1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka kumi ya Tony Blair

27 Juni 2007

Leo hii, waziri mkuu wa Uingereza , Tony Blair, anastaafu kutoka wadhifa wake na kumpisha Gordon Brown. Alipoingia madarakani miaka kumi iliyopita, baada ya muda mfupi tu, Tony Blair alipendwa sana na Waingereza.

https://p.dw.com/p/CHC5
Blair aondoka
Blair aondokaPicha: AP

Aliweza kukiokoa chama cha Labour kutoka upande wa upinzani na kukipa nguvu mpya. Lakini mafanikio yake yaliathirika tangu Uingereza kujiingiza katika vita dhidi ya Iraq. Blair pamoja na chama cha Labour walizidi kupoteza wafuasi. Leo basi anatoka madarakani, lakini hatoki kabisa katika jukwaa la siasa ya kimataifa. Uchambuzi wa mwandishi wetu wa Idhaa ya Kiingereza, Irene Quaile, juu ya muda wa Blair kuwa madarakani:

Kweli ni miaka kumi tu Blair aliiongoza Uingereza? Kuondoka kwake ni mwisho wa enzi maalum. Tangu yeye kuingia madarakani, karibu tumesahau kuwa kabla yake Uingereza ilikuwa mikononi mwa Wahafidhina. Bibi mkali Margaret Thatcher na mrithi wake John Major walisahauliwa haraka, baada ya kijana huyu kiongozi wa chama cha “New Labour”, Leba mpya, alishinda katika uchaguzi wa mwaka 1997 alielekea njia mpya kati ya mirengo ya kulia na kushoto.

Aliunda sura mpya ya chama cha Labour ambacho ni chama cha wafanyakazi wa viwanda na wa jumuiya za wafanyakazi, alikitoa kutoka upande wa kushoto kabisa na amekifanya kiweze kuchaguliwa tena na watu wa tabaka ya kati. Blair alikuwa waziri mkuu mwenye umri mdogo kabisa tangu mwaka 1812. Aliipeleka familia yake katika nyumba ya Downing Street No. 10, aliungwa mkono na waimbaji maarufu – ilikuwa ni enzi ya “Cool Britannia”.

Katika muda huu wa miaka kumi chini ya Tony Blair, Uingereza alifanya mageuzi mapya. Uchumi unakua. Idadi ya watu wasiokuwa na kazi imepungua. Mzozo wa Irland ya Kaskazini ulioendelea kwa miaka mingi, umetatuliwa. Majimbo ya Irland Kaskazini, Scotland na Wales yamepewa mabunge yao. Pia, serikali iliwekeza sana katika mfumo wa afya na elimu.

Hata hivyo, si kama kila kitu ni kizuri katika nchi hiyo ya Leba mpya. Bado kuna foleni ndefu kwenye vituo vya afya. Miradi fulani ya kubinafsisha viwanda haikufaulu. Licha ya hayo yote lakini, pengo kati ya maskini na matariji ni dogo kuliko zamani.

Kwa nini basi, chama cha Labour cha Blair kimepotea kura nyingi katika chaguzi za mabunge ya Wales na Scotland hivi karibu? Msingi wa sera za serikali ya Blair ni kuziuza kama mafanikio. Lakini mashaka kati ya wananchi yaliongezeka kuhusiana na kashfa juu ya silaha za kuwaangamiza watu wengi ambazo hazikupatikana nchini Iraq. Pamoja na upinzani mkubwa, Blair aliiingiza Uingereza katika vita, hatimaye lakini sababu aliyoitoa ilikuwa uwongo. Blair alitajwa kuwa ni kama kibaraka wa George Bush.

Juu ya hayo kuna tuhuma za kuwasaidia marafiki kupata vyeo vya juu, kama kwa mfano Peter Mandelson, ambaye alikuwa mshauri wa Blair na sasa ni kamishna wa Umoja wa Ulaya. Pia chama cha Labour kimatuhumiwa kula rushwa. Hivyo, sura nzuri ya Blair imeathirika.

Mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya uliofanywa hivi karibuni uliweka wazi kuwa Blair ameshinda na kuisongeza Uingereza karibu zaidi na Umoja wa Ulaya. Licha ya Blair mwenyewe kuunga mkono Umoja huu, wasiwasi wa Waingereza dhidi ya Umoja wa Ulaya ulizidi katika miaka ya nyuma.

Kwa hivyo, mude umewadia Blair aondoke madarakani. Tayari, wapiga kura wanajibu hatua hiyo, kwani chama cha Labour kinazidi kuungwa mkono tena na wananchi. Mrithi wake Gordon Brown anapendwa zaidi kuliko kijana David Cameron, kiongozi wa chama cha Conservative, ambaye anafanana na Blair wa zamani. Haya yanaonyesha kuwa enzi ya Blair imekwisha. “Cool Britannia” iko tayari kwa kiongozi mpya.

Lakini Blair amejihakikisha nafasi yake katika vitabu vya historia. Ikiwa kweli ataweza kuokoa sifa yake iliyoathirika kutokana na vita vya Iraq, itabidi tusubiri matokeo ya siku za usoni.