Meli ya abiria yapinduka; nahodha awekwa korokoroni
15 Januari 2012Vyombo vya habari nchini Italia vimeripoti jana kuwa nahodha wa meli ya abiria , inayojulikana kama Costa Concordia , ambayo ilipinduka katika pwani ya Toscana , nchini Italia, ikiwa na abiria 4,000 amekamatwa wakati uchunguzi unafanyika juu ya madai ya kuuwa bila kukusudia na kuitelekeza meli yake.
Meli hiyo ya abiria iligonga mwamba baharini na kusababisha tundu la mita 70 hadi 100 katika eneo lake la mbele , muda mfupi baada ya kuanza safari siku ya Ijumaa kutoka bandari ya Civitavecchia karibu na Rome. Kiasi ya watu 42 wamejeruhiwa , ambao watu wawili hali zao ni mbaya na wengine 41 ambao ni miongoni mwa watu waliokuwa ndani ya meli hiyo wakiwa hawajulikani waliko. Meli hiyo ilikuwa ikielekea katika bandari ya Savona kaskazini-magharibi ya Italia na ilitarajiwa kusimama katika bandari za Marseille nchini Ufaransa pamoja na Barcelona nchini Hispania.