1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbunge mwingine auwawa

20 Septemba 2007

Mauaji ya hivi karibuni ya mwanasiasa mwingine nchini Lebanon ni ishara tosha kwamba nchi hiyo inakabiliwa na sintofahamu ya kisiasa huku uchaguzi wa rais ukitarajiwa kufanyika katika muda usio mrefu.

https://p.dw.com/p/CH7x
Waziri mkuu Fuad Siniora
Waziri mkuu Fuad SinioraPicha: AP

Wachambuzi wa kisiasa hata hivyo wanasema hali hiyo inaitumbukiza Lebanon iliyogawanyika katika migogoro zaidi.

Mauaji hayo ya wanasiasa sio tu ujumbe unaopelekewa wanachama wa kundi kubwa linalotawala la March 14 lakini ishara hiyo ni sawa na kusema kwamba hali ya mgawanyiko nchini Lebanon inaongezeka hayo ni kwa mujibu wa mchambuzi wa maswala ya kisiasa bibi Amal Saad-Ghorayeb.

Tangu mwaka 2005 wanasiasa wanane wanaopinga mahusiano na Syria wameuwawa katika mazingira ya wingu zito la mauaji yasiyo na jibu.

Hivyo basi kuuwawa kwa mjumbe mwingine wa kundi la Marchi 14 Antoine Ghanem hapo siku ya jumatano kumetokea tu wakati makundi mawili yanayopingana yalielekea kufikia maelewano.

Mchambuzi wa maswala ya kisiasa bibi Amal Saad-Ghorayeb anahoji mazingira ya kutatanisha kufuatia kifo cha mjumbe Ghanem wakati ambapo makundi ya March 14 upande ulio na wengi unaotawala nchini Lebanon na March 8 upande wa upinzani unaoungwa mkono na Syria yakiwa katika muelekeo wa kufanya mazungumzo.

Hapa bibi Ghorayeb analenga mkutato uliopangiwa kufanyika kati ya spika wa bunge na kiongozi muhimu wa upinzani Nabih Berri pamoja pia na wanachama wa kundi la wengi linalotawala linaloungwa mkono na nchi za magharibi akiwemo kiongozi wao bungeni Saad Hariri.

Spika wa bunge Nabih Berri alikuwa atakutana pia na kiongozi mwenye ushawishi mkubwa wa kundi la Christian Maronite Nasrallah Sfeir leo hii siku ya ijumaa.

Mikutano hiyo sasa imeahirishwa lakini ililenga kutafuta maelewano kabla ya kikao cha bunge cha siku ya jumanne ambacho kingemchagua mrithi wa rais Emile Lahoud anaeungwa mkopno na Syria na ambae muda wake unamalizika mwezi Novemba.

Bunge la Lebanon linahitajika kumchaguwa rais mpya kati ya Septemba 25 na Novemba 24 jambo ambalo wadadisi wa maswala ya siasa nchini Lebanon wanasema kuwa pande zote mbili zinajaribu kujinufaisha kisiasa na kwamba huenda kuuwawa kwa mjumbe Ghanem kunalenga kutowa hisia kali kabla ya uchaguzi wa rais kufanyika na wakati huo huo kuongeza mafuta katika moto ambao tayari unawaka.

Kitendawili cha mauji ya wanasiasa nchini Lebanon kinaongeza hali ya wasiwasi baina ya makundi mawili yanayopingana upande unaotawala na upande wa upinzani ni kitendawili ambacho Walebanon wenyewe hawawezi kukifumbua.

Antoine Ghanem ni mjumbe wa nane kuuwawa miongoni mwa wajumbe wanaopinga ushawishi wa Syria nchini Lebanon kifo chake ni tangu kuuwawa mwezi Februari mwaka 2005 aliyekuwa waziri mkuu wa Lebanon Rafik Hariri.

Kifo cha Ghanem kimepunguza idadi ya wajumbe wa chama chake hadi kufikia 68 katika idadi jumla ya wabunge 127 wa bunge la Lebanon.

Wingi wa wajumbe una umuhimu mkubwa katika kumchagua rais mpya wa nchi hiyo.

Mzozo wa kisiasa nchini Lebanon uliongezeka mara pale mawaziri sita wa upinzani wanaoungwa mkono na Syria walipotangaza kujiondoa kutoka katika serikali ya waziri mkuu Fuad Siniora anaeungwa mkono na nchi za magharibi.

Wadadisi wa maswala ya siasa wanasema kwamba kutokufikiwa muafaka na pande zote za kisiasa nchini Lebanon juu ya kumchagua rais wa nchi hiyo kutasabisha mvutano wa kugombea madaraka au hata kusababisha kuanzishwa serikali mbili na hivyo kuirudisha Lebanon katika miaka ya 1975 hadi 1990 kulipozuka vita vya wenyewe kwa wenyewe wakati pande mbili zilipopigania kutawala.