1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Afrika

Matokeo ya uchaguzi wa Bunge Misri kutolewa leo

Matokeo ya uchaguzi wa bunge uliofanyika nchini Misri Jumatatu wiki hii yanatazamiwa kutolewa leo, huku vyama vya kiislam vikisadikika kupata ushindi mkubwa.

Wamisri wakifurahia kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza huru.

Wamisri wakifurahia kupiga kura katika uchaguzi wa kwanza huru.

Katika uchaguzi huu ambao ni wa kwanza huru kufanyika nchini Misri tangu kuangushwa kwa utawala wa kifalme mwaka 1952, wapiga kura wanaelekea kuvipa nafasi vyama vya kiislamu. Akizungumza baada ya kupiga kura yake, raia mmoja nchini humo Ramadhan Abdel Fattah alisema, ''Tumejaribu kila njia, kwa nini wakati huu tusiupe nafasi uislamu?''

Sura kamili ya bunge la Misri itafahamika baada ya kukamilika kwa zoezi zima la uchaguzi mwezi Januari mwakani, na baada ya hapo, bunge hilo litakuwa katika nafasi ya kuliwekea changamoto baraza la kijeshi ambalo linatawala nchi hiyo tangu kuondolewa kwa utawala wa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari mwaka huu.

Mohammed Morsi kiongozi wa Udugu wa Kiislamu ambao unatarajiwa kupata ushindi katika uchaguzi huu

Mohammed Morsi kiongozi wa Udugu wa Kiislamu ambao unatarajiwa kupata ushindi katika uchaguzi huu

Ulimwengu unafuatilia kwa makini uchaguzi huu, kwa sababu utengamano wa Misri ni muhimu kwa dunia. Nchi hiyo imesaini mkataba wa amani na Israel, na inamiliki mfereji wa Suez ambao ni kiungo kati ya Ulaya na Asia. Wakati wa utawala wa Hosni Mubarak wa zaidi ya miaka 30, Misri ilikuwa pia mshirika mkuu wa nchi za magharibi.

Marekani na washirika wake wa Ulaya wanajikuta njia panda kuhusiana na hali ya mambo nchini Misri. Ingawa nchi hizo zinalihimiza baraza la kijeshi kuharakisha mchakato wa kukabidhi madaraka kwa viongozi wa kiraia, wana wasiwasi kuwa utawala wa kiislamu unaweza kukandamiza uhuru wa watu na kuhatarisha mkataba wa amani na Israel.

Udugu wa Kiislamu unasema chama chake kipya cha Uhuru na Haki (Freedom and Justice Party) kitashinda angalau asilimia 40 ya viti bungeni. Chama kingine cha wahafidhina wa kisalifisti kinategemea kujipatia asilimia 20 ya viti katika bunge hilo.

Kuna uwezekano wa vyama hivyo viwili vya kiislamu kuunda mseto katika bunge ingawa Udugu wa Kiislam haujatangaza nia ya kufanya hivyo. Baadhi ya wamisri wanahofia kuwa huenda utawala wa kiislamu ukaweka sheria kali za kidini, ambazo zinaweza kukwamisha sekta ya utalii ambayo ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi yao.

Baadhi wana hofu huenda Udugu wa Kiislamu ukabana uhuru wa watu

Baadhi wana hofu huenda Udugu wa Kiislamu ukabana uhuru wa watu

Katika juhudi za kuondoa hofu hizo, Udugu wa Kiislamu umetoa tamko ukisema lengo lao kubwa ni kumaliza ubadhirifu na kufufua uchumi, si kupiga marufuku pombe na kuwalazimisha wanawake kuvaa hijabu.

Wakati huo huo, waandamanaji bado hawajalegeza msimamo wao kuwataka majenerali wa baraza tawala la kijeshi kukabidhi haraka madaraka kwa serikali ya kiraia. Leo hii (Ijumaa) wamepanga kufanya maandamano mabwa kote nchini, wakidai madaraka yakabidhiwe kwa serikali ya kitaifa.

Mwandishi: Daniel Gakuba/RTRE/DPA
Mhariri:Josephat Charo