Mfululizo maalum wa ripoti wiki moja kabla ya mkutano wa Bali | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mfululizo maalum wa ripoti wiki moja kabla ya mkutano wa Bali

Kabla ya mazungumzo ya Bali kuanza, wiki hii nzima tutaangalia masuala kadhaa yanayohusiana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani kote. Kila siku katika matangazo yetu ya jioni na asubuhi tutaweletea ripoti maalum.

Kama ziwa limekauka...

Kama ziwa limekauka...

Makubaliano ya Kyoto ambayo yaliafikiwa miaka 10 iliyopita mjini Kyoto nchini Japan, hadi leo ni makubaliano makubwa kabisa yanayolenga kutunza hali ya hewa. Lakini makubaliano haya yataishia mwaka wa 2012. Ndiyo sababu, Umoja wa Mataifa umeuitisha mkutano mwingine wa kilele utakafanyika wiki ijayo kisiwani Bali, Indonesia. Mwaka uliopita mkutano huu wa kilele juu ya hali ya hewa ulifanyika Nairobi, Kenya, lakini bila ya kuleta mafanikio.

Mkataba wa Kyoto ni makubaliano ya kwanza ya kimataifa ambayo yanaweka viwango vya kupunguza utoaji wa gesi chafu kama Carbondioxide ambazo zinaaminika kuchangia zaidi katika ongezeko la ujoto duniani. Licha ya mataifa makubwa kama Marekani na Australia bado hazijatia saini mkataba huu, hadi leo nchi 170 zimejiunga na makubaliano ya Kyoto.

Hata hivyo, naibu katibu mkuu wa idara ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya hali ya hewa, Yvo de Boer, anaamini kwamba itakuwa vigumu wa viongozi wa serikali watakaohudhuria mkutano wa Bali kukubaliana. Bado lakini, Bw. Boer hajakata tamaa: “Habari muhimu zaidi kama ninavyoamini mimi ni kwamba, ndiyo, namna utoaji wa gesi chafu duniani kote na hasa katika nchi za kiviwanda inavyoendela inatia wasiwasi, lakini nchi zimeanza kutekeleza masharti ya kisiasa ili zifikie malengo ya mkataba wa Kyoto. Kulingana na makadirio yetu, hatua zinazochukuliwa zitatosha kwa nchi kufikia malengo yao.”


Ili lakini juhudi hizo zilizoanza ziwe na matokeo katika siku za usoni, inabidi masharti ya mkataba wa Kyoto yaendelezwe na hilo ndilo lengo la mkutano wa Bali.

Naibu katibu mkuu huyo Yvo de Boer anakumbusha juu ya ripoti iliyotolewa hivi karibu na wataalamu waliokutana Valencia, Uhispania: “Kimsingi, wataalamu wanasema kwamba tuna muda kama miaka 10 au 15 kubadilisha mwenendo katika utoaji wa gesi chafi upunguzwe ili tuyazuie matokeo mabaya ya mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa hivyo, mkutano wa Bali ni wakati wanasiasa wataweza kusimamisha mwenendo ulivyo na kuweka sera za pamoja hali ya hewa. Wakishindwa hatutaweza kuchukua hatua katika muda tulioupewa na wataalamu.”


Licha ya kwamba idara hiyo ya Umoja wa Mataifa inakaridia kwamba malengo ya mkataba wa Kyoto yatafikiwa, hata hivyo utoaji wa gesi chafu umefika kilele kipya. Sababu ni kwamba miongoni mwa watoaji wakubwa zaidi wa gesi chafu duniani, Marekani haijatia saini mkataba huu, na China na India hazilazimishwi kutimiza masharti yake. Mkutano wa Bali basi utakabiliwa na kazi ngumu kuzishawishi nchi hizi ziungane na makubaliano haya.

Bw. Yvo de Boer anasema kuna vitu vitatu lazima vitimizwe: “Suali ni je, mkutano wa Bali utaweza kuanzisha mazungumzo? Na la pili: Itawezekana kukubaliana juu ya ajenda kwa mazungumzo haya? Na tatu: Utawekwa wakati wa mwisho kufikiwa kwa makubaliano? Ikiwa haya yote matatu yatatekelezwa, basi mkutano huo wa Bali utakuwa umefanikiwa. La sivyo, tutabaki nyuma na tutakuwa tumeshindwa.”


Kwa hivyo, inabidi washiriki wote wawe tayari kukubaliana na kuelekea katika njia ya pamoja.

 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CTO2
 • Tarehe 26.11.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CTO2

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com