Michezo mwishoni mwa juma
26 Julai 2010Real Madrid yasema adios kwa Raul aliyeitumikia timu hiyo ya mjini Madrid kwa muda wa miaka 18,
Mashindano ya ubingwa wa riadha ya bara la Ulaya kuanza kesho Jumanne,
na huko katika bara la Afrika mashindano ya riadha ya ubingwa wa Afrika kuanza Jumatano, nchini Kenya.
Kwa hayo na mengineyo nasema karibuni:
Real Madrid imethibitisha kuwa nahodha wake na pia mpachika mabao maarufu Raul Gonzalez, ataiacha mkono klabu hiyo maarufu leo Jumatatu baada ya kuitumikia kwa muda wa miaka 16 mfululizo na huenda atahamia katika klabu ya Ujerumani ya Schalke 04.
Raul ameichezea Real tangu mwaka 1994, ameshinda ubingwa wa ligi ya Hispania, La Liga mara sita pamoja na kombe la ligi ya mabingwa mara tatu katika wakati wake na vigogo hivyo vya soka nchini Hispania.
Amepachika mabao 323 katika mara 740 alizoingia uwanjani na timu hiyo. Mchezaji mwenzake Gutti , akiwa nae ni matokeo ya mfumo wa timu za vijana katika klabu hiyo ya Real na ambaye alinza kuichezea timu hiyo mwaka 1995, amesema mapema jana Jumapili kuwa anaondoka nae katika timu hiyo na Besuktas nchini Uturuki ndiko kutakuwa nyumbani kwake hivi sasa.
Wachezaji hao wote wawili wameambiwa na kocha mpya Jose Mourinho kuwa hawatakuwa sehemu ya mipango yake kwa ajili ya msimu mpya.
Raul mwenye umri wa miaka 33 ambaye ni kipenzi cha mashabiki wa Real , machozi yalikuwa yakimdondoka wakati akitangaza kuagana na klabu hiyo katika mkutano na waandishi habari katika uwanja wa Bernabeu.
Sherehe hizo za kumuaga zimefanyika mchana wa leo na kukiri kuwa huenda akahamia katika klabu ya Bundesliga ya Schalke 04 timu ambayo imesema itampa mkataba wa miaka miwili, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ujerumani , lakini amesema pia kuwa kuna uwezekano akahamia nchini Uingereza.
Mchezaji mwenzake Gutti amesema kuwa anafunga ukurasa wa enzi yenye utukufu mkubwa katika wakati wake wa kucheza soka ,baada ya miaka 15 ya kuichezea Real Madrid.
Huko Amerika ya kusini, wachezaji wa timu ya Corinthians wamempa kocha mpya wa Brazil Mano Menezes mkono wa kwaheri kwa kuichapa Guarani kwa mabao 3-1 na kujiweka kileleni mwa ubingwa wa ligi ya Brazil. Menezes , ambaye anachukua hatamu za kuifunza timu ya taifa ya Brazil leo Jumatatu ambapo anatarajiwa kutangaza kikosi chake kwa ajili ya mchezo wa kirafiki na Marekani mwezi ujao, alipewa kwaheri stahili baada ya mashabiki kusimama kwa heshima yake uwanjani hapo.Menezes ambaye aliiongoza Corinthians kutoka daraja la pili katika msimu wake wa kwanza akiwa kocha mwaka 2008, nafasi yake itarithiwa na Adilson Batista, ambaye alifurushwa na timu ya Cruzeiro mwezi uliopita.
Mawakala wa mchezaji nyota kijana wa Italia mshambuliaji Mario Baloteli wamekanusha leo Jumatatu kuwa mchezaji wao ametia saini kuichezea klabu ya ligi kuu ya Uingereza Manchester United. Ripoti za hapo kabla katika vyombo vya habari nchini Italia zimedai kuwa kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 mshambuliaji wa Inter Milan tayari amekubali mkataba na timu hiyo ya ligi kuu ya Uingereza na kwamba kile kinachokosekana kwa sasa ni makubaliano baina ya vilabu hivyo viwili. Lakini wakala wake Mono Raiola ameliambia shirika la habari la Ansa, kuwa hakuna kitu kama hicho kilichotiwa saini kati ya Baloteli na Manchester City na sidhani kama kuna kitu kama hicho kitatokea katika siku chache zijazo.
Na wiki moja baada ya kukataliwa kuhamia Fulham ya Uingereza, kocha wa Ajax Amsterdam Martin Jol anapaswa sasa kukitayarisha kikosi chake kupambana na PAOK Salonika ya Ugiriki katika ligi ya mabingwa duru ya tatu siku ya Jumatano.
