1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro mwingine wa Madeni wanukia?

15 Machi 2018

Ripoti ya 2018 kuhusu Madeni yaonya juu ya uwezekano wa kuzuka upya mgogoro wa madeni kutokana na nchi nyingi za Afrika kuwa hoi taabani kwa madeni na hali mbaya ya uchumi

https://p.dw.com/p/2uOeK
Kirchentag Demonstration Erlaßjahr 2000
Picha: picture-alliance/dpa

Ripoti kuhusu madeni ya mwaka 2018 inaonya kwamba hatua ya kuongezeka kwa wawekezaji wa kibinafsi kukimbilia barani Afrika inaweza kusababisha hatari. Ripoti hiyo inasema kwamba kutokana na kiwango cha riba barani Ulaya kuporomoka, wawekezaji walio wengi wanajikuta wakivutiwa zaidi kuwekeza barani Afrika lakini hatua hiyo inaweza kuongeza kwa kiasi kikubwa madeni.

Ripoti ya mwaka huu 2018 iliyochapishwa na mtandao wa Erlassjahr.de na shirika la Misereor inaonya kuhusu kuongezeka kwa madeni endapo hali ya wawekezaji wa kibinafsi ya kukimbilia barani Afrika haitobadilika barani Ulaya.Msumbiji kabla ya miaka miwili iliyopita ilikuwa bado ni nchi inayoangaliwa kama mfano wa kuigwa barani Afrika na ghafla ikaibuka kashfa nzito ikihusisha mabenki ya kigeni yaliyotowa mkopo wa mabilioni ya dolla kwa kampuni ambayo sio moja kwa moja ya umma au ya serikali  kwa ajili ya kununua maboti ya kupiga doria pamoja na maboti ya uvuvi na serikali ya Msumbiji ilikuwa mdhamini wa mkopo huo lakini mabilioni hayo ya dolla hakuna anayeweza kusema yalipotelea wapi.

Msumbiji ikashindwa kulipa kabisa deni lake na matokeo yake sarafu ya nchi hiyo ikaingia katika mporomoko wa thamani yake na gharama ya maisha ikaongezeka kupita kipimo. Msumbiji ni hali ya mfano mbaya unaoweza kusimuliwa lakini siyo nchi pekee inayoweza kuwa mfano wa hali halisi.

Mratibu wa mtandao wa Erlassjahr.de Jürgen Kaiser anaonya kwa kusema kwamba kwa kipindi cha miaka kadhaa wamekuwa wakiiangalia hali ya mambo kwa uhalisia na kubaini kwamba kuna kitisho cha kutokea mgogoro mwingine wa madeni.Kimsingi mtandao wa Erlassjahr.de unawakilisha jumla ya mashirika 600 ya kiaraia,makanisa na mashirika ya kisiasa  nchini Ujerumani ukiwa na dhamiraa ya kupigania kufutiwa madeni kwa nchi masikini za Kiafrika,lakini ripoti yake ya mwaka huu 2018 kuhusu madeni inaonya wazi juu ya kutokea hali mbaya kabisa ya madeni.

White Slums - South Africa
Picha: DW/V.da Rocha

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na mtandao huo nchi 119 kati ya 141 kulikofanyika utafiti zinaonesha kuwa katika hali mbaya ya madeni. Na tangu ulipozuka mgogoro wa kiuchumi mnamo mwaka 2008 nchi hizo zimekuwa zikiendelea kujikuta zikiongezeka madeni mara mbili.Kwa mujibu wa mtandao huo madeni yameongezeka tangu wakati huo na kufikia dolla Trilioni 6,877 na katika nchi 87 hali  imeonekana kuzidi kuwa mbaya. Mikopo inayotolewa barani Afrika na mashirika ya kibinafsi inatajwa kwamba ndiyo inayozidi kuliongeza deni la Afrika.

Kwa uchunguzi uliofanywa katika bara hilo la Afrika kuna nchi kumi ambazo ziko katika hali mbaya na pengine zipo mahututi kabisa kwa madeni na mwelekeo unaonesha kwamba hali hiyo itazidi kuwa mbaya. Na nchi zinazotajwa kuwa katika hali hiyo sio tu zile zilizozoelekea kuwa hoi taabani kiuchumi bali zipo pia nchi ambazo zilikuwa zikiangaliwa kama mfano wa nchi zinazosimama kichumi kama Ghana au nchi kama Angola yenye utajiri wa mafuta. Kadhalika miongoni mwa nchi zilizopo katika hali mahututi zaidi kwenye orodha hiyo zipo Somalia na Zimbabwe ambazo zinauwezo wa kulipa madeni yake ama kwa sehemu fulani  au kushindwa kabisa kuyalipa.

Mwandishi:Daniel Pelz/Saumu Mwasimba

Mhariri: Daniel Gakuba.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW