1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 10 tangu kuundwa kwa Benki Kuu ya Ulaya

R.Wenkel/P.Martin1 Juni 2008

Leo,Umoja wa Ulaya unasherehekea mwaka wa kumi tangu kuundwa kwa Benki Kuu ya Ulaya ECB.Wajibu mkuu wa benki hiyo ni kuhifadhi thamani ya Euro na uthabiti wa bei katika eneo linalotumia sarafu hiyo.

https://p.dw.com/p/EAd5
** ARCHIV ** Die Euro-Skulptur und Europaeische Zentralbank, EZB, fotografiert am 15.Maerz 2005 in Frankfurt am Main. Die Europaeische Zentralbank (EZB) wurde am 1. Juli 1998 gegruendet. Sie hat ihren Sitz in Frankfurt am Main. Erster Praesident der EZB war der Niederlaender Wim Duisenberg. Seit November 2003 steht der Franzose Jean-Claude Trichet an der Spitze der uebernationalen Institution. (AP Photo/Michael Probst) --- ** FILE ** Euro sculpture and European Central Bank, ECB, in Frankfurt, central Germany, Tuesday, March 15, 2005. (AP Photo/Michael Probst
Jengo la Benki Kuu ya Ulaya mjini Frankfurt Ujerumani.Picha: AP

Benki Kuu ya Ulaya ilipoanza kufanya kazi miaka kumi iliyopita,wengi walikuwa na shaka juu ya uwezo wa benki hiyo kudhibiti kiwango cha mfumuko wa bei na hivyo kuimarisha thamani ya sarafu ya pamoja Euro.Lakini miaka kumi baadae Benki Kuu ya Ulaya-ECB inapongezwa kwa kufanikiwa kujumuisha uchumi,kupunguza viwango vya riba na kuzalisha nafasi za ajira pamoja na kufanya mageuzi mbali mbali ya kifedha.

Kwa mujibu wa ripoti maalum iliyotolewa kuadhimisha miaka kumi tangu kuzinduliwa kwa ECB,sasa biashara na huduma zimeongezeka kati ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro,uwekezaji wa kigeni umeongezeka na nafasi zaidi za ajira zinaendelea kuzinduliwa.Kwa mfano,nafasi mpya za ajira milioni 15 zimepatikana katika eneo linalotumia Euro,tangu kuanzishwa kwa sarafu hiyo ya pamoja hapo Januari mosi mwaka 1999.Hata ukosefu wa ajira umefikia kiwango cha chini kabisa tokea mwanzoni mwa miaka ya 80.Kwa sehemu fulani,mageuzi yaliyopaswa kufanywa kabla ya kujiunga na kundi la nchi 15 zinazotumia Euro, yamesaidia kuimarisha uchumi.

Rais wa Benki kuu ya Ulaya Jean-Claude Trichet amesisitiza umuhimu wa kupambana na mfumuko wa bei. Miongoni mwa changamoto zingine ni kuendeleza sera za kimkakati na kifedha ili kanda ya Euro iwe na uwezo wa kujirekebisha kwa urahisi zaidi na kuimarisha uwezo wa kukua zaidi.Nchi zingine za Ulaya zinazoazimia kuingia katika kanda ya Euro zimeshauriwa kupambana kwa dhati na changamoto za aina hiyo.

Wakati huo huo ECB imetahadhari,ingawa nafasi za ajira zimeongezeka,uzalishaji wa bidhaa umepungua kasi tangu kati kati ya miaka ya 90.Kwa mujibu wa ripoti ya ECB, sheria kali za kuhifadhi mazingira,kodi kubwa pamoja na fikra za kupotosha zinazohusishwa na sheria za kuweka kiwango cha chini cha mshahara ni miongoni mwa mambo yanayowazuia wengi kushiriki katika soko la ajira.

Hata hivyo,sera za Benki Kuu ya Ulaya kutuliza thamani ya Euro,zimesaidia kupandisha thamani ya sarafu hiyo.Kwa mfano,Euro ilipozinduliwa Januari mwaka 1999,thamani yake ilikuwa sawa na senti 95 za Kimarekani,lakini leo hii Euro moja ni sawa na Dola moja na senti 55.Bila shaka kupanda kwa thamani ya Euro kumezisadia nchi zinazotumia sarafu hiyo kumudu gharama za kuongezeka kwa bei ya mafuta ghafi.