1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu Josina Machel, mwanamke mpigania uhuru

Sylvia Mwehozi
25 Julai 2018

Josina Machel ni jina muhimu katika historia ya Msumbiji. Ni mwanamama aliyekuwa mpigania uhuru ambaye alithubutu kushika silaha dhidi ya utawala wa Kikoloni wa kireno akiwahamasisha wanawake wengine pamoja na wanaume kuingia vitani kudai uhuru. Aidha Josina Machel alipigania haki ya mwanamke akiamini kwamba wanawake pia wana nafasi katika harakati za ukombozi.

https://p.dw.com/p/2vwqx

Mnamo mwaka 1964 kundi la wanafunzi waliondoka mji mkuu wa Msumbiji kujiunga na kambi ya mafunzo ya chama cha ukombozi cha FRELIMO, iliyokuwa Tanzania. Hawakufanikiwa kuwasili kwenye kambi hiyo. 
Walisimamishwa na polisi mpakani mwa Rhodesia na Zambia, na kurejeshwa nyumbani Msumbiji, ambako walifungwa jela kwa makosa ya harakati za kisiasa dhidi ya utawala wa kikoloni wa kireno. Miongoni mwa wanafunzi hao alikuwamo kijana Josina Muthemba. 

Josina anapata mafunzo ya kijeshi

Lakini Josina hakukata tamaa, baada ya vikwazo kadhaa alifanikiwa kuwasili katika kambi ya FRELIMO, ambako alikuwa ni mmoja ya wanawake 25 waliopatiwa mafunzo ya kijeshi.
Pia alikutana na Samora Machel aliyekuja kuwa mume wake, na baadae rais wa kwanza wa Msumbiji. Josina na wanawake wengine waliunga mkono mapambano nje ya uwanja wa vita. 

Ushiriki wake ndani ya chama

Alikuwa mwanachama wa tawi la wanawake la chama cha FRELIMO na kuandaa vituo vya afya, shule na vituo vya kulelea watoto wa raia waathirika wa vita. 
Josina alitajwa kuhudhuria ujumbe wa mkutano mkuu wa pili wa FRELIMO. Alitetea kikamilifu kushirikishwa kwa wanawake katika vita ya ukombozi. 

Mwaka 1969, alioana na Samora Machel. Mtoto wao wa kiume Samora Jr. alizaliwa mwaka huohuo. Josina alifariki kwa maradhi ya saratani ya ini mnamo Aprili 7, mwaka 1971. 
Chama cha FRELIMO kiliitangaza siku hii kuwa siku ya kitaifa ya wanawake Msumbiji. Ilikuwa ni miaka minne baadae ambapo uhuru ulipatikana.

Gwendolin Hilse amechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Lilian Mtono