Uganda yapeta kuingia awamu ya makundi
16 Novemba 2015Baada ya mashambulizi mjini Paris , ushindani wa kiuhasama baina ya timu za taifa za Uingereza na Ufaransa utashuhudia ukurasa mpya wa maombolezi na ukimya katika uwanja wa Wembley kesho wakati timu hizo zitakapopambana.
Na kansela wa Ujerumani Angela Merkel na baraza lake la mawaziri kuhudhuria mpambano wa soka wa kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi kesho wakionesha mshikamano na watu wa Ufaransa.
Morocco na jamhuri ya kidemokrasi ya Congo zasonga mbele na kukata tikiti katika michuano ya makundi ya kukata tikiti za fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwaka 2018.
Yawezekana kuiondoa michezo ya riadha katika mashindano ya olimpiki kutokana na matumizi makubwa ya madawa ya kuongeza nguvu misuli , Doping ?
Kwa hayo na mengi mengine, jina langu ni Sekione Kitojo, nakukaribisha katika ukurasa huu wa michezo mwishoni mwa juma.
Michuano ya kirafiki barani Ulaya sehemu ya maombolezo kwa wahanga
Uingereza na Ufaransa zitashuhudia upinzani wao mkubwa ukitimiza miaka 92 katika soka kesho Jumanne lakini mpambano huo utashuhudia hali ya ukimya na utulivu mjini London katika uwanja wa Wembley wakati timu hizo zitakapopambana na timu hizo zitaungana katika kuonesha mshikamano siku nne baada ya mashambulizi ya kigaidi mjini Paris.
Mashambulio ya Ijumaa yamegusa hususan kandanda kwa karibu, baada ya washambuliaji watatu wa kujitoa muhanga kujiripua nje ya uwanja wa stade de France wakati Ufaransa ikicheza na Ujerumani.
Binamu yake mchezaji wa kati wa timu ya Ufaransa Lassana Diarra ni mmoja kati ya watu 129 waliouwawa , wakati dada yake mchezaji mwenzake Antoine Griezmann alinusurika bila madhara yoyote kutoka katika shambulio hilo katika ukumbi wa burudani wa Bataclan mjini Paris.
Lakini shirikisho la kandanda la Ufaransa FFF, limesisitiza kwamba mchezo huo wa kesho uendelee na kwa sasa unaonekana kama fursa ya kuonesha mshikamano, na huku kampeni katika mitandao ya kijamii inawahimiza mashabiki wa Uingereza kujiunga na kuimba wimbo wa taifa la Ufaransa "La marseillase" , kabla ya mchezo huo kuanza.
"Mchezo huo utakuwa na kila ushindani, lakini pia utakuwa unatoa ishara kwamba ulimwengu wa kandanda uko pamoja dhidi ya mauaji," amesema kocha wa Uingereza Roy Hodgson.
Wakati huo huo kansela Angela Merkel wa Ujerumani na baraza lake la mawaziri watahudhuria mchezo wa kirafiki kati ya Ujerumani na Uholanzi mjini Hannover kesho ili kuonesha mshikamano na wahanga wa shambulio la kigaidi mjini Paris.
Shirikisho la kandanda la Ujerumani DFB lilifikiria kuufuta mchezo huo wa kirafiki mjini Hannover , lakini likaamua kuendelea na mchezo huo ili kutoa ujumbe wa wazi wakati Ufaransa itapambana na Uingereza usiku huo mjini London.
Rais wa muda wa shirikisho la kandanda la Ujerumani Reinhard Rauball amesema ujumbe ni wazi: "hatutatishwa na ugaidi."
Kikosi cha Ujerumani kupatiwa ulinzi zaidi Euro 2016
Maafisa wa kandanda nchini Ujerumani , wakati huo huo watafanya mapitio ya usalama katika michuano ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2016 nchini Ufaransa kufuatia mashambulizi hayo ya kigaidi mjini Paris.
Rais mwingine wa muda wa shirikisho hilo la DFB rainer Koch ameliambia gazeti la Bild leo Jumatatu kwamba shirikisho hilo litatafakari hatua gani nyingine zichukuliwe.
Kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani kililazimika kulala uwanjani Stade de France kaskazini mwa Paris baada ya pambano lao la kirafiki dhidi ya Ufaransa siku ya Ijumaa.
