Merkel aipa matumaini Ugiriki | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.08.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel aipa matumaini Ugiriki

Juhudi za kuutatua mgogoro wa madeni ya Ugiriki zinaendelea barani Ulaya, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameipa matumani Ugiriki hii leo (24.08.2012) akisisitiza kwamba anaitaka nchi hiyo kubakia ndani ya Umoja huo.

Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Samaras.

Kansela Angela Merkel akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wake na Samaras.

Merkel ameahidi kwamba nchi yake itaisaidia Ugiriki.Hata hivyo Ugiriki kwa upande wake inasema nchi hiyo haitaki msaada zaidi wa kifedha kutatua matatizo yake bali inahitaji muda wa kupumua.ili ijipange kukabiliana na hatua za kufunga mkaja pamoja na mageuzi.Saumu Mwasimba ameufuatilia mkutano kati ya Ugiriki na Ujerumani na kuandaa taarifa ifuatayo.

Baada ya kukutana na waziri mkuu wa Ugiriki Antonis Samaras hii leo ,Kansela Merkel alitoka akiwa na msimamo imara juu ya suala la mgogoro wa madeni wa nchi hiyo ya Ugiriki. ''Nataka kuweka wazi kama ambavyo nimekuwa nikisema tangu ulipoanza mgogoro huo wa kiuchumi,na huu pia ndio msimamo wa serikali yangu kwamba Ugiriki ni sehemu ya kanda ya Yuro na ninataka kuiona Ugiriki inabakia kuwa sehemu ya kanda hiyo.''

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande

Akisimama bega kwa bega na waziri mkuu wa Ugiriki Kansela Merkel amesema anaamini kwamba serikali mpya ya Ugiriki chini ya uongozi wa waziri mkuu Samaras inafanya kila iwezalo kuyatatua matatizo yanayoikabili nchi hiyo.Kansela Merkel amewahakikishia wagiriki kwamba Ujerumani itawasaidia katika kila hatua ya kuondokana na matatizo ya madeni,akisisitiza

''Ili kuirudisha tena imani yetu ,ni lazima mmatarajio yetu yatimizwe na kwahivyo nimeweka bayana katika mazungumzo ya leo kwamba tunaitarajia Ugiriki izingatie mapendekezo yetu.Tunatarajia kwamba nchi hiyo itachukua hatua ya kutimiza ahadi zake,'' alisema Merkel.

Samaras asema Ugiriki itatimiza wajibu wake

Waziri mkuu wa Ugiriki ameahidi kutekeleza ahadi zote zilizotolewa na serikali yake kwa wakopeshaji wa Kimataifa akisema kwamba nchi hiyo haihitaji msaada zaidi wa fedha bali inataka nafasi ya kupumua kukabiliana na matatizo yake.Samaras yuko katika ziara ya siku mbili Ulaya Kaskazini iliyoanzia Berlin na itakayomfikisha pia Ufaransa hapo kesho ambako atakutana na rais Francois Hollande.Ziara hii ni ya kutafuta uungaji mkono wa nchi hizo mbili zenye sauti kubwa ndani ya kanda ya Yuro,juu ya kutaka kupewa muda zaidi wa kupunguza mabilioni ya Yuro katika bajeti yake.

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande

Kansela Angela Merkel na rais wa Ufaransa Francois Hollande

Itakumbukwa kwamba Ugiriki iliyopewa msaada wa yuro billioni 130 wa kuisadia kujikwamua na madeni iliahidi kufanya mageuzi chungunzima ikiwa ni pamoja na kupunguza bajeti yake katika mwaka 2013 na 2014.Lakini kutokana na kiwango cha madeni kuwa kikubwa zaidi na hali ya kiuchumi kuwa mbaya inasadikiwa kwamba waziri mkuu Samaras anataka muda zaidi ya miaka 4 kuweza kuipunguza nakisi ya bajeti iliyosababishwa na mgogoro huo wa madeni.

Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri: Mohammed AbdulRahman

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com