1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgao wa Petroli wazusha hasira miongoni mwa Raia wa Iran

27 Juni 2007

Wananchi wenye hasira wamevitia moto vituo viwili vya Petroli katika mji mkuu wa Iran Tehran hii leo baada ya serikali kuanzisha hapo jana mgao wa Petroli kwa magari ya binafsi.

https://p.dw.com/p/CB3H
vituo kadhaa vya mafuta ya petroli vyatiwa moto na waandamanaji wenye hasira
vituo kadhaa vya mafuta ya petroli vyatiwa moto na waandamanaji wenye hasiraPicha: AP

Amri ya Iran ya kuanzisha mgao wa mafuta ya Petroli nchini humo imezusha hisia kali miongoni mwa raia na kusabisha kutiwa moto vituo kadhaa vya mafuta katika mji mkuu Tehran huku kukiwa na maandamano ya kitaifa.

Redio ya taifa imetangaza leo hii kwamba vituo kadhaa viliharibiwa vibaya vikiwemo vituo viwili vilivyotiwa moto na watu wenye hasira. Madereva wenye ghadhabu waliokuwa katika foleni ndefu za kusubiri mafuta pia wameripotiwa kupambana vikali na polisi baada ya kusikia tangazo kwamba mgao huo umeanza kufanya kazi tangu jana usiku.

Maandamano haya ndio ya kwanza makubwa kabisa kuwahi kutokea nchini humo tangu rais Mahmoud AhmedNejad kuingia madarakani mwaka 2005 licha ya kuwa wakosoaji hivi karibuni wamekuwa wakisema sera za rais huyo zinarudisha nyuma maendeleo na kuwaumiza raia waliomasikini.

Mapema mwezi huu zaidi ya wanauchumi 50 walimuandika barua ya wazi rais AhmedNejad na kumuonya juu ya athari zitakazotokea kutokana na sera zake za kiuchumi. Hata hiyvo rais AhmedNejad amesema serikali yake iko imara kuzuia mfumko wa bei na kupunguza kiwango cha umaskini nchini humo.

Hatua hii ya mgao wa petroli imechukuliwa na serikali ili kupunguza athari za vikwazo vya kichumi vilivyowekwa na Umoja wa mataifa dhidi ya nchi hiyo kuhusika na mradi wake wa Kinuklia.

Pamoja na kuwa Iran ni mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani huagiza kutoka nje zaidi ya asilimia 50 ya mafuta kukimu mahitaji kwasababu haina uwezo wa kusafisha mafuta ya kutosha.

Muda mfupi kabla ya amri hiyo kuanza kufanya kazi wenye magari ya binafsi na Taxi walikimbilia kuunga foleni ndefu kwenye vituo vya kuuza Petroli mjini Tehran na maeneo mingine ya nchi huku kukiwa na ulinzi wa polisi,baadhi ya watu iliwabidi hata kuchukua ndoo za kujaza mafuta.

Amri hiyo inasema kila mwenye gari ya binafsi ataruhusiwa kununua hadi lita 100 tu za Petroli kwa mwezi ilhali wenye kutumia petroli na gesi ya unyevunyevu wataruhusiwa kununua lita 30 tu.

Serikali imesema mgao huo utaendelea kwa muda wa miezi minne na huenda muda huo pia ukaongezwa hadi miezi sita.

Polisi wa kukabiliwa na ghasia wameshapelekwa katika maeneo yenye fujo mjini Tehran lakini maandamano yanaripotiwa kuendelea huku waandamanaji wakirusha mawe.

Wiki mbili zilizopita serikali ilianzisha duru ya mwanzo ya mgao huo ambapo ulilenga tu magari ya serikali na vile vile ikapandisha bei ya mafuta kwa asilimia 25.

Iran inakadiria kwamba bila ya kuwepo mgao huo basi kiwangoa cha kuagiza mafuta ya petroli huenda kikafikia dolla Billioni tisa na nusu kwa mwaka.