1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Noa Bongo

Michezo ya redio iliyopita: Awamu ya Kwanza

Katika michezo hiyo ya Karandinga utaungana na vijana wapelelezi wanaopigania haki na ukweli.

Michezo hii ya redio inazungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili vijana barani Afrika.

Ungana na maafisa wa upelelezi katika kupigania ukweli na haki, huku ukipata mitizamo ya thamani kuhusu masuala nyeti. Chimbuko la Itikadi Kali-Ugaidi, Wawindaji Haramu, Unyakuzi wa Ardhi pamoja na Dawa Bandia – huu ni mfululizo unaojikita katika mzizi wa changamoto za sasa. Kuendeleza utamaduni wa ufanisi wa michezo ya redio ya Noa Bongo Jenga Maisha yako, hadithi ya Karandinga inatoa elimu na taarifa katika mfumo wa kuburudisha na kuwatia moyo wasikilizaji wafikirie wenyewe.

Mwandishi mashuhuri wa vitabu kuhusu uhalifu Mukoma wa Ngugi (Kenya) alichangia hadithi kuhusu Dawa Bandia. Helon Habila (Nigeria) na Andrew Brown (Afrika Kusini) walichangia katika mradi huu kama washauri.

Wasanii kutoka kote barani Afrika huiga hadithi kwa uhalisia na kuzipa uhai. Kila hadithi kati ya hadithi nne ina vipindi vinane vyenye urefu wa dakika 12. Vipindi vinapatikana kwa lugha ya Kiingereza, Kiswahili, Kifaransa, Kihausa, Kireno na Kiamharik. Hadithi ya Karandinga hurushwa hewani na DW pamoja na redio zaidi ya 250 washirika kote barani Afrika. Hujadiliwa pia katika majukwaa ya mitandao ya kijamii ya DW.

Karandinga: Chimbuko la Itikadi kali

Bomu linalipuka katika duka kubwa huko Kululaland na maafisa vijana wa polisi Jude na Brenda wanakishughulikia kisa hicho. Mara wanagundua lilikuwa shambulizi la kujitoa muhanga lililofanywa na msichana. Cha kushtusha zaidi ni utambulisho wake. Mshambuliaji anaitwa Zorah Kassim – amemaliza masomo yake ya chuo kikuu na anatokea kwenye familia tajiri. Kama mtoto wa kike wa mwanasiasa mwenye ushawishi, zipi huenda zilikuwa sababu zake za kufanya shambulizi hilo? Je, alilazimishwa kulifanya? Au alilifanya kwa hiari? Kwa kutumia mbinu tofauti na wakiyahatarisha maisha yao, maafisa Jude na Brenda wanafanya uchunguzi unaofichua taratibu zinazowafanya vijana kujiunga na makundi ya kigaidi. Lakini nia iliyomuongoza Zorah katika safari yake ya kuwa na msimamo mkali wa kidini ni tofauti kabisa.

Karandinga: Wawindaji Haramu

Maafisa wawili wa polisi, kesi mbili. Afisa wa upelelezi Allan anachunguza kuchomwa kisu kwa daktari wa wanyama Patrick. Mwenzake Carl anamsaka Bwana G – mkuu wa mtandao wa ujangili unaosababisha athari kubwa huko Bovu. Wanawaua kinyama: tembo, chui na faru na aina nyingi za wanyama hawa ziko hatarini kutoweka kabisa. Mfumo wa viumbe hai unaathirika pamoja na uchumi huku majangili wakijipatia mamilioni ya fedha. Allan anafuata njia nyingi lakini Carl anakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu hakuna anayefahamu utambulisho halisi wa Bwana G. Kwa mshangao wa maafisa hao wawili wa upelelezi, kesi inakamilika wakati barua ya usaliti inapogunduliwa katika vitu vya Patrick inayotishia kufichua utambulisho halisi wa Bwana G. Je muhanga wa mauaji alijua Bwana G ni nani hasa? Je huenda hii ndiyo sababu kwa nini alitakiwa kufa? Hatimaye ukweli unajitokeza kuwa wa kushangaza zaidi…

Karandinga: Unyakuzi wa Ardhi ya Chongwe

Chifu Awombo amekufa, mwili wake ukiwa katika ukingo wa mto katika shamba la maua. Je aliuliwa na mnyama wa mwituni kama serikali inavyotaka watu wa Chongwe waamini? Ama aliuawa? Wengi wanashuku hivyo kwa kuwa shamba la maua ya waridi liko katika ardhi iliyokuwa ikimilikiwa zamani na Chifu Awombo. Alipigania ili watu waweze kujikimu kimaisha kutokana na shamba hilo, badala ya kulikodi kwa wawekezaji wa kigeni. Inspekta Mwamto anakabiliwa na wakati mgumu kuamua iwapo ashikilie msimamo rasmi au azma yake ya kutafuta hasa kilichotokea. Ni afisa upelelezi Mweri ambaye hatimaye anaanza kuutafuta ukweli. Anagundua suala la ardhi ni gumu mno kuliko lilivyoonekana awali. Linarudi nyuma wakati wa enzi za uhuru na nyaraka haziko katika orodha sahihi. Kuna sio tu kugombania manufaa ya kiuchumi, bali pia hali iliyojaa hisia nyingi. Je, Mweri anaweza kutegau kitendawili cha kifo cha Chifu Awombo?

Karandinga: Dawa za Kutibu, Dawa za Kuua

Peter, mvulana wa familia tajiri na yenye ushawishi, anakufa kutokana na kiwango kikubwa mno cha dawa. Wakati uchunguzi unapobaini hakujiua bali aliwekewa sumu, maafisa watatu wa upelelezi Kalumba, Salamisha na Chokbank wanaanza uchunguzi wao na wanajiingiza katika wimbi la fitina, ulafi na machafuko. Kumtafuta muuaji wa Peter, lazima wajiingize katika ulimwengu wa dawa bandia ambako watu wanaonufaika na biashara hiyo huwatumia vibaya wagonjwa na waliopoteza matumaini. Dawa bandia huuzwa kwa bei nafuu na watu hawafahamu kuhusu kitisho cha dawa hizo kwa afya zao. Taarifa kadhaa zinawapeleka maafisa hao kwa daktari mashuhuri, mganga wa kienyeji, muuzaji dawa na mpaka kwa waziri wa afya. Kadri uchunguzi unavyoendelea, maisha ya wapelelezi hao yanatishwa zaidi ya mara moja. Hatimaye, wanafaulu kutathmini ni kwa kiwango gani Peter alijihusisha na biashara hii chafu na kwa nini alitakiwa kufa.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com