Mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini yaanza leo mjini Beijing | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.03.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini yaanza leo mjini Beijing

Marekani na Korea Kaskazini zimeutanzua mzozo wa zaidi ya dola milioni 25 za kimarekani huku mazungumzo ya mataifa sita kuhusu mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini yakianza leo mjini Beijing nchini China.

Mjumbe wa Marekani kwenye mkutano wa Beijing Cristopher Hill

Mjumbe wa Marekani kwenye mkutano wa Beijing Cristopher Hill

Marekani na Korea Kaskazini zimeusuluhisha mzozo juu ya kiwango cha zaidi ya dola milioni 25 za kimarekani zilizokuwa zikizuiliwa katika benki moja ya Macau. Maafisa wa Marekani wamesema hatua hiyo imeondoa kikwazo kikubwa kilichoyakabili mazungumzo ya mataifa sita juu ya mpango wa nyuklia wa Korea Kaskazini. Mazungumzo hayo yameanza leo mjini Beijing China.

Mjumbe wa Marekani katika mazungumzo ya mataifa sita ya mpango nyuklia wa Korea Kaskazini, Christopher Hill, amesema kutanzuliwa kwa mzozo huo ni muhimu kwa maslahi ya pande zote husika. Ana matumaini halitakuwa tatizo tena kadri wanavyoendelea na mazungumzo.

´Swala la kuzuiliwa kwa fedha limekuwa swala nyeti kwa miezi kadhaa iliyopita. Lakini nina hakika halitakuwa tatizo kadri tunavyoendelea mbele na mazungumzo. Swala muhimu ni kusonga mbele katika hatua mpya ya mazungumzo, kukomesha mpango wa nyuklia baada ya siku sitini na kuweza kufikia hatua ya kusaini mkataba. Nafikiri maswala yote mawili yatakuwa muhimu kati ya mambo tutakayoyafanya leo.´

Afisa wa wizara ya fedha ya Marekani, Daniel Glaser, amesema fedha za Korea Kaskazini zilizokuwa zikizuiliwa katika benki ya Banco Delta Asia, BDA, huko Macau, zitarudishwa mjini Pyongyang kupitia benki ya China mjini Beijing. Glaser ameaambia waandishi wa habari mjini Beijing kwamba wamehakikishiwa fedha hizo zitatumiwa kwa kugharimia huduma za kiutu na elimu. Hata hivyo, marufuku dhidi ya taasisi za fedha za Marekani zinazofanya biashara na Banco Delta Asia haitafutiliwa mbali. Marekani inailaumu benki hiyo kwa kutumiwa na Korea Kaskzini kufanya biashara isiyo halali.

Mtaalamu wa China wa mswala ya nyuklia ya Korea Kaskazini katika chuo kikuu cha Renmin mjini Peking, Jin Canrong, ameonya juu ya mauzungumzo ya mjini Beijing.

´Mtu hatakiwi kuwa na matumaini makubwa kabla ya mkutano huo lakini tunatakiwa bila shaka kuwa na ujasiri kwa sababu kuna ishara kadhaa za matumaini. Bado kuna shaka shaka ikiwa kweli mkataba utafikiwa. Tatizo kubwa, kama ilivyokuwa hapo zamani, ni kukosekana uaminifu baina ya Marekani na Korea Kaskazini.´

Aidha Canrong amesema umoja uliodhihirishwa na jumuiya ya kimataifa umeivunja makali Korea Kaskazini.

´Kuungana pamoja kwa jumuiya ya kimataifa kumeibinya Korea Kaskazini na kuinyima nafasi ya kuendelea na mchezo wake. Wakati huu Korea Kaskazini inakabiliwa na shinikizo kubwa. Juu ya hayo, mashirika ya kimataifa yameonya kwamba Korea Kaskazini mwaka huu iko katika tatizo kubwa kiuchumi. Kwa hiyo Korea Kaskazini haina nguvu.´

Mjumbe wa Korea Kaskazini katika mazungumzo ya Beijing, Kim Kye-Gwan, amesema mazungumzo yameanza leo huku serikali ya Pyongyang ikisema itakifunga kinu chake cha nyuklia cha Yongbyon, mara tu itakapopokea dola milioni 25. Kiongozi huyo ameongeza kusema shuhguli zote katika kinu hicho zitakomeshwa ikiwa vikwazo vyote dhidi ya Korea Kaskazini vitaondolewa.

 • Tarehe 19.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHHy
 • Tarehe 19.03.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/CHHy

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com