji nyota huyo kuranda katika rauni za mwanzo za kombe la Ulaya mwezi June mwakani.

Dakika chache baada ya firimbi ya mwisho kulia huko Anfield,Manchester City watateremka katika uwanja wa Aston Villa,wakijiwekea matumaini ya kuibuka na ushindi ili kuwaondowa kileleni The Red Devils pindi wakiteleza.

Chelsea inayojikuta pointi tatu nyuma ya timu hizo mbili zinazoongoza inapewa nafasi nzuri ya kuishinda Everton.Pambano jengine linalosubiriwa kwa hamu ni lile la kesho kati ya Newcastle inayoshikilia nafasi ya nne ya matokeo jumla ya ligi kuu na ambayo haijawahi kushindwa hata mara moja msimu huu na Tottenham,iliyoshinda mecho zake zote nne za amwisho.

ARCHIV - Der Äthiopier Haile Gebrselassie (l) jubelt am 25.09.2000 im Olympiastadion von Sydney beim Zieleinlauf im Finale über 10 000 m der Männer über seine Goldmedaille. Rechts kommt der Kenianer Paul Tergat als Zweiter ins Ziel. Haile Gebrselassie hat mit seinem abrupten Rücktritt die Leichtathletik-Welt geschockt. «Ich trete zurück, lasst mich einen anderen Job machen», sagte Gebrselassie am Sonntag (07.11.2010) nach seiner Aufgabe beim New-York-Marathon. Foto: Oliver Multhaup +++(c) dpa - Bildfunk+++

Haile Gebrselassie aliposhinda mbio za mita elfu kumi huko Sydney september 25 mwaka 2000

Riadha:

Mwendaji mbio mashuhuri Haile Gebrselassie wa Ethiopia,kiwa ziarani nchini Afrika kusini,amesema anapanga kushiriki katika mbio za marathon za Tokyo Japan February 26 mwakani.Mwanariadha huyo wa Ethiopia mwenye umri wa miaka 38 ambae rekodi yake ya dunia (saa mbili,dakika tatu na sekondi 59) imevunjwa kwa sekondi 21 na Patrick Makau wa Kenya katika mbio za Marathon za Berlin mwezi uliopita,anakabiliwa na ushindani mkubwa nyumbani.Anabidi aweke muda wa saa mbili na dakika tano kuweza kuchaguliwa kushiriki katika michezo ya Olympic ya mjini London hapo mwakani.

Mshindi wa mbio za Olympik za mita elfu kumi mnamo mwaka 1996 na 2000 atabidi adhihirishe uwezo wake katika mbio fupi za Marathon zitakapofanyika huko Birmingham.

Na hatimae maafisa wanne wa shirikisho la kabumbu la nchi za Amerika ya kaskazini,kati na nchi za Caribian wamezuwiliwa na shirikisho la kabumbu la kimataifa FIFA kutokana na kuhusika kwao na visa vya rushwa.Adhabu kali zaidi amepewa mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu la visiwa vya Uengereza-Virgin Islands Franka Pickering aliyezuwiliwa kwa muda wa miezi 18 na kutozwa faini ya Euro zaidi ya 400.

Hatua hizo zimepitishwa kufuatia mkutano uliofanyika mwezi May mwaka huu huko Port of Spain katika visiwa vya Trinidad na Tobago ambapo Mohammed bin Hammam wa Qatar anasemekana aliwahonga wanachama wa shirikisho la kabumbu la CONCACAF ili badala yake wampigie kura aweze kuchaguiliwa kuwa mwenyekiti wa shirikisho la kabumbu ulimwenguni-FIFA.

Mohammed bin Hammam amezuwilia maisha uanachama wake-mwenyewe lakini anakanusha madai hayo.

Mwandishi: Hamidou, Oumilkheir/ap,rtre,afp,SID

Mhariri: Martin,Prema

 • Tarehe 15.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12sc0
 • Tarehe 15.10.2011
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/12sc0