1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya amani ya Afganistan

Admin.WagnerD4 Oktoba 2016

Mazungumzo ya kimataifa ya siku mbili kuhusu amani ya Afghanistan yameanza leo mjini Brussels huku yakigubikwa na mapigano kati ya vikosi vya usalama na wanamgambo wa Taliban

https://p.dw.com/p/2Qqvn
Afghanistan Kämpfe gegen Taliban in Kundus
Wanajeshi wa jeshi la Afghanistan katika makabiliano na waasi wa Taliban mjini KunduzPicha: Reuters/N. Wakif

Mkutano huo unayakutanisha mataifa 70, pamoja na asasi za kimiataifa 30. Shabaha ikiwa kutoa ahadi za kisiasa na kifedha kusaidia maendeleo ya taifa hilo hadi mwaka 2020. Pamoja na mabilioni ya dola misaada ambayo yametolewa kwa nchi hiyo katika kipindi cha miaka 15 iliyopita bado Afghanistan imeendelea kuwa taifa masikini zaidi duniani na kutokuwa na utengamano wa kisiasa huku rushwa ikilitafuna taifa hilo.

Suala la usalama linabaki kuwa la wasiwasi, wakati jeshi lenye mafunzo duni la nchi hiyo linakabiliana na majukumu ya kulinda usalama, wakati huo huo kundi la Dola la Kiislamu linaongeza kitisho chake.

Siku ya pili ya mapigano

Afghanistan | Kampf um Kunduz
Wanajeshi wa Afghanistan katika mapambanoPicha: picture-alliance/AP Photo/N. Rahim

Mashambulizi ya Taliban mjini Kunduz yanaingia siku yake ya pili leo hii, ikiwa zaidi ya mwaka baada ya kundi hilo la wenye itikadi kali kuuteka mji huo kwa kipindi cha wiki mbili. Leo hii vikosi vya serikali vinaelezwa kufanya operesheni ya kusafisha mji huo, huku likiwaonya wanamgambo wa Taliban waliojificha katika makazi ya watu baada ya operesheni za kijeshi zilizofanikishwa kwa msaada wa mashambulizi ya angani ya NATO.

Maafisa wanasema kwa kiasi fulani mapigano yanaendelea katika maeneo ya kimkakati ya viunga vya jiji la Kunduz lakini katika maeneo ya katikati ya mji huo kumekuwa hakuna kabisa wapiganaji wa Taliban na kwamba mmoja wa maafisa hao anasema mamia ya wa wanamgambo waliuwawa katika operesheni hiyo.

Mohammed Qasim Jangalbagh, mkuu wa polisi  amethibitisha kutokea idadi kubwa ya vifo lakini alisema mpaka wakati huu hawajawa na idadi kamili. Mmoja kati ya wanajeshi ya Afghanistan Nohammad Wadood alisikika akisema "Tumefanya operesheni iliyofanikiwa sana na maadui hawajawa na uwezo wa kukabiliana nasi. Tunawahakikishia watu wa Kunduz tutawaangamiza maadui wote na utakuwa shuhuda wa hilo"

Lakini mkazi Habib Khan alikuwa na tathimini tofauti "Mpaka wakati huu ni eneo ambalo lipo katika uelekeo wa Chuo Kikuu tu ndio lipo katika udhibiti wa majeshi ya Afghanistan lakini maeneo mengine yaliosalia yanadhibitwa na Taliban.

Taarifa ya NATO kuhusu operesheni

Katika mtandao wake wa Twitter, jeshi la NATO nchini Afghanistan limesema serikali inaudhibiti mji wa Kunduz, wakati Wizara ya Ulinzi ya Marekani nayo ikithibitisha kuwa jeshi lake limeendesha operesheni yake ya mashambulizi ya angani bega kwa bega na vikosi vya Afghanistan.

Kimsingi lengo la mazungumzo yanayoanza leo mjini Brussels ambao yanaratibiwa na Umoja wa Ulaya ni kukusanya fedha katika kipindi cha miaka minne toka sasa, kwa kiwango cha bilioni 4 kwa mwaka kama ilivyoahidiwa mwaka 2012 shabaha ikiwa kufikisha kikomo mapigano kama hayo.

Mwandishi: Sudi Mnette RTR
Mhariri: Daniel Gakuba