HALI MBAYA UKANDA WA GAZA
6 Machi 2008
Mashirika yanayotetea haki za binadamu yamesema hali inayowakabili watu kwenye Ukanda wa Gaza imefikia kiwango kibaya, kisichokuwa na mithili tokea sehemu hiyo ianze kukaliwa na Israel mwaka 1967.
Mashirika hayo yameripoti kuwa watu wanaothirika kutokana na hali hiyo ni pamoja na watoto wa shule.
Madai hayo yametolewa pia na mashirika ya misaada ya Uingereza na yameutaka Umoja wa Ulaya uanze mazungumzo na viongozi wa chama cha Hamas wanaoongoza kwenye Ukanda wa Gaza.
Asasi za kutetea haki za binadamu pamoja na mashirika hayo ya misaada pia yameilaumu Israel kwa kuwawekea vikwazo wapalestina wa Ukanda wa Gaza na kuchukua hatua za kijeshi zinazochochea moto zaidi.
Katika ripoti yao mashirika hayo yamesema Israel inawaadhibu wapalestina wote wanaoishi kwenye Ukanda wa Gaza ikiwa pamoja na watoto wa shule.
Ripoti imesema hali inayowakabili wapalestina milioni moja na laki tano katika sehemu hiyo imefikia hatua mbaya isiyokuwa na mithili tokea sehemu hiyo ianze kukaliwa na Israel mwaka 1967.
Katika ripoti hiyo mashirika manane yisiyokuwa ya kiserikali yamesisitiza umuhimu wa kufanyika mazungumzo na viongozi wa Hamas waliotwaa mamlaka ya Ukanda wa Gaza mwezi juni mwaka jana ambao wanatathminiwa kuwa magaidi na Umoja wa Ulaya,Marekani na Israel.
Asasi za kimataifa zimelalamika kwamba jumuiya ya kimataifa inawatenga wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Wawakilishi wa asasi hizo wameeleza katika ripoti yao kuwa sera ya kuwatenga wapalestina haijaleta manufaa kwa yeyote Wameutaka Umoja wa Ulaya uachane na sera hiyo na uanze mazungumzo na wawakilishi wote wa wapalestina.
Maisha ya wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza yamezidi kuwa mabaya kutokana na hatua ya Israel kuwabana wapalestina hao kwa vikwazo ,ikiwa ni njia mojawapo ya kuzuia mashambulio ya roketi yanayofanywa na wapiganaji wa kipalestina dhidi ya Israel, lakini mashirika hayo yamedai katika ripoti yao kuwa hatua za Israel haziongezi usalama kwa wapalestina wala kwa waisraeli wenyewe. na kutokana na hayo mashirika hayo ya misaada yameutaka Umoja wa Ulaya utoe kauli kali kulaani hatua za Israel za kuendelea kuwabana wapalsetina wa Ukanda wa Gaza kwa vikwazo na kuwazingira watu hao.
Hali ya Ukanda wa Gaza imekuwa mbaya kiasi kwamba asilimia 80 ya watu wanategemea msaada wa chakula kutoka nje na asimilia 40 ya watu hawana ajira.
Kutokana na vikwazo spea, haziingii Ukanda wa Gaza na kutokana hali hiyo hospitali haziwezi kuendesha mashine za kuokolea maisha ya watu.
Watoto wa shule pia hawapati vitabu kutokana na vikwazo vya Israel.
Mashirika ya kimataifa yamesema ikiwa vikwazo havitaondoshwa, wapalestina wa Ukanda wa Gaza watakabiliwa na maafa makubwa zaidi.
Mashirika ya kimataifa yamesema hali imezidi kuwa mbaya kutokana na hatua za kijeshi zilizoanza kuchukuliwa mwezi februari na Israel ili kuzuia mashambulio ya roketi.
Tokea wakati huo wapalestina zaidi ya 120 wameuliwa na majeshi ya Israel ikiwa pamoja na watoto 20.