1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaaziri wa kiarabu wakutana Cairo

Oummilkheir23 Novemba 2007
https://p.dw.com/p/CSGs
Flaggen-Montage: DW / SteinmetzPicha: DW

Viongozi wa Misri,Jordan na Palastina wamesema „wana matumaini mema“ kuelekea mkutano wa jumanne ijayo huko Annapolis Marekani,mkutano uliolengwa kuufufua utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina.

Rais Hosni Mubarak wa Misri aliwakaribisha kwanza rais mwenzake wa Palastina Mahmoud Abbas,na mfalme Abdallah wa pili wa Jordan katika kituo cha mapumziko cha Sharm el Sheikh,katika bahari ya Sham,kabla ya kukutana baadae jana usiku na mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi za kiarabu mjini Cairo.

Nchi kadhaa za kiarabu,mfano Saud Arabia,zinajiuliza kama zishiriki au la katika mkutano wa Annapolis,viongozi wakihofia mkutano huo usije ukamalizika bila ya lolote muhimu kufikiwa.

Viongozi wa Misri,Jordan na Palastina wamesema “wana matumaini mema”-mkutano wa Annapolis unaweza kutuliza “kiu cha wapalastina na ulimwengu wa kiarabu pamoja pia na wale wote wanaofuatilizia kwa karibu sana suala la wapalastina na utaratibu wa amani kwa jumla”

“Risala ya mwaliko wa mkutano huo inazungumzia amani na juhudi za waarabu pamoja pia na mpango wa kubadilishana ardhi kwaajili ya amani” amesema hayo msemaji wa rais Hosni Mubarak Suleiman Awadh.

Lakini hitilafu za kina za maoni kati ya wapalastina na waisrael kuhusiana na masuala tete-mfano kanuni za Jerusalem ya Mashariki,mipaka ya taifa la siku za mbele la Palastina,kanuni za wakimbizi wa kipalastina na hatima ya makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi zinatishia kukorofisha mkutano huo wa Annapolis.

Marekani inazungumzia hivi sasa juu ya kile kitakachofuatia baada ya Annapolis.Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice anahisi pekee kuitishwa mkutano kati ya waisrael na wapalastina ni ufanisi.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuia ya nchi za kiarabu wanakutana tangu jana mjini Cairo na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas alijiunga nao pia hivi punde.

Mada kuu ni kama nchi za kiarabu zisihiriki Annapolis au la.

Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa jumuia ya nchi za kiaragu wameitumia risala ya dharura Marekani ijumuishe suala la milima ya Golan katika ajenda ya mazungumzo.Syria inafungamanisha suala hilo na kushiriki kwake mazungumzoni.

Oman ni nchi ya kwanza ya kifalme katika Ghuba kutangaza rasmi itashiriki katika mkutano wa Annapolis.

Mkutano wa mawaziri wa jumuia ya nchi za kiarabu unahudhuriwa pia na wanachama 13 wa kamati inayosimamia juhudi za amani za nchi za kiarabu zilizofufuliwa upya na Saud Arabia March mwaka huu mjini Ryadh.Juhudi hizo zinazungumzia juu ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya nchi za kiarabu na Israel ikiwa Israel itayahama maeneo ya waarabu yaliyotekwa tangu mwaka 1967,ikiwa taifa la Palastina litaundwa na Jerusalem Mashariki kua mji mkuu wake na kufikiwa “ufumbuzi wa haki na unaokubalika wa suala la wakimbizi wa Palastina.