Mashambulizi hatari mjini Paris hayatadhuru nafasi za mji huo kuwa mwenyeji wa michezo ya majira ya joto ya Olimpiki mwaka 2024, amesema rais wa kamati ya kimataifa ya Olimpiki IOC Thomas Bach leo.
Mji ambao utakuwa mwenyeji wa mashindano ya mwaka 2024, utajulikana mwaka 2017 lakini Bach anaamini mashambulio mjini Paris , mji ambao umetangazwa kuwa moja na miji inayowania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, hayatakuwa na mwelekeo wowote katika matokeo ya kura itakayopigwa na kamati hiyo ya olimpiki.
Argentina ni kufa kupona dhidi ya Columbia
Wakati dunia nzima ikisimama pamoja na Ufaransa baada ya mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu wasio na hatia mjini Paris siku ya Ijumaa , mapambano ya kandanda duniani kote yanafanyika.
Kocha wa Argentina Gerardo Martino amesema mpambano wa kuwania kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi , inalazimika kushinda licha ya kikosi chake kukumbwa na wingi wa majeruhi, baada ya timu hiyo kuambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Brazil iliyokuwa na wachezaji 10 uwanjani baada ya David Luiz kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Argentina inapambana na Colombia kesho katika mchezo wa kuwania kufuzu katika fainali za kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Hungary yafanikiwa kucheza mashindano makubwa baada ya miaka 30
Hungary imemaliza kipindi cha miaka 30 ya kusubiri kufuzu katika fainali za mashindano makubwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1986 ilipofikia fainali za kombe la dunia , baada ya kuishinda Norway kwa mabao 2-1 jana Jumapili na kushinda kwa jumla ya mabao 3-1 katika pambano la mchujo kwa ajili ya fainali za kombe la Ulaya 2016.
Kocha wa Hungary Mjerumani Bernd Storck akisaidiwa na Andreas Mueller amelifikisha taifa hilo katika fainali za mwakani za kombe la mataifa ya Ulaya. Storck amesema tulifanya mazowezi magumu na kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu.
"Na niliwaamini, niliwaona wakifanya mazowezi, tulifanya mazowezi vizuri sana, wamejifunza mengi, walitaka kujifunza mengi, niliwaambia, chezeni kwa kujiamini, chezeni bila woga, na kisha mtafanikiwa. Na nafikiri wamefanya hivyo leo. Leo mmeona. Kiwango kilikuwa cha kushangaza, nafikiri , ilikuwa kiwango cha ajabu, kile tulichokiona leo kwa timu yetu."
Mgombea wa kiti cha urais wa FIFA Nakhid akata rufaa
Na katika sakata la kuwania kugombea kiti cha urais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA , mchezaji wa zamani wa kimataifa wa Trinidad na Tobago David Nakhid amekata rufaa katika mahakama ya juu ya michezo duniani kuhusiana na uamuzi wa kumzuwia kugombea urais wa shirikisho hilo lililokumbwa na kashfa la FIFA.
Chini ya sheria za uchaguzi za FIFA , Nakhid alihitaji uungwaji mkono kwa maandishi kutoka kwa vyama vitano vya taifa vya kandanda ili aweze kugombea katika uchaguzi utakaofanyika Februari 26 kutafuta mtu atakayechukua nafasi ya Sepp Blatter.
Amezuiwa kujiandikisha na kamati ya uchaguzi ya FIFA mwezi uliopita kwasababu chama kimoja kilitia saini barua ya kumuunga mkono Nakhid pamoja na mgombea mwingine.
Leo (16.11.2015)mahakama ya upatanishi yenye makao yake makuu nchini Uswisi CAS imesema Nakhid amekata rufaa dhidi ya uamuzi huo.
Uganda yapeta kuingia awamu ya makundi
Na katika bara la Afrika , Uganda imesonga mbele katika awamu ya makundi kwa ajili ya kuwania kufuzu kucheza katika kombe la dunia mwaka 2018 katika bara la Afrika.
Farouk Miya mwenye umri wa miaka 17 alipachika bao akiisaidia Uganda kuikandika Togo mabao 3-0.
Nahodha Geoffrey Massa alipachika mabao mengine mawili mjini Kampala na kuihakikishia Uganda kuingia katika awamu ya makundi kwa jumla ya mabao 4-0.
Zambia pia imesonga mbele kwa kuishinda Sudan kwa mabao 2-0 mjini Ndola.
