Matumizi ya baiskeli Afrika
Kuni, maji, mboga, wanyama - Waafrika wanatumia baiskeli kusafirisha vitu vingi. Watu wengi hawawezi kujinunulia gari na kwa kutumia ubunifu kidogo tu, baiskeli inaweza kutumiwa kusafirishia kila aina ya mzigo
Mzigo wa kilo 300
Hakuna jambo lisilowezekana - labda hayo yalikuwa mawazo ya bwana huyu kutoka Msumbiji. Amepakia magunia sita ya mkaa kwenye baiskeli yake. Mzigo huo una uzito wa karibu kilo 300. Hapo hakuna tena kuendesha, kinachobaki ni kuisukuma baiskeli. Amefunga kamba kwenye usukani ili aweze kuiongoza baiskeli yake vizuri.
Nishati juu ya magurudumu mawili
Mkaa husafirishwa hadi umbali wa kilomita 100 kwa baiskeli na kupelekwa Beira, mji wa pili kwa ukubwa Msumbiji. Katika maeneo ya vijijini barabara nyingi ni mbovu kwa hiyo wakati mwingine ni rahisi zaidi kusafiri kwa baiskeli kuliko kwa gari. Wakaazi wengi wanawategemea wauza mkaa kwa sababu hawana uwezo wa kununua umeme au gesi.
Msaada unapopata pancha
Nguo inapochanika inapelekwa kwa fundi, kiatu kinapoharibika pia kinapelekwa kwa fundi. Mafundi daima wanajua namna ya kusaidia na hata gurudumu linapopata pancha wakati mwingi kuna fundi karibu anayeweza kusaidia. Mara nyingi mafundi wanapatikana kando ya barabara na hivyo wanaweza kutoa msaada wa haraka.
Hakuna kipato bila baiskeli
Mara nyingi watu wanahitaji muda wa masaa mengi kwenda shuleni au kwenda kuchota maji, kutafuta kuni au chakula. Katika maeneo mengi hakuna usafiri wa umma, magari yanauzwa kwa bei kubwa sana. Hivyo wakati mwingine watu wanashindwa kusafirisha bidhaa zao. Lakini mkulima huyu amepata suluhisho. Anaweza kupeleka bidhaa zake sokoni kwa kutumia baiskeli.
Bidhaa za dukani
Mtu anayemiliki duka bila kuwa na gari la kusafirishia mizigo lazima atafute mbinu ya kubeba bidhaa mpya kwa ajili ya duka lake. Nchini Tanzania bidhaa hizo hutolewa mijini na kupelekwa sehemu za ndani kabisa vijijini. Waafrika wengi wanapenda kunywa coca cola hivyo muuzaji anayeweza kubeba masanduku mengi ya kinywaji hicho atafaidika.
Biashara ya kuuza kwenye baiskeli
Baiskeli zinatumika pia kama aina ya maduka. Muuzaji huyu kutoka Tanzania ana viatu, mabegi na bakuli za plastiki. Afrika kuna "wamachinga" wengi, yaani wauzaji wa barabarani. Wengi wao hawajasajiliwa rasmi na ndio maana mara kwa mara wanapata matatizo na polisi.
Safari ya kuku
Usukani wa baiskeli unaweza kubeba kuku wangapi? Muuzaji huyu kutoka Nigeria anataka kujua jibu la swali hilo. Wakati mwingine anauza baadhi ya kuku wake njiani. Lakini nia yake ni kuwapeleka sokoni ambapo watu huuza bidhaa freshi. Ndiyo maana kuku hawa hawajachinjwa.
Mee, mee
Mbuzi hawa wamebananishwa kweli! Mmiliki wao anawapeleka katika soko moja la mjini Bauchi, Nigeria, kuwauza. Bei ya mbuzi mmoja ni kama Naira 7000 hivi, sawa na Euro 35. Bila shaka wakishanunuliwa watakwenda kuchinjwa.
Safari na familia Malawi
Katika nchi nyingi za Kiafrika baiskeli hutumiwa kama teksi. Kiti cha nyuma cha kubebea mizigo hutengenezwa vizuri ili abiria aweze kukaa. Baskeli hizo zina majina tofauti. Tanzania, Kenya na Uganda zinaitwa "boda boda", jina linalotokana na maneno ya kiingereza "border to border" - mpaka hadi mpaka. Hii ni kwa sababu katika miaka ya 1960 zilitumika zaidi kwenye maeneo ya mipakani.
Leseni ya kuendesha baiskeli
Utawala wa mji wa Quelimane, uliopo kaskazini mwa Msumbiji, unajaribu kupunguza idadi ya waendesha teksi za baiskeli. Mwanzoni mwa mwaka 2010 ulianzisha leseni kwa waendesha baiskeli iliyogharimu metical 350, sawa na Euro 12. Lakini waendesha teksi za baiskeli waliandamana kupinga leseni hiyo. Utawala wa mji ulikubali na mpaka leo bado haujaweka sheria wa kutaka waendesha baiskeli wawe na leseni.
Raha tupu
Mbali na kutumika kama njia ya usafiri, baiskeli hutumika pia katika michezo. Ndiyo maana hata baiskeli za kisasa aina ya "mountain bike" zinauzwa pamoja na zile za kawaida. Kijana huyu wa visiwa vya Shelisheli anaendesha baskeli, si kwa ajili ya kutafuta kipato ila kwa ajili ya kujifurahisha tu.