1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jee hakuna vita tena Darfur?

Abdu Said Mtullya28 Agosti 2009

Kamanda wa jeshi la kimataiafa katika Darfur jenerali Agwai adai, hakuna vita tena katika jimbo hilo!

https://p.dw.com/p/JKsu
Mgogoro wa Darfur wakaribia kumalizika?Picha: AP

Jimbo la Darfur halimo tena katika hali ya vita na kwamba sasa limebakia kundi moja pekee la waasi lenye uwezo wa kufanya mashambulio ya kiwango kidogo. tu.

Hayo amesema mkuu wa jeshi la kimataifa la kulinda amani katika sehemu hiyo kamanda Martin Luther Agwai.

Kamanda Agwai wa jeshi la pamoja la Umoja Mataifa na Umoja wa Afrika,UNAMID ,katika jimbo la Darfur aliwaambia waandishi habari kwamba mgogoro wa Darfur umegeuka kuwa ujambazi na kwamba mashambulio yanayotokea ni ya kiwango cha chini.

Hatahivyo kamanda Agwai aliemaliza muda wake katika jimbo la Darfur amesema bila ya mapatano ya amani kufikiwa hata mashambulio hayo ya kiwango kidogo yanaweza kuiathiri sehemu ya magharibi ya jimbo la Darfur.

Jenerali Martin Luther Agwai amesema anaondoka Darfur wakati ambapo mapambano yamepungua sana.

Hatahivyo kiongozi wa kundi la Justice and Equality Movement Khalil Ibrahim amesema kinachoonekana sasa ni kipindi shwari kitakachofuatiwa na dhoruba. Khalil Ibrahim amesema mnamo siku za karibuni jenerali Agwai atatambua kuwa aliyoyasema siyo sahihi.

kiongozi huyo amesema, kuwa kamanda wa jeshi la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa amezungumza kama mwanasiasa anaetaka kuonesha kuwa amefanikiwa.

Mgogoro wa Darfur ulianzia mnamo mwaka 2003 baada ya waasi kuanzisha mapambano dhidi ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa kiarabu.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa watu mia tatu alfu wamekufa na milioni mbili na laki saba wamekuwa wakimbizi wa ndani

Jukumu la kuliongoza jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika litachukuliwa na Patrick Nyamvumba kutoka Rwanda baada ya jenerali Martin Luther Agwai kumaliza muda wake wiki ijayo. ....

Mwandishi/ Mtullya Abdu/AFP

Mhariri/.Abdul-Rahman