Mfumo wa kuonya mapema Tsunami
23 Desemba 2009Katika kituo hicho kikuu chenye vyombo vya kuonya mapema mabadiliko yanayotokea baharini na kuweza kusababisha Tsunami, kundi la kama watu saba huelekeza macho yao kwenye skrini kubwa iliyo ukutani kutazama tetemeko la ardhi la mwisho lilikotokea nchini Indonesia na lini. Kiongozi wa wafanyakazi hao Bayu Pranata anasema kuwa kwa wastani, kama mitetemeko 40 hutokea kila siku katika kanda hiyo na kuongezea:
"Tunachotaka kujua ni ile mitetemeko inayopindukia 7 katika Kipimo cha Richter na inayotokea si zaidi ya kilomita 70 kwenda chini ya usawa wa bahari. Hali hiyo ikitokea basi ni lazima kukusanya habari zaidi ili kuweza kuamua iwapo wakaazi waonywe juu ya hatari ya kutokea mawimbi ya Tsunami."
Baada ya kukusanya data hizo muhimu, Pranata na wafanyakazi wenzake wana muda wa kama dakika tano tu kuamua iwapo watoe tangazo la kwanza la kuwatahadharisha wakaazi. Uamuzi wa haraka ni muhimu sana.
Zaidi ya asilimia 90 ya mawimbi ya Tsunami husababishwa na mitetemeko ya ardhi inayotokea chini ya bahari. Kwa hivyo, data zinazokusanywa na vyombo maalum vilivyowekwa sehemu mbali mbali nchini Indonesia, ni kiini cha mfumo wa kusaidia kuonya mapema hatari ya kutokea mawimbi ya Tsunami.
Mfumo wa kutoa onyo la Tsunami unahitaji vyombo mbali mbali vinavyoweza kupima kwa haraka mabadiliko yote yanayotokea na kupeleka data hizo upesi iwezekanavyo katika kituo kikuu cha vipimo.Kwa njia hiyo ndio maisha ya binadamu wengi yataweza kunusurika.
Ujenzi wa kituo kikuu cha Ujerumani na Indonesia unatazamiwa kukamilika mwakani katika mwezi wa Machi. Lakini hiyo haimaniishi kuwa wataalamu wa Kijerumani wataondoka moja kwa moja,kwani kuna mipango na mikakati inayohitaji kujadiliwa ili kuhakikisha kuwa mradi huo wa kuwaonya wakaazi mapema vya kutosha utaendelezwa.
Mwandishi: Z.Robina/ZPR/P.Martin
Mhariri: Miraji, Othman