1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel ataka marekebisho makubwa katika Mkataba wa Umoja wa Ulaya

Baada ya kukamilisha mazungumzo yake na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa hapo jana, asubuhi ya leo (02.11.2011) Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelihutubia Bunge la Ujerumani.

Kansela Angela Merkel akihutubia Bunge la Ujerumani.

Kansela Angela Merkel akihutubia Bunge la Ujerumani.

Katika hotuba yake, Merkel amelifahamisha bunge matokeo ya mazungumzo hayo yaliyotuwama juu ya hali tete katka Kanda ya Sarafu ya Euro na kile ambacho Ujerumani itakiwasilisha katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya wiki ijayo, huko Brussels.

Lakini kitu kimoja kinachoweza kuelezeka kwa ufasaha ni kwamba Ulaya iko maji shingoni, na kwamba lazima kila jitihada zichukuliwe sasa, kabla haijazama kabisa.

Hata hivyo, Kansela Merkel ameliambia Bunge kwamba jitihada hizo hazipaswi kuwa za kukurupuka, kwani zitaliangamiza zaidi eneo linalotumia sarafu ya euro, badala yake wamekubaliana na Rais Sarkozy pawe na chombo maalum cha kudhibiti nidhamu za bajeti kwenye mataifa wanachama wa Kanda ya Euro haraka sana.

"Sio kwamba tunazungumzia tu umoja wa fedha kudhibiti bajeti, bali tayari tumeanza kuunda," alisema Merkel. Na huu utakuwa na kanuni kali, angalau kwenye eneo letu la euro." Amesema Merkel.

Kansela Merkel amesema kwamba kwa siku za hivi karibuni kimekuwa kipindi kigumu sana kwa Kanda ya Euro, kikishuhudia kuporomoka kwa masoko, kitisho cha deni la Ugiriki, na misuguano ya kisiasa ndani ya Umoja wa Ulaya wenyewe.

Merkel aendelea kukataa kutumika kwa dhamana za Ulaya

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Hata hivyo, Kansela Merkel amekataa katakata wazo la kutumia dhamana za Ulaya kutatua tatizo la madeni, akisema kwamba huko hakutasaidia kuikwamua sarafu ya euro.

"Serikali ya Ujerumani imeweka wazi msimamo wake kwamba matatizo ya sarafu ya euro hayatatuliwa kwa mkupuo mmoja, bali ni mchakato ambao utachukuwa muda mrefu. Huo ni ukweli tunaopaswa kuukubali sote," alisema Kansela huyo wa Ujerumani.

Katika mkutano wao wa jana, Kansela Merkel na Rais Sarkozy walikubaliana kuweka shinikizo kwa wanachama wengine wa Umoja wa Ulaya, kuupitia Mkataba wa Umoja huo, na ufanyiwe mageuzi yanayoendana na hali halisi ya sasa.

Akizungumza na kundi la watu wanaomuunga mkono hapo jana mjini Toulon, Ufaransa, Rais Sarkozy alisisitiza ulazima wa kuleta mageuzi hayo, ikiwemo pia kuweka adhabu kwa nchi zinazokiuka nidhamu ya bajeti. Sarkozy pia akawataka wananchi wake wawe tayari kwa hatua za kubana matumizi katika sekta ya umma.

"Lazima Mkataba wa Ulaya urekebishwe"

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto) na Knasela Angela Merkel wa Ujerumani.

Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron (kushoto) na Knasela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kupitia hotuba zote mbili, iliyotolewa jana na Sarkozy mjini Toulon, na ya Merkel leo Bungeni, wachambuzi wanasema kwamba kinachotafutwa sasa ni kuundika upya Mkataba wa Umoja wa Ulaya, kwa kile ambacho Kansela Merkel ameliambia Bunge ni "kuepusha mpasuko wa kisiasa kati ya mataifa ya Umoja wa Ulaya yaliyo wanachama wa Kanda ya Euro na yale yasiyo wanachama wa sarafu hiyo."

Itakumbukwa kuwa katika mkutano wa mwisho wa kilele uliofanyika Brussels mwanzoni mwa mwezi uliopita, Rais Sarkozy, ambaye nchi yake ni mwanachama wa Sarafu ya Euro, alitoa maneno makali dhidi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ambaye nchi yake si mwanachama wa sarafu hiyo. Sarkozy alimwambia Cameron, awache kuingilia mambo yasiyomuhusu.

Mkutano mwengine wa kilele unafanyika tarehe 9 mwezi huu mjini Brussels, na mapendekezo ya Ufaransa na Ujerumani juu ya mabadiliko ya Mkataba wa Umoja wa Ulaya, yanatarajiwa kuwa ajenda.

Mwandishi: Mohammed Khelef/PDA/AP/Reuters
Mhariri: Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com