1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

May kuanzisha rasmi mchakato wa BREXIT

Lilian Mtono
29 Machi 2017

Waziri mkuu wa Uingereza Theresa May leo hii anatarajia kuwasilisha rasmi nyaraka za Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya, na  kuanzisha mchakato wa makubaliano yasiyojulikana hatima yake

https://p.dw.com/p/2aD9V
Großbritannien Theresa May Downing Street in London
Picha: Reuters/R. Pohle

Makubaliano hayo, ambayo yatadumu miaka kadhaa yataonekana kuwa mtihani kwa uvumilivu wa Umoja wa Ulaya.

Ikiwa ni miezi tisa baada ya Uingereza kupiga kura ya kujiondoa Umoja wa Ulaya, Waziri Mkuu May atamuandikia Rais wa baraza la Umoja huo, Donald Tusk barua ya kuthibitisha kuwa Uingereza iliyojiunga tangu mwaka 1973, hatimaye inajitoa kwenye umoja huo.

Jana jioni picha zilimuonyesha May akisaini barua hiyo kuhusu kifungu cha 50 cha mkataba wa Lisbon na kuuarifu rasmi Umoja wa Ulaya kuhusu hata hiyo ya Uingereza kujitoa.

Waziri Mkuu May, ambaye awali alipinga mpango huo wa BREXIT, na kuchaguliwa kushika wadhifa huo wakati kukiwa na msukosuko mzito wa kisiasa kufuatia kura ya maoni, atakuwa na miaka miwili ya kukamilisha mkakati huo wa talaka kabla ya kuanza utekelezwaji wake mwishoni mwa mwezi Machi mwaka 2019.

"Kwa kuwa hivi sasa maamuzi yamefikiwa ya kuondoka Umoja wa Ulaya, ni wakati wa kuungana pamoja” May aliwaambia wabunge, ikiwa ni maoni yaliyosambazwa na ofisi yake.

Siku moja kabla ya BREXIT, May anakabiliwa na jukumu zito zaidi, miongoni mwa mawaziri wakuu wa hivi karibuni, la kuwaunganisha pamoja Waingereza wakati ambapo kuna kitisho cha kuanza upya kwa madai ya Scotland ya kupewa uhuru wake, wakati ikiwa inaendelea mazunguzmo magumu na nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya kuhusiana na masuala ya fedha, biashara, usalama na masuala mengine tata.

Matokeo ya mazunguzmo hayo yataonyesha mustakabali wa Uingereza, yenye uchumi unaofikia Dola Trilioni 2.6, na nchi ya tano kwa ustawi wa uchumi duniani, na kuangazia iwapo Uingereza inaweza kusalia katika nafasi hiyo, ya kuwa mmoja ya mataifa mawili yenye nguvu zaidi kifedha duniani.

Schottland | Parlament stimmt für neues Unabhängigkeitsreferendum
Waziri Kiongozi wa Scotland(Kulia pichani) Nicola Sturgeon, akiwasili bungeni akiwa na naibu wake John SwinneyPicha: Getty Images/J. J. Mitchell

Kwa upande wa Umoja wa Ulaya, ambayo tayari inayumba kutokana na kukabiliwa na migogoro mfululizo ya madeni na wakimbizi, kuondoka kwa Uingereza ni pigo kubwa kutokea katika kwa juhudi za kipindi cha miaka 60 za hatua madhubuti za kuweka mshikamano Barani Ulaya baada ya kuathirika pakubwa na vita mbili kuu za dunia.

Viongozi wake wanasema hawatataka kuiadhibu Uingereza. Lakini kutokana na utaifa, kuibuka kwa vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya miongoni mwa jumuiya, hawataweza kuipa Uingereza masharti rahisi ambayo yanaweza kuyahamasisha mataifa mengine wanachama kufuata mfano huo na kujiengua.

Katika hatua nyingine, Bunge la Scotland limeunga mkono mwito wa waziri kiongozi wa nchi hiyo Nicola Sturgeon ya kuwa na awamu ya pili ya kupiga kura ya maoni ya kujitenga na Uingereza. Wabunge 69 dhidi ya 59 walipiga kura za kumpa jukumu Sturgeon kuomba idhini kwa Uingereza ya kura hiyo kupigwa kati ya Septemba 2018 na machi 2019.

Uingereza ilipiga kura ya maoni ya BREXIT mnamo mwezi Juni mwaka jana baada ya kampeni zilizoligawa taifa hilo. Scotland na Ireland ya Kaskazini kwa wingi wao walipiga kura ya kusalia ndani ya Umoja huo, wakati England na Wales wakiungwa mkono na idadi kubwa ya raia wakipigia kura ya kuondoka.

Mwandishi: Lilian Mtono.

Mhariri: Gakuba Daniel