1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Mastadi wa dimba wamtukuza Mandela

Mastadi wa kabumbu duniani wakiongozwa na Pele wamekusanyika Cape Town kuadhimisha miaka 89 tangu kuzaliwa Nelson Mandela.

Mabingwa wa dunia na wa Copa America-Brazil jana walirudi kileleni mwa orodha ya timu bora za dimba duniani.Mganda amchoma kisu nduguye na kumuua kwa kuwa tu amezima TV wakati wa finali ya majuzi ya Copa America kati ya Brazil na Argentina.

Katika Kombe la Asia,Saudi Arabia yailaza Bahrein mabao 4-0 na kukata tiketi yake ya robo-finali.Na wakati mzee Fudel Castro wa Cuba,asahau kula dawa kwa kuangalia michezo ya -Pan AMERICAN Games inayoendelea huko Brazil,mzee Nelson Mandela, aadhimishwa na mastadi wa dimba akina Pele,Beckham na Sumuel Eto’o huko Cape Town.

Punde tu kutawazwa kwa mara ya pili mfululizo mabingwa wa Copa America kwa kuibwaga Argentina mabao 3:0 huko Venezuela juzi jumapili,FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni limeitawaza Brazil kitini kama timu bora kabisa ya dimba duniani wakati huu.

Brazil imechupa kutoka nafasi ya 3 ya ngazi ya timu bora na kuparamia hadi nafasi ya kwanza.Makamo-bingwa wa Copa America Argentina wamechupa nao kutoka nafasi ya 4 hadi ya pili na hivyo kubadilishana nafasi na m akamo-bingwa wa dunia-Ufaransa.Ujerumani,Holland,Croatia ,Ureno,Spain na Mexico zimeangukia katika kundi la timu 10 bora kabisa duniani.Kwani, mexico iliothubutu kuilaza Brazil katika Copa America, imechupa kutoka nafasi ya 26 hadi ya 10.

Ujerumani iko nafasi ya 4 nyuma ya mabingwa wa dunia-itali.

FIFA imegeuza kipimo chake cha timu na kuachana na jinsi timu zilivyocheza katika kombe lililopita la dunia mwaka uliopita na kuelekea mechi za kuania tiketi za kombe la ulaya 2008 mwakani.

Hii imepelekea kwa timu 2 za Afrika-Ghana na Ivory Coast, kuangukia nafasi ya 31 na 37.Katika Kombe la bara la asia, Saudi Arabia imekta jana tiketi yake ya robo-finali baada ya kuitimua Bahrein kwa mabao 4:0.Korea ya kusini nayo inaifuata Saudia kufuatia ushindi wa bao 1:0 dhidi ya Indonesia.

Finali ya jumapili iliopita ya Copa America kati ya Brazil na Argentina imetoa mhanga maisha ya shabiki mmoja nchini Uganda:Kwani polisi nchini Uganda imemtia nguvuni Sam Naluswa kwa tuhuma za kumpiga kisu na kumuua nduguye Moses Kyegombe.Kisa nini ?

Kwa muujibu wa shahidi aliejionea mkasa huo,Kyegombe –shabiki mkubwa wa Argentina alizima Rundinga au TV baada ya timu yake kuzabwa mabao 2:0 na Brazil.Kwavile hayo yalikua matokeo ya kipindi cha kwanza tu na mpira ukiendelea,nduguye Naluswa-shabiki mkubwa wa Brazil, alikasirishwa na kitendo hicho cha kumaliza mpira kabla ya firimbi ya mwisho kulia.

Jaribio la baba yao kuwazuwia wasigombane halikufanikiwa.Na ,licha ya timu yake ya Brazil kuingo’a meno Argentina kwa mabao 3:0,Naluswa akitaka kulipiza kisasi chake cha kuzimiwa TV alimfuata nduguye nyumbani baada ya mpira kwisha na kumchoma kisu-zasema taarifa za shirika la AFP.Mechi za nje zina ushabiki mkubwa Afrika mashariki na wazimu wa mpira umekua hauna mpaka.

Wazimu wa dimba ulimtembelea jana mzee Nelson Mandela,mbondia wa zamani alieadhimisha jana siku kuu ya kuzaliwa akifikia umri wa miaka 89.FIFA ilimtunza jana mzee Mandela jazi maalumu kama zawadi na dimba maalumu kati ya timu ya mchanganyiko wa mastadi ya dunia na ile ya Afrika huko Cape Town.

Pele mfalme wa dimba akiwa miongoni mwa mastadi hao pamoja na Samuel Eto’o wa Kamerun na David Beckham wa Uingereza, alinukuliwa kusema:

“Nimekutana na waheshimiwa wengi maishani mwangu,lakini mzee Nelson Mandela ni wa aina ya kipekee.Nimeingiwa na hamasa kubwa na ni heshima kuongoza timu ya dunia kuadhimisha siku ya kuzaliwa mzee Mandela.”-alisema Pele.

Kiongozi wa FIFA Jack Warner,alimuarifu mzee Mandela kwamba FIFA inaweka matarajio makubwa kwa Kombe la dunia 2010 nchini Afrika kusini na kwamba litakua ndilo bora kuliko yote .

Wakati mzee Mandela akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa, mkongwe mwengine mzee Fudel Castro alifichua jana kwamba jinsi alivyoshughulika kuangalia michezo ya bara la America-Pan American Games huko Brazil,baadhi ya nyakati husahau kula dawa zake.Fidel Castro anaeugua amesema hakuna mchezo unaompita kwenye TV.

Pan American Games inaendelea wakati huu mjini Rio de Jeneiro hadi Julai 29.Cuba hadi jana ikijikuta nafasi ya pili katika orodha ya medali inayoongozwa na Marekani.August 13 ijayo,mzee Fidel castro ataadhimisha nae miaka 81 ya kuzaliwa.