1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kuwania madaraka huko Sri Lanka

Sylvia Mwehozi
1 Novemba 2018

Rais wa Sri Lanka ameondoa hatua ya kusimamisha bunge leo Alhamis na kuitisha mkutano wa wabunge wiki ijayo ambao unaweza kumaliza mvutano wa kuwania madaraka baina ya mawaziri wakuu wawili hasimu. 

https://p.dw.com/p/37Wm0
Sri Lanka Protest von Unterstützern des abgelösten Ministerpräsidenten
Picha: Reuters/D. Liyanawatte

 

Hatua hiyo ya rais Maithripala Sirisena ambaye alichochea mgogoro kwa kumfuta kazi Ranil Wickeremesinghe kama waziri mkuu na kumteua kiongozi wa zamani aliye na nguvu Mahinda Rajapakse kuchukua nafasi yake, kunaweza kusababisha upigaji kura itakayoamua baina yao wawili nani ana uungwaji mkono miongoni mwa manaibu wake.

Sirisena aliahirisha bunge hadi Novemba 16, muda mchache baada ya kumfuta kazi waziri mkuu Ijumaa iliyopita na kuzidisha mgogoro uliosababisha spika wa bunge kuonya kwamba kutatokea vita hadi kura itakapofanyika.

Spika wa bunge Karu Jayasuriya ametangaza kwamba atakutana na viongozi wa vyama vya siasa kesho Ijumaa ili kujadili hatua zitakazofuata katika jitihada za kuumaliza mgogoro huo. Bado haijawa wazi lini kura hiyo itapigwa.

Afisa mmoja anayehusika katika mchakato huo ameliambia shirika la habari la AFP kwamba spika amepata maelewano na rais, la sivyo angemkiuka rais na kuitisha bunge hapo kesho Ijumaa.

Sri Lanka Abgesetzter Premierminister  Ranil Wickremesinghe
Waziri mkuu aliyefutwa kazi Ranil WickremesinghePicha: Reuters/D. Liyanawatte

Sirisena anasisitiza kwamba maamuzi yake yalikuwa halali lakini spika wa bunge ambaye ndiye mtu wa tatu kimamlaka alikataa kutetea maamuzi hayo. Mwanasheria mkuu Jayantha Jayasuriya naye pia ana wasiwasi na uhalali wa hatua za rais Sirisena na hivyo kumwongezea shinikizo.

Wanadiplomasia wa magharibi walioko mjini Colombo wameweka wazi kwamba hawako tayari kuutambua utawala mpya. Marekani, nchi jirani ya India pamoja na mfadhili mkubwa wa kiuchumi wa Sri Lanka China, wametoa wito kwa pande zote hasimu kumaliza mgogoro huo kwa amani.

Wickremesinghe amesalia katika makazi rasmi ya waziri mkuu mjini Colombo huku mamia ya wafuasi wake wakipiga kambi  nje. Amerejelea kudai kwamba bunge liitishwe tena ili aweze kudhihirisha uungwaji mkono mkubwa katika bunge lenye viti 225. Na hapa anasema nchi hiyo sasa iko katika mkwamo mkubwa.

Rajapakse, ambaye miaka yake 10 kama rais kufikia 2015 ilimfanya kujulikana kwa madai ya ufisadi na kumalizwa kikatili kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ya Tamal, hivi sasa anatengeneza makazi mengine ambayo yatakuwa ni ofisi rasmi ya waziri mkuu.

Mahinda Rajapaksa
Rais wa zamani aliyeteuliwa kuwa waziri mkuu mpya Mahinda RajapaksaPicha: picture-alliance/Pacific Press/P. Dambarage

Kiongozi huyo mwenye miaka 72 tayari ametangaza timu ya baraza lake dogo la mawaziri 12 na kuzungumza na watendaji   katika wizara ya fedha. Ameahidi kwamba atapanua baraza lake na kufikia mawaziri 30.

Mahasimu hao pia wanaendeleza mapambano ya kuwania madaraka nyuma ya pazia, wakijaribu kuwashawishi wabunge kutoka pande zinazokinzana ili waongeze nguvu pale kura ikapoitishwa. Pande zote mbili zimewaomba wabunge waliokuwa ziara za nje kurejea nyumbani hima. Rajapakse amewapatia wabunge watano kutoka chama cha hasimu wake nafasi tano za uwaziri, baada ya kuondoka. Naye Wickremesinghe amewashawishi angalau wabunge wawili kutoka chama cha rais Sirisena ili kujiunga na chama chake cha United National Party.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP

Mhariri: Iddi SSessanga