1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Michezo

Michezo ya Afrika Algiers

Michezo ya bara la afrika yakaribia kilele chake mjini Algiers wakati Marekani yaongoza orodha ya medali katika Pan American Games huko Rio.

Kinyan’ganyiro cha kombe la klabu bingwa barani Afrika kimewasili nusu-njia kikisaka bingwa mpya au wa zamani.Mabingwa Al Ahly ya Misri walikuwa na miadi ijumaa na Esperence ya Tunisia.Macho ya mashabiki yanaukodolea mpambano wa jumapili kati ya ASEC Abidjan ya Ivory Coast na Al Hilal ya Sudan.Al Hilal itakuwa nyumbani Khartoum.

Katika orodha ya watiaji mabao kabla firimbi kulia mwishoni mwa wiki hii, Cheikh Oumar Dabo wa JS Kabylie ya Algeria akiongoza kwa mabao yake 6.Nafasi ya pili akifuata Amine Latifi wa Esperence kwa mabao yake 5.

Kesho itakuwa “asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo- mkutano mjini Toronto,K anada.Jamhuri ya Czech inaumana na Argentina na ikirudi na kombe hilo Prague,nyumbani, imeahidiwa kitita cha dala 196.000.

Hii imetangazwa na shirikisho la kabumbu la Jamhuri ya Czech.Jamhuri ya Czech ilikata tiketi yake ya finali ya kesho iliipiga kumbo Australia kwa mabao 2:0 wakati mahasimu wao-Argentina, waliitimua Chile.

Kabla ya finali hii ya kombe la dunia la chipukizi chini ya umri wa miaka 20,Chile na Austria,zitaingia uwanjani kuania nafasi ya tatu.

Afrika iliwakilishwa katika kombe hili la dunia la vijana na Nigeria,Zambia,Kongo na Gambia.

Katika kinyan’ganyiro cha kombe la Asia,Saudi Arabia ina miadi kesho na Uzbekistan kukata tiketi ya finali ya kombe la mwaka huu la bara la Asia.Saudi Arabia kwanza iliikongoa meno Bahrein kwa mabao 4:0 na ina hamu sana kufuta madhambi ya kombe la Asia 2004 huko china, ilipotolewa duru za kwanza.

Tukigeukia dimba nchini Ujerumani wakati timu kadhaa zikijinoa kwa msimu mpya utakaoanza mwezi ujao,mashabiki wa Hamburg,kwa ukorofi wao karibuni tu waweza wakampoteza staid wa Ivory Coast Boubacr Sanogo na kumfanya ahamie kwa mahasimu wao jirani-Bremen au hata kwa mabingwa Stuttgart.

Baada ya Bremen kumuuza mshambulizi wao hatari Miroslav Klose kwa Bayern Munich,Bremen inasaka mshambulizi mwengine kujaza pengo lake.Sanogo,mwenye umri wa miaka 24, akikasirishwa na mashabiki wa klabu yake ya Hamburg wanaomzomea uwanjani.Hii imeathiri imani na ari yake ya mchezo.

Sanogo aliichezea Hamburg mara 31 msimu uliopita na kocha mpya wa Hamburg, Huub Stevens amempanga katika listi yake ya msimu mpya.Stuttgart,mabingwa wapya wa Bundesliga, wamekwisha jitolea kumkomboa Sango kwa kitita cha Euro milioni 2.5.

Hii ilikuwa mwaka jana wakati akiichezea Kaiserslauten. Hamburg lakini,inadai kurejeshewa kitita chake cha Euro milioni 3.8 walichotoa kumnunua Sanogo.

Nae kipa wa Bayern Munich,Oliver Kahn, alisema kati ya wiki hii, kuwa angependa kucheza finali ya mwaka ujao ya kombe la ulaya la UEFA na baadae kufunga virago na kustaafu.Kahn, alilinda lango la Bayern Munich juzi kwa muda wa dakika 45 ilipokomewa mabao 2:1 na Borussia Monchengladbach.

MICHEZO YA BARA LA AFRIKA:ALL AFRICA GAMES:

Michezo ya 9 ya bara la Afrika ikiendelea huko Algiers na kukaribia kilele chake, mashinda no ya riadha yalianza juzi jumatano kwa kishindo.

Wakenya na waethiopia wakapimana nguvu katika masafa marefu.Meseret Defar,bingwa wa olimpik wa Ethiopia katika masafa ya mita 5000 wanawake alitamba tena kinyume na bingwa wa olimpik wa Kenya katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi ambazo Kenya yadai ni mali yake.

Kenya ikitaka kuzoa medali zote 3,lakini Ethiopia haikuridhia.wakati wengi wakitazamia bingwa huyo wa Olimpik Ezekiel kemboi angetamba, ilikua willy Komen aliekuja kutoroka na ushindi akimuachia medali ya fedha mwenzake Ezekiel.Medali ya shaba ikaenda kwa muethiopia Naham Mesfin.

Katika mita 5000 wanawake,Defar ambae pia ni bingwa wa rekodi ya dunia alimpiku mwenzake Meselech Melkamu aliebidi kuridhika na medali ya fedha huku ile ya shaba ikienda kwa Silvia Kibet wa Kenya .

Afrika kusini ilitoroka na medali ya dhahabu katika kuchupa mara tatu-triple jump.Yamile Aldama ndie mshindi alipochupa mita 14.46.

Michezo ya pan American Games –inaendelea pia mjini Rie de Jeneiro,Brazil.Miongoni mwa changamoto za msisimko ni riadha,baseball na hata volleyball.Marekani, kabla mwishoni mwa wiki hii, ikielekea kutia kikapuni jumla ya medali 100 ikifuatwa nafasi ya pili na Cuba am,bayo rais wake Fidel Castro anaeugua amekuwa akiangalia mashindano hayo kwa hamu kuu.Mzee Castro amesema kwamba jinsi alivyoshughulika kuangalia pan American games kwa shauku kubwa, akisahau kula dawa zake.

Mbio za baiskeli za tour de France zilizoanza mapema mwezi huu huko London,zimetia tena for a kwa vichwa vya habari vya madhambi ya doping-matumizi ya madawa kutia nguvu.Kati ya wiki hii maji yalipozidi unga, vituo 2 vya TV vya Ujerumani-ZDF na ARD viliamua ghafula kuacha kutangaza mashindano hayo.

Muendeshaji-baiskeli wa kijerumani Patrik Sinkiewitz,aligunduliwa na madhabi hayo.Kabla ya hapo waendeshaji wengi baiskeli wa timu ya T-Mobile na watangulizi wao Telekom waliungama madhambi ya doping.

Hii ikapelekea serikali ya Ujerumani nayo kuarifu kwamba inachunguza kwa makini visa vya hivi punde vya madhambi ya doping katika mbio za baiskeli na ikawataka viongozi wa mchezo huu warekebishe mambo ama sivyo,watachukua hatua. Wametakiwa kufanya hivyo kabla ya mbio za baiskeli za Septemba mwaka huu huko Stuttgart,kusini mwa Ujerumani.

 • Tarehe 20.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHbd
 • Tarehe 20.07.2007
 • Mwandishi Ramadhan Ali
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHbd