Mawakili wahofia huenda Paul Rusesabagina akateswa Rwanda | Matukio ya Afrika | DW | 08.09.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mawakili wahofia huenda Paul Rusesabagina akateswa Rwanda

Kundi la wanasheria wa Paul Rusesabagina limewasilisha malalamishi kwa Umoja wa Mataifa likisema Rusesabagina anakabiliwa na hatari ya kutendewa ukatili.

Kulingana na wanasheria hao, Rusesabagina anakabiliwa na "hatari ya haraka" ya kutendewa ukatili wakati anaendelea kutengwa na mawakili, maafisa wa ubalozi na familia yake zaidi ya wiki moja ya kuonekana akiwa amefungwa pingu nchini Rwanda.

Malalamishi hayo yaliyowasilishwa siku ya Jumatatu na Nils Melzer yanataka kufanyika kwa uchunguzi wa mara moja kuhakikisha kuwa Rusesabagina ambaye ni mkosoaji wa wazi wa muda mrefu wa serikali ya Rwanda ‘'bado yuko hai.''

Siku ya Jumapili rais wa Rwanda Paul Kagame aliashiria kuwa huenda Rusesabagina alidanganywa kupanda ndege kuelekea katika taifa hilo ambalo hajaishi tangu mwaka 1996. Akizungumza kupitia televisheni ya kitaifa, Kagame aliongeza kuwa hatua hiyo haikukumbwa na kasoro hii ikimaanisha kuwa Rusesabagina alijileta mwenyewe nchini humo hata kama hakunuia kufanya hivyo.

Rais huyo hata hivyo hakusema jinsi Rusesabagina alivyochukuliwa kutoka Dubai alipozungumza mara ya mwisho na familia yake nchini Rwanda.

Familia ya Resesabagina wa umri wa miaka 66 ambaye sasa ni raia wa Ubelgiji na mwenye makao ya kudumu nchini Uingereza, imesema kuwa hangeweza kupanda ndege kuelekea Rwanda kwa ufahamu wake mwenyewe na kwamba "ametekwa nyara.”

Rwanda inamtuhumu Rusesabagina kwa kuongoza kundi la wanamgambo ambalo limesababisha vifo vya raia wengi wa nchi hiyo.

Serikali hiyo imetaja video iliyosambazwa katika mtandao mwishoni mwa mwaka 2018 ambapo alielezea kuunga mkono kundi la kujihami la mtandao wake wa upinzani wa kisiasa na kusema wakati umewadia kwao kutumia njia yoyote ya kuleta mabadiliko nchini Rwanda kwa kuwa njia zote za kisiasa zimejaribiwa na kushindwa.

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Rais wa Rwanda Paul Kagame

Katika siku zilizopita, Rusesabagina alikanusha madai ya kufadhili waasi nchini Rwanda na kusema analengwa kwa kuikosoa serikali ya rais Kagame kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kuzuiliwa kwa Rusesabagina kumeibua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kwamba huu ni mfano wa hivi karibuni wa serikali ya Rwanda kuwalenga wakosoaji wake nje ya mpaka wake.

Rusesabagina aliibuka kuwa maarufu kwa kuwalinda zaidi za watu elfu moja alipokuwa meneja wa hoteli wakati wa mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 nchini Rwanda ambapo watu laki nane wa jamii ya Watutsi na wengine kutoka jamii ya Wahutu waliuawa. Kutokana na juhudi zake, alitunukiwa tuzo la rais la uhuru la Marekani mnamo mwaka 2005.

Wikendi iliyopita, wakili mmoja wa Rwanda alisema kuwa anamuwakilisha Rusesabagina. Malalamishi ya kundi hilo la wanasheria yamepinga hatua hiyo na kusema inaonekana wakili huyo aliteuliwa bila ya idhini ya Rusesabagina na kwamba haiwezekani kwa Rusesabagina kufanya mahojiano na kuajiri kwa hiari wakili bila ya kushauriana na familia yake kwanza.

Bado haiko wazi ni wakati gani Rusesabagina atakapofikishwa mahakamani. Sheria ya Rwanda inasema kuwa mshukiwa nchini humo anaweza kuwa kizuizini kwa muda wa siku 15 na muda kuongezwa tena hadi siku 90.