1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashindano ya Ubingwa wa riadha.

29 Julai 2010

Kenya yajinyakulia dhahabu yake ya kwanza.

https://p.dw.com/p/OXNA
Mturuki Elvan Abeylegesse asherehekea ushindi wa mbio za mita 10,000 Barcelona.Picha: AP

Wenyeji Kenya wa mashindano ya ubingwa wa riadha barani Afrika yanayoingia siku ya pili hii leo, wamejinyakulia nishani yake ya kwanza ya dhahabu hapo jana, wakati mwanariadha Wilson Kiprop,  alichukua uongozi katika mbio za mita 10,000 kwa wanaume. Huku nako Barcelona katika mashindano ya ubingwa barani Ulaya, Christophe Lemaitre wa Ufaransa, akiibuka mkimbiaji haraka zaidi Ulaya katika mbio za mita 100.

Mweka rekodi  wa taifa nchini Kenya, Wilson kiprop,  alitoa ushindi safi hapo jana wa dakika 27 sekundi 32.91, ambao Moses Kipsiro kutoka Uganda aliyemfuata nyuma, alishindwa kuuhimili, miongoni mwa wengine walioshiriki katika mbio hizo za mita 10,000.

Awali mashindano hayo ya masafa marefu yalitarajiwa kuzua upinzani mkali kati ya Kenya na Ethiopia,lakini hali ilibadilika wakati mshindani wa Ethiopia, Sileshi Sihine na Teklemariam Medhin, walipotupwa nyuma baada ya roundi 15 katika mbio hizo, huku Wakenya walioongozwa na Kiprop wakifanikiwa kuipeperusha bendara ya nchi yao juu zaidi.

Wakati huo wote, Mganda, Kipsiro ambaye  ni mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 5000 ulimwenguni, aligandamana na Wakenya hao na kufanikiwa kuibika wa pili na kupokea nishani ya fedha,mbele ya mkenya Goefrrey Mutai aliyepokea ya shaba.

Nigeria ilitawala mbio za masafa mafupi katika mbio za ufunguzi wa mashindano hayo ya 17 ya ubingwa wa riadha barani Afrika.

Agnes Osazuwa  mshindi wa nishani ya shaba katika mashindano ya olimpiki yaliofanyika Beijing mnamo mwaka 2008, aliibuka wa kwanza katika mbio za kufuzu kwa nusu fainali za mashindano ya mita 100 kwa wanawake kwa kumaliza kwa muda wa  sekundi 11.51.

Perennes Pau Milama kutoka Gabon aliibuka wapili,huku watatu na wanne wakiwa ni ,Okagbare na Osayemi wote wakifanikiwa kushiriki katika nusu fainali hizo, hii leo.

Kwa upande wa wanaume Mnigeria, Obinna Metu alimaliza katika muda wa sekundi 10.37 na kuchukua uongozi mbele ya Seoud Mustafa wa Misri aliyeibuka wa pili katika mbio hizo za mita 100.

Na moto haukuwa tofauti huko Barcelona ambapo Mfaransa Christophe Lemaitre, sasa atakumbukwa kama mkimbiaji upesi zaidi barani Ulayam baada ya ushindi aliopata katika fainali za mbio za mita hizo 100 hapo jana.

Lemaitre aliongeza kasi baada ya kuanza vibaya  na kushinda katika muda wa sekundi 10.11.

Zilikuwa ni mbio zilizo washangaza wengi, maana wanariadha wanne waliomfuata nyuma Lemaitre kwa uchache wa sekundi, walionekana kumaliza kwa muda mmoja.

Ilibidi kusubiri ukaguzi wa kanda za video zilizowanasa wanariadha hao, kuangaliwa kwa makini, na hatimai kutuzwa Muingereza Mark Lewis Francis wa pili, huku Mfaransa Martial Mbandjock, akitajwa mshindi wa tatu.

Kinyume na hicho,Mturuki Elvan Abeylegesse, alifurahia ushindi wake wa mbio za mita 10,000 kwa wanawake alipowawacha wapinzani wake nyuma kwa tofauti ya sekundi 12 nzima.

Mwandishi: Maryam Abdalla/RTRE/AFPE

Mhariri:Josephat Charo