Mbinyo wazidi dhidi ya Assad, msaada wafika Homs
25 Februari 2012Mkutano wa zaidi ya mawaziri wa mambo ya kigeni 60 nchini Tunisia umeshuhudia miito ya kutaka vikosi vya kulinda amani vya mataifa ya kiarabu kuingilia kati na upinzani kupewa silaha , pamoja na onyo lililotolewa na Marekani kuwa Assad atawajibika kwa kiasi kikubwa kwa kudharau utashi wa kimataifa.
Waliojeruhiwa wapatiwa msaada
Katika ishara ya mwanzo kuwa mbinyo unaoongezeka huenda ukawa na athari kwa utawala huo, magari ya kubebea wagonjwa ya shirika la kimataifa la msalaba mwekundu na hilali nyekundu yameingia katika wilaya ya Baba Amr katika mji uliozingirwa wa Homs na kuwaondoa Wasyria saba waliojeruhiwa katika mashambulio ya makombora yaliyofanywa na jeshi la serikali.
Magari matatu ya kubebea wagonjwa yameingia katika eneo la Baba Amr na yameondoka. Yamewaondoa hadi sasa watu saba waliojeruhiwa ambao ni raia wa Syria , msemaji wa shirika hilo la kimataifa la msalaba mwekundu Saleh Dabbakeh ameliambia shirika la habari la AFP mjini Damascus.
Lakini waandishi habari wawili kutoka mataifa ya magharibi ambao wamejeruhiwa bado hawajaondolewa, pamoja na miili ya waandishi habari wengine wawili, ameongeza Dabbakeh.
Majadiliano yanaendelea pamoja na maafisa wa Syria na upande wa upinzani katika juhudi za kuwaondoa watu wote , bila kubagua , ambao wanahitaji msaada wa haraka, amesema.
Vikwazo viongezwe
Mjini Tunis , mkutano wa kwanza wa kile kinachoitwa "marafiki wa Syria", umetoa azimio linalotaka kumalizwa mara moja kwa ghasia na kuwekwa vikwazo vipya.
Kundi hilo limeitaka serikali ya Syria kusitisha mara moja ghasia na matumizi ya nguvu ili kuruhusu makundi ya kutoa misaada kuweza kuwafikia walengwa na kuamua kuchukua hatua za kuweka vizuwizi na vikwazo kwa utawala huo wa Syria.
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton amesema kuwa Assad ajawajibika kwa kiasi kikubwa kwa kudharau matakwa ya jumuiya ya kimataifa.
Utawala wa rais Assad umepuuzia kila onyo, na kupoteza kila nafasi , na kuvunja kila makubaliano, Clinton amesema. Ikikabiliwa na maandamano ambayo hayakomi ambapo waandamanaji wanadai haki zao za kimsingi na utu wao, utawala huo unajenga hali ya kutisha ya kiutu.
Msaada wa kiutu
Clinton pia ametangaza msaada wa dola milioni 10 kwa ajili ya juhudi za msaada wa kiutu nchini Syria.
Mjini Washington rais Barack Obama amewaambia waandishi habari ; "Tutaendelea na mbinyo na kuaangalia kila nyenzo inayopatikana kuweza kuzuwia mauaji ya raia wasio na hatia nchini Syria".
Ni muhimu kuwa hatuwi watazamaji tu wakati wa matukio haya yasiyo ya kawaida, ameongeza.
Na huko Syria kwenyewe , kiasi watu 53 zaidi wameuwawa katika ghasia mpya jana Ijumaa, siku mbili kabla ya kufanyika kura ya maoni nchini Syria kuhusu katiba mpya ambayo inaweza kumaliza miaka 50 ya utawala wa chama cha Baath, wakati madaraka makubwa yatakuwa kwa rais.
Tunisia ambayo imekuwa mwenyeji wa mkutano wa mataifa hayo marafiki wa Syria , imetoa wito kwa walinzi wa amani kutoka mataifa ya kiarabu kupelekwa nchini Syria kusaidia kumaliza mauaji, na kwamba Assad apewe kinga ili kumshawishi kuondoka madarakani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Sudi Mnette