Licha ya kuwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ililazimishwa sare ya mabao 2-2 nyumbani na Burundi na Morocco kupoteza mchezo wake kwa bao 1-0 dhidi ya Guinea ya Ikweta , timu hizo mbili zilizowahi kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia hapo nyuma zilitoka vifua mbele.
Guinea , iliyolazimika kucheza michezo yake katika mji wa Casablanca nchini Morocco dhidi ya Namibia kutokana na ugonjwa wa Ebola , ilishinda kwa mabao 2-0 ikiingia katika mchezo huo na ushindi wa bao 1-0 kutoka mchezo wa kwanza.
Kenya inakwenda Cape Verde kuwania nafasi hiyo katika mchezo utakaofanyika kesho , baada ya kuishinda timu hiyo ya visiwani kwa bao 1-0 mjini Nairobi Ijumaa.
Nayo Taifa Stars ya tanzania baada ya kuduwazwa na sare ya mabao 2-2 mjini Dar es Salaam dhidi ya Mbweha wa jangwani Algeria, imewasili mjini Algiers tayari kwa pambano lao la kuwania kuingia katika duru ya makundi kesho Jumanne.
Tanzania ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0 hadi mwishoni mwa kipindi cha pili walipoachia fursa hiyo adhimu na kuruhusu Algeria kurejesha mabao hayo mawili.
Kocha Boniface Mkwasa ana kibarua kigumu kuweza kuiwezesha timu hiyo kuingia katika awamu ya makundi licha ya kucheza vizuri katika kipindi cha kwanza na sehemu ya kipindi cha pili.
Makundi ya michuano ya CHAN yapangwa
Katika kinyang'anyiro cha kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani maarufu mashindano ya CHAN , timu zilizofuzu kwa michuano hiyo zimepangwa tayari katika makundi mjini Kigali jana.
Wenyeji Rwanda wamewekwa kundi moja na Morocco na Cote d'Ivoire. Wakati Rwanda haikushiriki katika michuano ya mchujo kwa ajili ya mashindano hayo , Wamorocco na Cote d'Ivoire walifanya vizuri katika kupata nafasi ya kucheza katika michuano hiyo itakayojumuisha timu 16.
Gabon ambayo inakamilisha kundi A litakalocheza michezo yake mjini Kigali , itakayofanyika kuanzia Januari 16 hadi Februari 7 , ilichukua njia tofauti kabisa hadi kufika hapo , ikishinda ugenini na kupoteza mchezo nyumbani dhidi ya Chad.
Makundi yamepangwa kama ifuatavyo ; Kundi A , Rwanda , Gabon, Morocco na Cote d'Ivoire , kundi B lina timu za Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo, Angola, Cameron na Ethiopia , Kundi C ni timu za ; Tunisia , Nigeria , Niger na Guinea na kundi D lina timu za Zimbabwe , Mali , Uganda na Zambia.
WADA yaja juu
Na kwa upande wa riadha , shirika la dunia la kupambana na matumizi ya madawa ya kuongeza nguvu misuli , Doping, WADA linatarajiwa kutoa uamuzi dhidi ya shirika la kupambana na Doping la Urusi katika mkutano muhimu mjini Colorado nchini Marekani siku ya Jumatano ambao utalenga kuweka mikakati kwa ajili ya vita dhidi ya Doping duniani.
Uongozi wa WADA utakutana kutathmini uchunguzi wao wa jopo lake huru , ambalo limefichua mpango mkubwa uliokuwa ukiungwa mkono na taifa wa Doping nchini Urusi ambao umeutumbukiza mchezo wa riadha katika mzozo mkubwa katika historia.
Shirika la vyama vya riadha duniani IAAF siku ya Ijumaa limewazuwia wanariadha wa Urusi kushiriki mashindano ya kimataifa, na kuweka ushiriki wa wanariadha hao katika michezo ya Olimpiki ya Rio de Janeiro katika mashaka .
Lakini pia shirikisho la kimataifa la vyama vya riadha IAAF linaweza kukabiliana na uwezekano ambao ni pamoja na kuondolewa kutoka katika mashindano ya Olimpiki wakati sehemu ya pili ya shirika la kupambana na Doping itakapowasilishwa, kwa mujibu wa mmoja wa makamishina wa tume huru ya shirikisho hilo.
Lakini uamuzi wowote wa kuisimamisha IAAF kutoshiriki katika michezo utahitaji kufanywa na kamati maalum ya kimataifa ya Olimpiki IOC.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / afpe / dpae
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman