1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel kukubali kima cha chini

17 Novemba 2013

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amedokeza kuwa tayari kukubali dai la chama cha Social Demokratik cha SPD la kuwa na kima cha chini cha mshahara kisheria ili kuweza kufikia makubaliano yao ya kuunda serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/1AJ4p
Kansela Angela Merkel akiwa na Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto mjini Berlin (11.11.2013).
Kansela Angela Merkel akiwa na Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto mjini Berlin (11.11.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Merkel ameanza kuwaandaa wahafidhina wenzake kwa ajili ya kufikia muafaka huo kwa kuuambia mkutano wa vijana wa chama chake cha Christian Demokratik hapo Ijumaa usiku kwamba kiwango cha malipo ya euro 8.50 kwa saa ambacho kinadaiwa na chama cha SPD kitakuwa na dhima katika kipindi cha usoni.Ameongeza kusema " Haitokuwa dira yetu ya kiwango cha chini cha mshahara.", lakini amekiri haitokuwa rahisi kwa chama chake kupata kile inachokitaka kutoka kwa SPD juu ya suala hilo.

Merkel ameshinda muhula wa tatu katika uchaguzi wa mwezi wa Septemba lakini ameshindwa kupata wingi wa viti bungeni kuunda serikali moja kwa moja na waliokuwa washirika wao wadogo katika serikali ya mseto chama cha mrengo wa kati kulia cha Free Demokratik wameshindwa kuambulia kiti bungeni.Hiyo ndio sababu iliomlazimisha kutaka kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya mseto na chama cha SPD ambacho kimepata matokeo mabaya kabisa ya uchaguzi ya baada ya kipindi cha vita lakini kimeendelea kubakia kuwa chama cha pili kwa ukubwa nchini Ujerumani.

Merkel anataka serikali iwe imeundwa kufikia Krismasi na mazungumzo juu ya makubaliano ya sera na nyadhifa yawe yamekamilika katika kipindi cha siku 10 zijazo.

Kansela Angela Merkel na viongozi wenzake wa vyama ndugu CDU/CSU katika mazungumzo ya serikali ya mseto mjini Berlin. (11.11.2013).
Kansela Angela Merkel na viongozi wenzake wa vyama ndugu CDU/CSU katika mazungumzo ya serikali ya mseto mjini Berlin. (11.11.2013).Picha: picture-alliance/dpa

SPD yan'gan'gania kima cha chini

Chama cha SPD kimekubali kuachana na ahadi yake ya kampeni ya kuongeza kodi kwa matajiri lakini kinagoma kuachana na ahadi yake ya kuweka kima cha chini cha mshahara .Takriban wanachama nusu milioni wa chama hicho watayapigia kura makubaliano hayo ya serikali ya mseto mapema mwezi wa Disemba jambo ambalo linazidi kuutia mashaka mchakato huo mzima.

Wahafidhina wanapendelea kuwekwa kwa kima cha chini cha mshahara lakini chini ya msingi wa sekta kwa sekta katika kiwango kitakachokubalika na waajiri na wafanyakazi badala ya kuamuliwa na serikali kuu. Kwa chama cha SPD inataka euro 8.50 kwa saa nchini kote venginevyo haitojiunga na serikali hiyo ya mseto.

Mwenyekiti wa chama cha SPD Sigmar Gabriel ameuambia mkutano wa chama hicho hapo Jumamosi (16.11.2013) mjini Leipzig kwamba "Wapenzi wahafidhina sasa inabidi mulitekeleze hilo."

Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akihutubia mkutano wa chama chake mjini Leipzig.(16.11.2013).
Mwenyekiti wa SPD Sigmar Gabriel akihutubia mkutano wa chama chake mjini Leipzig.(16.11.2013).Picha: picture-alliance/dpa

Katika hotuba yake ya dakika 20 iliojaa hamasa ya kufunga mkutano huo amesema hatokiongoza chama cha SPD miaka 150 baada ya kuasisiwa kwake kwa kuingia kwenye makubaliano ambayo hana imani nayo kamili.

Hotuba ni zinduo

Ralf Stegner waziri mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein amesema hotuba hiyo ya Gabriel ilikuwa ni zinduo kwa chama na amewahimiza wenzake kuwa wajumbe wenye misimamo imara katika mazungumzo ya serikali ya mseto kuliko wale wa chama cha Free Demokratik wenye kupendelea biashara ambao ni washirika wa zamani wa Merkel katika serikali ya mseto

Amesema "Hatutotelekeza uaminifu wetu kwa ajili ya kudhibiti nyadhifa chache za wizara.Chama cha SPD hakipatikani kwa kutumia masharti yaliotumika kwa chama cha Free Demokratik".

Ralf Stegner Waziri Mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein kutoka chama cha SPD.
Ralf Stegner Waziri Mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein kutoka chama cha SPD.Picha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa Merkel bungeni Volker Kauder pia ameonekana kujiandaa kuridhia hilo kwa kuliambia gazeti mashuhuri la "Bild am Sonntag" katika matamshi aliyoyatowa kabla ya chapisho lake la Jumapili kwamba " ukuaji wa uchumi na ajira havipaswi kuathirika " kutokana na kuanzishwa kwa kima hicho cha chini cha mshahara.Baadhi ya viongozi wa kibiashara wana wasi wasi kwamba kitadhoofisha ushindani.

Kauder amesema ingelikuwa busara zaidi kuanzisha kima cha chini cha mshahara hatua kwa hatua katika iliokuwa Ujerumani Mashariki ambapo mishahara ni ya chini na ukosefu wa ajira ni mkubwa ili kuepuka kuzihatarisha ajira. Lakini vyama vya wafanyakazi vyenye kuunga mkono SPD yumkini ikawawia vigumu kulikubali jambo hilo.

Volker Kauder Mwenyekiti wa wa kundi la wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU katika bunge la Ujerumani.
Volker Kauder Mwenyekiti wa wa kundi la wabunge wa vyama ndugu vya CDU/CSU katika bunge la Ujerumani.Picha: John Macdougall/AFP/Getty Images

Chama cha SPD pia kinadai kuridhiwa kwa madai yao ya kuwepo kwa uraia wa nchi mbili kwa raia ambao sio wa nchi za Umoja wa Ulaya jambo ambalo wahafidhina wa Merkel wamekuwa wakilipinga kwa muda mrefu. Hilo ni suala kubwa kwa jamii ya Waturuki walio wachache nchini Ujerumani ambalo Merkel hivi sasa inaonekana pia yuko tayari kuliridhia.

Mwandishi: Mohamed Dahman/Reuters/DW

Mhariri:Mtullya Abdu