Mfumo wa sheria nchini Rwanda unatiliwa shaka | Masuala ya Jamii | DW | 02.11.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Mfumo wa sheria nchini Rwanda unatiliwa shaka

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetoa mwito wa kusimamishwa kuwapeleka watuhumiwa wa mauaji ya halaiki, makosa ya ukiukaji haki za binadamu na uhalifu wa kivita katika mahakama zinazoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita za nchini Rwanda CTR hadi kwanza ithibitishwe kuwa kesi hizo zitaendeshwa chini ya sheria zinazokubalika za kimataifa.

Irene Khan katibu mkuu wa shirika la Amnesty International

Irene Khan katibu mkuu wa shirika la Amnesty International

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu Amnesty International limetoa mwito wa kusimamishwa kuwapeleka watuhumiwa wa mauaji ya halaiki, makosa ya ukiukaji haki za binadamu na uhalifu wa kivita katika mahakama zinazoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita za nchini Rwanda CTR hadi kwanza ithibitishwe kuwa kesi hizo zitaendeshwa chini ya sheria zinazokubalika za kimataifa.

Shirika hilo la kimataifa linalotetea haki za binadamu limetoa mwito huo kwa serikali zote leo hii kwamba zisiwapeleke watuhumiwa wa makosa ya uhalifu wa kibinadamu uliotokea nchini Rwanda mwaka 1994 ambako zaidi ya raia laki nane wa kabila la Watusi na Wahutu waliuwawa katika maujai ya halaiki.

Shirika hilo limesema, sababu ya kutoa mwito huo ni kwamba linashuku mfumo wa sheria katika mahakama za nchini Rwanda.

Shirika la Amnesty International limesema, licha ya kuwepo mabadiliko katika mfumo wa sheria nchini Rwanda bado kuna shaka juu ya uwezo wa Kigali wa kuchunguza na hatimae kuwafunguliwa mashtaka watuhumiwa wa makosa ya uhalifu wa kivita kwa kufuata haki na kiwango cha sheria za kimataifa.

Wakati huo huo Erwin van der Borght afisa wa shirika la kimataifa la Amnesty International anaeshughulika na mpango wa barani Afrika wa shirika hilo amesema shirika hilo linafahamu umuhimu wa mahakama za nchini Rwanda na jinsi zinavyowajibika na jukumu la kufanya uchunguzi na kuwafikisha mbele ya mahakama watuhumiwa wote wa uhalifu wa kibinadamu lakini bado kuna kazi kubwa inayobidi kufanyika ili kuhakikisha kwamba haki za kibinadamu za watuhumiwa na wahanga zinaheshimiwa na kulindwa na mahakama.

Mahakama ya umoja wa mataifa iliyoko mjini Arusha nchini Tanzania na ambayo hasa inahusika na kesi za watuhumiwa wakuu wa mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda imetolewa mwito wa kusimamisha hatua ya kuzihamisha kesi za watuhumiwa hao hadi nchini Rwanda mpaka pale utawala wa Kigali utakapothibitisha kuwa kesi hizo zitashughulikiwa kwa haki bila upendeleo na kwamba watuhumiwa, wahanga au mashahidi watalindwa.

Hata hivyo Rwanda imekataa mwito huo wa shirika la kimataifa linalotetea ahaki za binadamu.

Muongoza mashtaka mkuu nchini Rwanda Martin Ngoga amesema mahakama za nchini mwake zimekuwa zikiendesha kesi nyingi za aina hiyo kuliko mahakama ya mjini Arusha au hata kuliko mahakam za nchi nyingine za kigeni.

Shirika la Amnesty International limependekeza kuwa mahakama ya umoja wa mataifa ya mjini Arusha iombe muda zaidi na ufadhili kutoka kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuliko kuzihamishia kesi zaidi za uhalifu wa kibinadamu nchini Rwanda pale muda wake utakapokamilika mwaka ujao.

Tangu mahakama ya umoja wa mataifa ilipoanzishwa mjini Arusha mwaka 1994 na kusikiliza kesi ya kwanza mwaka 1997 hadi sasa mahakama hiyo ya kimataifa imesikiliza jumla ya kesi 34.

Watuhumiwa 28 wamehukumiwa, watuhumiwa watano wameachiwa huru na kesi moja imehamishiwa katika mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ya mjini The Hague nchini Uholanzi.

Mpaka sasa mahakama hiyo ina kesi 29 ambazo zinaendela kusikilizwa,kati ya hizo kesi sita zinasubiri hukumu.