1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hii inatokana na sakata mauaji ya simba, Zimbabwe

4 Agosti 2015

Mashirika ya ndege nchini Marekani yamepiga marufuku usafirishaji wa nyara katika ndege za shirika hilo, kufuatia sakata linaloendelea la mauaji ya simba maarufu aitwae Cecil nchini Zimbabwe lililotokea hivi karibuni.

https://p.dw.com/p/1G9Rf
Ndege ya shirika la Delta
Ndege ya shirika la DeltaPicha: dapd

Mapema iwezekanavyo shirika la ndege la Delta litaanza rasimi utekelezaji wa hatua ya kupiga marufuku usafirishaji wa shehena ya nyara za wanyamapori wote kama vile simba, chui, tembo, faru na nyati katika maeneo yote ndege za shirika hilo zinakosafiri duniani kote.

Hatua iliyochukuliwa na mashirika hayo pia imekwisha chukuliwa na mashirika mengine ya ndege ya Emirates na shirika la ndege la Afrika ya kusini.

Marufuku hiyo inakuja katika kipindi ambacho ni msimu wa juu wa uwindaji katika mataifa kadhaa barani Afrika na pia kilio cha dunia nzima kulaani kuuawa kwa Simba Cecil nchini Zimbabwe kulikofanywa na muwindaji Daktari wa meno wa Marekani.

Shirika la ndege la Delta limesema litapitia upya sera zake zinazohusiana na usafirishaji wa nyara zitokanazo na uwindaji kwa kushirikiana na mawakala sahihi wa serikali na mashirika mengine yanayohusika na suala hilo.

Simba huyo Cecil alikuwa kivutio cha kipee kwa watalii ambao wamekuwa wakitembelea mbuga nchini Zimbabwe ya Hwange.

Simba aliyeuawa, Cecil
Simba aliyeuawa, CecilPicha: picture-alliance/dpa/Zumaress

Mamlaka ya wanyamapori nchini Zimbabwe hivi karibuni ilimtaja mtu mwingine ambae pia ni raia wa Marekani kwa tuhuma za kumua simba mwingine nchini humo.

Taarifa ya serikali pia ilisema muandaaji wa safari za wanyamapori nchini humo pia amekamatwa kufuatia operesheni kabambe ya kupambana dhidi ya uwindaji haramu katika hifadhi ambayo simba Cecil alikuwa akiishi.

Muwindaji mmarekani Walter Palmer alimua simba Cecil kwa kutumia upinde na mshale na kulipa dola 50,000 kwa uwindaji huo.

Uwindaji wa aina hiyo katika mbuga kama hizo umepigwa marufuku isipokuwa kwa kibali maalumu kutoka mamlaka ya wanyamapori.

Mwandishi: Isaac Gamba/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef