Mazungumzo ya Sudan na Sudan Kusini yaendelea
4 Septemba 2012Sudan na Sudan Kusini zimekuwa zimekumbwa na msururu wa migogoro tangu Sudan Kusini ilipojitenga kutoka kwa jirani yake wa Kaskazini zaidi ya mwaka mmoja uliopita chini ya mkataba wa amani wa mwaka 2005. Mkataba huo ulimaliza miongo kadhaa ya vita.
Mapigano katika mpaka wenye umbali wa kilometa 1,800 yalitishia kuzitzmbukiza nchi hizo mbili katika vita kamili mnmo mwezi Aprili wakati Sudan Kusini ilipolichukuwa eneo tajiri la mafuta ambalo limedhibitiwa na Sudan kwa muda mrefu. Sudan Kusini ilifunga visima vyake vya mafuta mwezi Januari baada ya kushindwa kukubaliana na Sudan kuhusu ada inayostahili kulipa ili kusafirisha mafuta kupitia ardhi ya Sudan. Wanadiplomasia wan chi za Magharibi na wapatinishi wa Umoja wa Afrika sasa wanatarajia kukamilisha mazungumzo hayo baada ya nchi hizo mbili kukubaliana kuhusu mkataba wa mwanzo wa ada ya mafuta mwezi uliopita. Sudan inasema inataka mkataba wa usalama wa mpakani kabla ya usafirishaji mafuta kuanza tena.
Maafisa kutoka pande zote wameelezea matumaini makubwa kuhusu mazungumzo hayo kuliko jinsi ilivyokuwa katika mazungumzo ya awali. Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za kigeni wa Sudan, El-Obeid Morawah, anasema ujumbe wa Sudan uko tayari kufikia makubaliano ifikapo mwishoni mwa awamu hii ya mazungumzo.
Mwenyekiti wa kamati ya masuala ya mpakani ya Sudan kusini, Michael Makuei Leúeth, anasema ana matumaini kuhusu kutatua masuala kama vile ya biashara ya mpakani, hali ya uraia katika nchi hizo mbili, pamoja na jimbo linalogombaniwa la Abyei. Anasema kuwa ikiwa serikali ya Sudan inakwenda kufanya mazungumzo kwa nia njema, basi kuna uwezekano wa kukubali kila kitu isipokuwa tu mipaka ambayo itafuata baadaye.
Pande zote mbili zinahitaji sana mapato ya mafuta ili kuanzisha tena uchumi wao. Mafuta yalikuwa yakitoa zaidi ya nusu ya mapato ya serikali nchini Sudan na kuchangia takribani asilimia 98 ya mapato ya serikali nchini Sudan Kusini kabla ya visima hivyo kufungwa. Nchi zote mbili zinakabiliwa na ughali wa maisha na uhaba wa fedha za kigeni zinazohitajika kulipia chakula kutoka ng'ambo.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeweka Septemba 22 kuwa siku ya mwisho kwa nchi hizo mbili kutatua matatizo yao au zikabiliwe na vikwazo. atika kuanza, wapatanishi wanataka kujadili kuhusu kuwekwa eneo la amani mpakani lenye upana wa kilometa 10 ili kusaidia kuhakikisha kuwa upande wowote hauyasaidii makundi yenye silaha kuvuka mipaka, na kurejesha usafiri wa kawaida na bishara baina ya nchi hizo mbili.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Miraji Othman