1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia ya Iran kuanza leo Baghdad

Admin.WagnerD23 Mei 2012

Iran na Mataifa sita yenye nguvu duniani wanasaka mapatano ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo leo mjini Baghdad huku kukiwa na matumaini ya kukififisha kile ambacho Rais Barack Obama amekiita kuwa ni "kitisho cha vita" .

https://p.dw.com/p/150Ok
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Baraza la Usalama la Umoja wa MataifaPicha: AP

Kiini cha majadiliano hayo ni hofu juu ya miradi ya nyuklia ya Iran ambayo mataifa hayo yanaishuku kuwa ni mwanzo wa kulekea kwenye utengenezaji wa silaha za atomiki ingawa nchi hiyo imekanusha na kusema kuwa mpango wake huo ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Mataifa ya magharibi yana wasiwasi huenda nchi hiyo ikazidi kuvuruga amani kwenye nchi za Mashariki ya Kati ambazo tayari ziko katika hali mbaya kutokana na machafuko ya mara kwa mara, pamoja na kuzizika juhudi za kimataifa za kuzuia utengenezaji wa silaha za nyuklia zinazoendeshwa kwa miaka 60 sasa.

Viongozi wanaoshirki mkutano huo wamepaza sauti zao wakiitahadharisha Iran kutokuvuruga mazungumzo hayo, lakini pia wakiahidi kuwa tayari kuisaidia nchi hiyo kusonga mbele endapo itaonyesha ushirikiano na kuuweka wazi mpango wake wa nyuklia.

Shabaha kuu kwenye majadiliano hayo ni kuifanya Iran ipunguze kiwango cha urutubishaji wa madini ya Uranium pamoja na kuruhusu Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki, IAEA, kuvikagua vinu vyake vya nyuklia kikiwemo cha Puchin kama alivyoeleza Mkuu wa shirika hilo Yukia Amano

Kundi hilo linaloongozwa kwenye mazungumzo hayo na Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashiton, linatarajia kutoa matakwa yake kwa Iran ambayo itawakilishwa na kiongozi wake wa mazungumzo ya nyuklia Saeed Jalili ikiwemo suala la kujenga ujasiri.

Said Jalili, Kiongozi wa mazungumzo ya nyuklia wa Iran
Said Jalili, Kiongozi wa mazungumzo ya nyuklia wa IranPicha: Fars

Hakuna nia ya kulegeza vikwazo dhidi ya Iran

Nchi za magharibi zimesema kuwa hazitarajii kulegeza vikwazo vya kiuchumi zilizoiwekea Iran ambavyo vinatajwa kuongeza makali ya shinikizo kwa taifa hilo. Mazungumzo ya sasa ni yanafuatia yale yaliyofanyika mjini Instanbul zaidi ya mwezi mmoja uliopita.

Mazungumzo ya Baghdad yanafanyika muda mfupi baada ya Amano kutangaza kuwa IAEA iko mbioni kusaini makubaliano ya ukaguzi wa vinu vya nyuklia na Iran.

Hapo jana Marekani ilitangaza kuiwekea vikwazo vya kiuchumi nchi hiyo kama hatua ya kuishinikiza kukubali matakwa ya mataifa hayo juu ya mpango wake wa nyuklia vikiongeza idadi ya vile ambavyo tayari vimekwishawekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Umoja wa Ulaya.

Rais wa nchi hiyo Barack Obama ameapa kuendeleza shinikizo hadi hapo mambo yatakapokaa sawa.

Barack Obama, Rais wa Marekani
Barack Obama, Rais wa MarekaniPicha: Reuters

Iran inarutubisha madini ya Uraniumu kwa kiasi cha asilimia 20 kiwango ambacho wataalamu wanasema kuwa ni sawa na asilimia 90 ya urutubishaji unaohitajika kutengeneza silaha za nyuklia.

Wawakilishi wa nchi tano Wananchama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanaoshiriki mazungumzo hayo yaani Urusi, China, Marekani Ufaransa, na Uingereza tayari wanaelekea katika eneo la mkutano. Ujerumani pia inashiriki mazungumzo hayo.

Mwandishi: Stumai George/Reuters/ AFP

Mhariri: Hamidou Oummilkheir