Jol amewaongoza mabingwa mara tano wa ligi ya mabingwa barani Ulaya Ajax kuwa makamu bingwa wa ligi ya Uholanzi, Eredivisie, nyuma ya FC Twente msimu uliopita, lakini amekasirishwa na kile anachokiona kuwa ni klabu hiyo kutokuwa na nia ya kuwazuwia wachezaji wao muhimu kuondoka katika klabu hiyo. Ni katika wakati huu ndipo Jol alipokubali mualiko wa kujiunga na Fulham ya Uingereza, lakini alikataliwa ruhusa ya kuondoka na ameapa kusahau yote hayo na kuganga yajayo.
Manchester United imepata kipigo chake cha kwanza katika ziara yake ya kabla ya kuanza kwa msimu wa ligi katika mataifa ya Amerika ya kaskazini wakati walipobanjuliwa kwa mabao 2-1 dhidi ya Kansas City Wizards mjini Kansas jana Jumapili.
Mbele ya mashabiki 52,000 katika uwanja wa Arrowhead, Wizards walifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 11 kwa bao la mchezaji wa kati Davy Arnaud kabla ya Dimitar Berbatov kurejesha bao hilo kwa mkwaju wa penalti, lakini Kei Kamara aliirejeshea ushindi Kansas dakika moja baadaye.
Dane Richards alipachika bao katika dakika ya 70 kuipa ushindi New York Red Bulls katika ushindi wa mabao 2-1 pia dhidi ya timu ya ligi kuu nchini Uingereza ya Manchester City jana Jumapili , timu ambayo nayo kama Man United iko katika ziara katika bara la Amerika.
Tottenham Hotspurs wametoka sare ya bao 2-2 dhidi ya Sporting Lisbon katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa mjini New Jersey , Marekani jana Jumapili, ambako timu zote hizo mbili ziko ziarani kwa ajili ya kujiandaa na ligi za nchi zao.
Kiongozi mkuu mpya wa chama cha soka nchini Japan Junji Ogura ataogoza juhudi za nchi hiyo za kutaka kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la dunia mwaka 2022, chama hicho kimesema leo Jumatatu.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 71 ameteuliwa kuwa rais mpya wa chama cha soka nchini Japan , JFA, jana Jumapili baada ya mtangulizi wake Motoaki Inukai kujiuzulu baada ya kipindi cha utawala cha miaka miwili akielezea kujizulu kwake ni kutokana na sababu za kiafya.
Michezo ya riadha ya bara la Ulaya inaanza rasmi siku ya Jumanne mjini Barcelona. Na mwanariadha, Christophe Lemaitre mkimbiaji kutoka Ufaransa anakumbana na mkimbiaji kutoka Uingereza Dwain Chambers katika pambano la mita 100 katika mashindano ya ubingwa wa riadha katika bara la Ulaya yanayoanza kesho Jumanne mjini Barcelona.Kijana huyo mwenye umri wa miaka 20 yuko katika chati za juu za wakimbiaji barani Ulaya kwa mbio za mita 100 na 200 akiwa yuko katika hali nzuri kabisa katika wakati muhimu kwa ajili ya mashindano hayo yanayofanyika katika mji wa Barcelona.
Mbio hizo za mita 100 pia hazitavuta hisia kwa wanariadha hao wawili tu, ambapo raia wa Norway Jaysuma Saidy Ndure akiwa nae anawania taji hilo kama alivyo Martial Mbandjock kutoka Ufaransa pia.
Kuruka juu wanawake pia ni tukio linalosubiriwa kwa hamu kubwa wakati bingwa wa dunia , mwaka 2007 na 2009, Blanka Vlasic akilenga kuivunja rekodi ya muda mrefu ya dunia ya mita 2.09 iliyowekwa na Stefka Kostadinova.
Tennis.
Bingwa wa mchezo wa tennis katika michuano ya Wimbledon Serena Williams anaendelea kuwa katika nafasi ya juu ya orodha ya wachezaji wa tennis duniani iliyotolewa leo na shirikisho la tennis duniani , WTA. Msichana huyo kutoka Marekani anafuatiwa na Jelena Jankovic kutoka Serbia pamoja na dada yake Venus Williams akishika nafasi ya tatu.
Mwandishi : Sekione Kitojo/ AFPE/ DPAE / RTRE
Mhariri : Josephat Charo.