1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mchuano wa kombe la mataifa ya Afrika kati ya Misri na Jamhuri ya Afrika ya Kati wasongezwa hadi Juni

17 Februari 2012

Mchuano wa kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya bara la Afrika kati ya Misri na Jamhuri ya Afrika ya Kati umeahirishwa hadi mwezi Juni kufuatia ghasia za soka mjini Port Said zilizowauwa watu 74 Februari mosi.

https://p.dw.com/p/145CD
Wachezaji wa timu ya Al-Ahly wakitoroka ghasia uwanjani
Wachezaji wa timu ya Al-Ahly wakitoroka ghasia uwanjaniPicha: picture-alliance/dpa

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limethibitisha kuwa mchuano huo uliotarajiwa kugaragazwa mnamo Februari 29, umepangwa upya. Shirikisho la Soka la Misri wiki iliyopita liliwaomba wenzao wa Jamhuri ya Afrika ya Kati likitaka mchuano huo uhairishwe na CAF imethibitisha makubaliano hayo. Nchi hizo mbili sasa zitavaana wikendi zitakazofuatana mwezi Juni. Mkondo wa kwanza utachezwa mjini Cairo Juni 15 na kisha mkondo wa pili mjini Bangui Juni 24.

Botswana ambao waliwashangaza wengi baada ya kufuzu katika mechi za kombe la mataifa ya bara la Afrika wamekataa ombi la kucheza mechi ya kirafiki na mabingwa wa zamani wa kombe hilo Misiri mwezi huu kwa sababu hawawezi kukichagua kikosi. Kocha wa Bostwana Stanley Tshosane aliliambia shirika lake la habari kukataa mwito huo wa kucheza tarehe 29 mwezi huu wa Februari kwa sababu hakuwa na uhakika yule angemchagua katika kikosi hicho. Alisema wengi wa wachezaji wakongwe wakikosi hicho walidokeza kuwa wanajiuzulu soka ya kimataifa na hivyo hangeweza kuwa na kikosi chochote kwa mchuano huo wa kirafikii dhidi ya Misri.

Kocha wa Zambia kuongezwa mkataba

Mfaransa Herve Renard anatarajiwa kuongeza mkataba wake kama kocha wa Zambia kwa miaka mingine miwili, siku chache tu baada ya kuongoza nchi hiyo katika kutwaa taji lake la kwanza la kombe la mataifa ya bara la Afrika. Renard ambaye mkataba wake ulitarajiwa kukamilika mwaka huu, atasalia kama kocha wa Zambia hadi baada ya fainali za kombe la dunia mwaka 2014. hayo ni kulingana na waziri wa michezo Chishimba Kambwili, ambaye alisema watautia saini mkataba huo hivi karibuni na kumpa kocha huyo donge nono ili asivutiwe na nchi nyingine ambazo zinamwinda.

Kocha wa Zambia Herve Renard
Kocha wa Zambia Herve RenardPicha: picture-alliance/dpa

Katika soka ya Ujerumani ni kwamba mabingwa Borussia Dortmund watakuwa bila ya huduma za kiungo mshambuliaji Shinji Kagawa kwa hadi wiki tatu baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu akiwa mazoezini. Mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Japan, ambaye alikosa awamu ya kwanza ya msimu baada ya kuvunjika mguu, amefunga magoli saba na kuwasaidia Dortmund kuchukua uongozi wa ligi kwa faida ya pointi mbili.

Man City yalalamika rasmi kuhusu madai ya kibaguzi

Nchini Uingereza klabu ya Manchester City imewasilisha ombi rasmi kwa shirikisho la soka barani ulaya UEFA, ikidai kuwa baadhi ya wachezaji wake walitolewa matamshi ya kibaguzi na baadhi ya mashabiki wakati wa mchuano wao walioushinda wa Europa League dhidi ya Porto siku ya Alhamisi. Mshambulizi Muitalia Mario Balotelli aliwaambia maafisa kuwa alizisikia sauti za kumuiga tumbili kutoka kwa mashabiki naye kiungo wa kati Yaya Toure akisema pia alisikia kitu kama hicho. Toure alisema ndio maana wanapenda kucheza soka yao katika Primia league kwa sababu matukio ya aina hiyo hayapo.

