1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa yanayoinukia kiuchumi, BRICS yakutana Afrika Kusini

25 Julai 2018

Viongozi wa mataifa yanayoinukia kiuchumi - BRICS Brazil, Urusi, India; China na Afrika Kusini wanakutana Jumatano huko Johannesburg Afrika Kusini kwa mkutano wa kilele wa siku tatu.

https://p.dw.com/p/3238r
China Xiamen BRICS-Treffen Narendra Modi und Xi Jinping
Picha: Imago/Kyodo News

Lengo la mkutano huo ni  kujadili vita vya kibiashara vinavyoongozwa na Marekani. Msimamo mkali wa Rais wa Marekani Donald Trump umetilia mkazo vita vya kibiashara baada ya kuziwekea ushuru bidhaa za mabilioni ya dola kutoka China na bidhaa zengine za kimataifa.

Rais wa China Xi Jinping, Rais wa Urusi Vladimir Putin, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi na Rais wa Brazil Michel Temer wanahudhuria mkutano huo wa kilele wa kila mwaka pamoja na viongozi kadhaa wa Afrika walioalikwa kama wageni. Xi alifanya mazungumzo na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa hapo Jumanne akisema mkutano huo wa Johannesburg una umuhimu mkubwa kwa ushirikiano wa BRICS.

Shirika la Fedha Duniani IMF limeonya kuhusu vita hivyo vya kibiashara

Mapema mwezi huu China na Marekani wote waliwekeana ushuru katika bidhaa zenye thamani ya jumla ya bilioni 34 katika hatua ya kulipiziana kisasi. Tangu wakati huo Marekani imetangaza mpango wa kuwekea ushuru bidhaa zaidi za China zenye thamani ya Dola bilioni 200. China imesema ushuru huo wa Marekani ni "unyanyasaji" na mwanzo wa "vita vikubwa zaidi vya kibiashara katika historia".

Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa akiwa bungeni
Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa atahudhuria mkutano huo wa kilelePicha: Getty Images/AFP/R. Bosch

Lakini Shirika la Fedha Duniani IMF limeonya kwamba vita hivyo vya kibiashara baina ya Marekani, China na hata Umoja wa Ulaya huenda vikawa na athari katika uchumi wa dunia.

Kundi la nchi za BRICS linalojumuisha zaidi ya asilimia arubaini ya idadi ya watu duniani, linawakilisha baadhi ya nchi  zinazoinukia kiuchumi lakini limeshindwa kupata sauti moja na nchi hizo zimekuwa na viwango tofauti katika ukuaji wa chumi zao.

Lakini wachambuzi wanasema sera ya biashara ya Marekani inaweza kuwapa umoja mpya. Sreeram Chaulia ni mchambuzi wa masuala ya biashara kutoka Chuo cha Kimataifa cha Jindal huko New Delhi na ameliambia shirika la habari la AFP kwamba viongozi hao watakubaliana kwamba Marekani imeanzisha vita vya kibiashara ambavyo vinamuumiza kila mwanachama wao.

Reccep Tayyip Erdon atakutana na Vladimir Putin

Wachambuzi kutoka Afrika nao wanahisi  mkutano huo utaliletea manufaa bara hilo. Cobus van Staden ni mtafiti katika Taasisi ya Masuala ya Kimataifa ya Afrika Kusini.

Putin akiwa katika mkutano wa BRICS
Rais wa Urusi Vladimir Putin atakutana na Reccep Erdogan wa Uturuki siku ya mwishoPicha: picture-alliance/dpa/TASS/M.l Metzel

"Nafikiri kuna umuhimu wa mkutano wa BRICS kwa Afrika kwasababu inaleta mbadala wa maendeleo ya Afrika," alisema van Staden. "Ni hatua nzuri na yenye maoni. Nafikiri ina uwezo wa kusaidia sana katika sehemu tofauti za dunia," aliongeza Mtafiti huyo.

Mkutano huo wa kilele unafunguliwa mchana wa Jumatano kwa mkutano mkuu wa biashara kabla marais hao kufanya mazungumzo Alhamis. Viongozi wa Afrika Paul Kagame wa Rwanda, Joao Lourenco wa Angola, Macky Sall wa Senegal na Yoweri Museveni wa Uganda watahudhuria mpango wa BRICS wa mataifa yasiyo katika kundi hilo siku ya Ijumaa.

Kiongozi wa Uturuki Reccep Tayyip Erdogan pia atahudhuria kama mwenyekiti wa jumuiya ya Ushirikiano wa nchi za Kiislamu OIC na atakutana na Rais Putin wa Urusi mwishoni mwa Mkutano huo wa Kilele.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/DPAE

Mhariri: Yusuf Saumu