1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo kutafuta serikali mpya yaendelea Ugiriki

7 Novemba 2011

Pirika pirika za kisiasa zimeanza nchini Ugiriki kuunda serikali ya muungano ambayo itaidhinisha mkopo wa kanda ya sarafu ya Euro kuikwamua nchi hiyo na hatari ya kufilisika.

https://p.dw.com/p/136EH
Waziri mkuu anaeondoka madarakani Ugiriki George PapandreouPicha: dapd

►Pirika pirika za kisiasa zimeanza nchini Ugiriki kuunda serikali ya muungano ambayo itaidhinisha mkopo wa kanda ya sarafu ya Euro kuikwamua nchi hiyo na hatari ya kufilisika. Maafikiano yalifikiwa usiku wa kuamkia leo baada ya mazungumzo marefu baina ya serikali na upinzani, ambamo pia imekubaliwa kuwa waziri mkuu wa sasa, George Papandreou, ataachia madaraka. Kitendawili sasa ni nani atachaguliwa kuchukua nafasi hiyo.

Makubaliano ya kuundwa kwa serikali mpya yalifikiwa baada ya mazungumzo baina ya waziri mkuu anaeondoka madarakani, George Papandreou, na kiongozi wa kambi ya upinzani, Antonis Samaras. Mkutano huo ulioendelea hadi usiku wa manane uliongozwa na rais wa Ugiriki, Karolos Papoulias.

George Papandreou und Karolos Papoulias
Rais wa Ugiriki Karolos Papoulias akizungumza na waziri mkuu anaeondoka madarakani, Papandreou.Picha: dapd

Jina la waziri mkuu mpya na pia serikali atayoiongoza vinatarajiwa kutangazwa baadaye leo baada ya mazungumzo yanayoendelea hivi sasa. Vyama viwili vikubwa nchini Ugiriki vimeweka tarehe 19 Februari mwaka ujao kuwa ni siku muafaka kwa uchaguzi ambao ulitakiwa na upinzani kama sharti la kuukubali mpango wa Ulaya wa kuikopesha ugiriki Euro bilioni 130, kuepusha uwezekano wa kuangamia kwa uchumi wa nchi hiyo.

Ingawa baadhi ya wagiriki wameyapokea kwa mashaka maafikiano ya jana usiku, kuna wale ambao wanasema nchi yao ilihitaji kuongea kwa sauti moja.

"Kama watafikia makubaliano, hiyo itakuwa ni hatua nzuri, kwa sababu taifa linafaa kukabili hali hii kwa msimamo mmoja."

Jana Umoja wa Ulaya ulikuwa umueishinikiza Ugiriki kutoa jibu la haraka juu ya namna itakavyotumia mkopo huo wa dharura kusaidia uchumi wake. Mawaziri wa fedha wa nchi zinazotumia sarafu ya Euro watakutana kuamua kama wataipa Ugiriki sehemu ya kwanza ya mkopo huo, kiasi cha Euro bilioni kumi na moja, ambayo serikali ya nchi hiyo yenye matatizo inasema inahitaji kablaya tarehe 15 Desemba kuweza kuendesha mambo yake.

Kabla ya mkutano huo utakaofanyika Brussels, magwiji wa masuala ya uchumi wa Ugiriki kutoka upande wa serikali na ule wa upinzani nao watakutana kutathmini hali ya mambo.

Malumbano ya kisiasa ambayo yameitikisa Ugiriki katika siku chache zilizopita yaliwakasirisha viongozi wa Ulaya, ambao kwa maoni yao uliibika kwa wakati usiofaa, huku kanda nzima ya Euro ikihangaishwa na mgogoro wa madeni, na mkopo kwa nchi hiyo hiyo ya Ugiriki ukiwa miongoni mwa masuala tete.

Miongoni mwa watu wanaodokezwa kuweza kuchaguliwa kuwa waziri mkuu mpya ni waziri wa fedha Evangelos Venizelos, na Lucas Papademos ambaye aliwahi kuwa makamu rais wa Benki kuu ya Ulaya.

Kufikiwa kwa muafaka nchini Ugiriki hakuitaepusha nchi hiyo na shinikizo kutoka Ulaya, kuitaka nchi hiyo kuchukua hatua zaidi za kukaza mkwiji kama sharti la kupokea mkopo ulioahidiwa. Serikali itakayoundwa itatwishwa jukumu la kusimamia hatua hizo.

Mzozo wa kisiasa ulizuka nchini Ugiriki wiki iliyopita, baada ya waziri mkuu anaeondoka madarakani, George Papandreou, kutangaza kuwa angeitisha kura ya maoni kuamua juu ya mkopo huo mkubwa wa kuukwamua uchumi wa nchi, ambao lakini unaandamana na masharti makali ya kubana matumizi.

Mwandishi: Daniel Gakuba/AFP

Mhariri: Miraji Othman