Stürmer Mario Balotelli aufgenommen am Samstag (29.08.2009) während des Serie A-Spiels AC Mailand gegen Inter Mailand im San Siro Stadion in Mailand, Italien. Foto: Daniele Badolato +++(c) dpa - Report+++
Mario BalotelliPicha: picture-alliance/ dpa

Wakati huo huo kocha wa klabu ya Chelsea Andre Villas Boas amekiri kuwa baadhi ya wachezaji wake hawamuungi mkono. Mkufunzi huyo amekuwa na kipindi kigumu cha msimu huu uwanjani Stamford Bridge tangu alipochukua nafasi ya Carlo Ancelotti msimu uliopita na matokeo duni ya hivi punde yameibua mnong'onozano miongoni mwa wachezaji wake.

Ubaguzi wa kijinsia katika mashindano ya Olimpiki

Mwenyekiti wa mashindano ya Olimpiki jijini London mwaka 2012 amesema Kamati ya Olimpiki - IOC inahitaji kuhimiza umoja zaidi kutoka kwa nchi ambazo haziwatumi wanawake katika mashindano hayo lakini akaonya kuwa michezo siyo tiba ya maovu yote. Sebastian Coe, mwenyekiti wa michezo ya Olimpiki ya London amesema michezo inaweza kutumiwa kwa njia fulani kuhimiza mabadiliko ya kijamii. Lakini akaongeza kuwa wakati mwingine kunakuwepo vizingiti ambavyo haviwezi kuvunjwa kwa usiku mmoja.

Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadam - Human Rights Watch mapema wiki hii liliwashtumu waandalizi wa mashindano ya Olimpiki kutofanya juhudi za kutatua suala la ubaguzi wa kijinsia katika mataifa ya ghuba; Saudi Arabia na Qatar pamoja na nchi ndogo ya Kusini Mashairiki ya Asia Brunei. Shirika hilo lilisema, ukweli kwamba wanawake na wasichana hawawezi kufanya mazoezi ili kushiriki kwenye mashindano hayo unaonyesha wazi ukiukaji wa ahadi ya mkataba wa Olimpiki kuhusu usawa na hivyo unayapaka doa mashindano yenyewe ya Olimpiki. Nchi hizo tatu hazijawahi kumtuma mwanariadha wa kike kwenye mashindano ya Olimpiki, ijapokuwa Qatar imetangaza nia yake ya kuwatuma wanariadha wa kike katika mashindano ya Olimpiki jijini London mwaka huu wa 2012.

Nembo ya mashindano ya Olimpiki jijini London 2012
Nembo ya mashindano ya Olimpiki jijini London 2012Picha: picture-alliance/dpa

Katika riadha ni kuwa Mkenya Vivian Cheruyiot, ambaye ni bingwa wa ulimwengu katika mbio za mita 5,000 na 10,000, alijiondoa kutoka mashindano ya leo Jumamosi mjini Birmingham katikati mwa Uingereza baada ya kupatwa na homa. Cheruyiot, ambaye ni mmoja wa wale wanaotazamiwa kunyakua dhahabu katika mashindano ya Olimpiki mwaka huu jijini London Uingereza, alitarajiwa kushiriki katika mbio za mita 3,000 za National Indoor Arena. Lakini mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 28 alisema kupitia taarifa kuwa kabla ya kuanza safari yake kutoka Nairobi kuelekea Uingereza, aliüatwa na homa na hakujiskia vyema kusafiri. Aliongeza kuwa atachukua kipindi cha mapumziko kabla ya kurejea mazoezini kikamilifu.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman