1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mfululizo wa miripuko ya mabomu waitikisa Nigeria

Miripuko ya mabomu imeendelea mfululizo katika maeneo kadhaa nchini Nigeria wakati wa maadhimisho ya sikukuu ya Krismasi, ambapo hadi sasa yameshasababisha vifo vya watu 28 na wengine kadhaa kuachwa majeruhi.

Mripuko katka mji wa Kaduna

Mripuko katka mji wa Kaduna

Mripuko wa kwanza ulitokea asubuhi ya leo katika Kanisa la Mtakatifu Theresa kwenye mtaa wa Madalla, mjini Abuja, wakati waumini wakishiriki sala ya Krismasi. Miripuko mingine imetokea mchana katika miji Jos, Damaturu na Gadaka.

Msemaji wa kundi lenye msimamo mkali wa kidini, Boko Haram, ameliambia Shirika la Habari la AFP kwa njia ya simu kwamba kundi lake linahusika na mashambulizi hayo.

"Tunachukuwa dhamana ya kuhusika na mashambulizi yote katika siku za hivi karibuni, ikiwemo miripuko ya leo ya mabomu katika kanisa mjini Madalla. Tutaendelea na mashambulizi kama hayo upande wa kaskazini katika siku chache zijazo." Amesema msemaji huyo, Abul Qaqa.

Makao Makuu ya Kanisa Katoliki, Vatican, yamelaani mshambulizi hayo katika Sikukuu ya Krismasi, ambapo Baba Mtakatifu wa 16, ameyaelezea kama matunda ya "ukatili na chuki zisizo na maana".

Mashambulizi katika mji wa Maiduguri

Mashambulizi katika mji wa Maiduguri

Msemaji wa Baba Mtakatifu, Federico Lombardi, amesema kwamba mauaji hayo yaliyofanyika kwenye nchi ya Afrika Magharibi ni ishara za ukatili na chuki ambazo haziheshimu maisha ya binaadamu.

"Tupo pamoja na mateso yanayolipata Kanisa Katoliki la Nigeria, na watu wote wa taifa hilo, ambalo linapitia kipindi kichungu cha vurugu za kigaidi katika siku hii ambayo ilitakiwa iwe ya furaha na amani. Tunatarajia kuwa mashambulizi haya hayatodhoofisha nia ya kuishi pamoja na majadiliano." Amesema Lombardi.

Vikosi vya usalama vinaripotiwa kuyafunga maeneo yalikotokea mashambulizi, huku wafanyakazi wa uokozi wakifanya jitihada ya kuondoa maiti na kuwaokoa majeruhi.

Katika mripuko wa kwanza kwenye kanisa la Mtakatifu Theresa, kwenye kitongoji cha Madalla, miili kadhaa ilitolewa kwenye kifusi ikiwa imekatikakatika vibaya, jambo lililofanya kazi ya kuzitambua maiti kuwa ngumu.

Shahidi mmoja, Ndubuisi Chukuemeka, ameliambia shirika la habari la Ujerumani (DPA) kuwa dada yake ni miongoni mwa waliouawa.

"Tulipokuwa tunatoka kanisani, nilisahau kadi ya Krisimasi niliyokuwa nimepewa, nikarudi kwenda kuichukua. Muda mchache baadaye nikasikia mripuko na lilikuwa ni hilo bomu. Nikaonma moshi na watu wanapiga kelele na kukimbia. Nikaziona nguo za dada yangu zimechanikachanika." Amesema Chukuemeka kwa majonzi.

Mashambulizi katika mji wa Maiduguri

Mashambulizi katika mji wa Maiduguri

Shahidi mwengine, Micheal Ogar, amesema kuwa mripuko ulitokea baada ya gari kuegesshwa karibu na kanisa hilo. Gari na nyumba kadhaa karibu na kanisa hilo pia zimeharibiwa na mripuko huo.

Msemaji wa Shirika la Huduma za Dharura la Nigeria, Yushau Shuaib, amesema kwamba idadi ya waliokufa na majeruhi huenda ikaongezeka. Shuaib ameomba wananchi wachangie damu kuokoa maisha ya majeruhi wanaopelekwa katika hospitali mbalimbali za mjini Abuja, ingawa amelalamikia upungufu mkubwa wa gari za kubebea wagonjwa na vifaa vya matibabu.

Kabla ya mashambulizi haya, mtaa wa Madalla haukuwa kamwe ukifikiriwa kuwa ungelishambuliwa. Sasa waumini wanaripotiwa kuyakimbia makanisa mengine mjini Abuja, wakihofia usalama wao.

Miripuko ya leo imetokea, huku kukiwa na taarifa kwamba mapambano baina ya jeshi la Nigeria na kundi la Boko Haram yamesababisha vifo vya watu karibu 100 katika miji ya Damaturu na Maiduguri kaskakazini mwa Nigeria. Idadi kubwa ya waliouawa ni wanachama wa Boko Haram, wanaopigania kuudwa kwa taifa linalofuata Shariah.

Kundi hilo linalaumiwa kwa kuendesha kampeni ya mauaji na mashambulizi ya mabomu, yakiwemo yale yaliouwa watu 65 katika mji wa Damaturu hapo Novemba na yale yaliyofanyika mwezi Agosti katika mji mkuu, Abuja, moja likiwa kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa. Watu 26 waliuawa baada ya mshambuliaji wa kujitoa mhanga kujiripua ndani ya gari.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/PDA/Reuters
Mhariri: Abdou Mtullya

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com