Mawaziri wa Fedha wa G20 wanakutana Korea ya Kusini kujadili mikakati ya kuleta ustawi na kuepusha migogoro. | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.06.2010
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mawaziri wa Fedha wa G20 wanakutana Korea ya Kusini kujadili mikakati ya kuleta ustawi na kuepusha migogoro.

Mawaziri wa fedha wa nchi za G20 wanajadili njia za keupusha migogoro ya uchumi na ya mabenki.

default

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble na mwenzake wa Marekani,Timothy Geithner.

Mawaziri wa fedha kutoka nchi za G 20 wanaokutana katika mji wa Busan, Korea yaKusini wanatarajiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na nchi za ukanda wa sarafu ya Euro katika kukabiliana na mgogoro wa madeni. Lakini mawaziri hao bado wanatofautiana juu ya kodi ya mabenki.

Mawaziri hao wametoa kauli ya uwazi kuonyesha wasiwasi juu ya matatizo yaliyopo katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro.Wamesema wazi kabisa kwamba migogoro ya madeni na ya mabenki katika nchi za ukanda wa Euro inaweza kuuteteresha mkondo wa kurejea hali nzuri ya uchumi wa dunia.

Waziri wa fedha wa Canada Jim Flaherty amesema suala la matatizo ya madeni ya Ugiriki na nchi nyingine za ukanda wa Euro zenye madeni makubwa ,ndilo linalopewa kipaumbele kwenye mkutano wa mawaziri hao kutoka nchi tajiri na zinazoinukia kiuchumi.

Waziri Flaherty amezitaka nchi za Ulaya ziutatue mgogoro wa mabenki ili kuweza kudumisha ustawi wa uchumi.Amesema nchi za Ulaya zinazokabiliwa na madeni zinapaswa kufanya juhudi za kurekebisha bajeti zao.

Naye waziri wa mipango wa Afrika Kusini Trevor Manuel ametoa mwito wa kupitishwa maamuzi juu ya kuepusha hatari ya kudorora tena kwa uchumi. Waziri huyo ametahadharisha kwamba hali ya kuanza kustawi tena kwa uchumi bado ni dhaifu.

Lakini akizungumza kwenye mkutano huo waziri wa fedha wa Marekani Timothy Geithner amesema pana matumaini juu ya uchumi wa dunia na kwamba inawezekana kuondokana na hali ya sasa. Waziri Geithner pia amesisitiza juu ya umuhimu wa kuwapo taratibu za pamoja za kuzuia nyendo kama zile zilizosababisha mgogoro mkubwa wa mabenki miaka 2 iliyopita.

Hata hivyo mawaziri wa fedha wa nchi za G 20 wanaokutana katika mji wa Busan Korea ya Kusini, bado wanatofautiana juu ya kuyatoza mabenki malipo yanayoweza kutumiwa endapo mabenki yanafilisika badala ya kuwabebesha walipa kodi mzigo wa kuyaokoa mabenki hayo. Mawaziri wa fedha wa nchi za G20 wanakutana katika mji wa Busan huku kukiwa na ulinzi mkali kutokana na kuongozeka kwa mvutano baina ya Korea ya Kusini na ya Kaskazini.

Mawaziri hao wanatayarisha mkutano wa kilele wa marais na mawaziri wakuu wa nchi za G20 utakaofanyika mwishoni mwa mwezi huu Toronto Canada.

Mwandishi: Mtullya Abdu/ RTRE/AFPE/ZAR

Mhariri/Josephat Charo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com