Mashambulizi yazidi nchini Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 12.06.2012
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashambulizi yazidi nchini Syria

Vikosi vya serikali ya Syria vimeushambulia kwa mizinga mji wa Haffa katika jimbo la kaskazini magharibi la Latakia kwa siku ya nane mfululizo kwa kile kinachoelezwa kama maandalizi ya kuuvamia mji huo.

Mmoja wa majeruhi wa mashambulizi ya Haffa.

Mmoja wa majeruhi wa mashambulizi ya Haffa.

Shirika la Uangalizi wa Haki za Binaadamu nchini Syria limesema majeshi pia yameshambulia kwa mizinga kitongoji cha mji wa mashariki wa Deir Ezzor leo hii na kuuwa watu 10, akiwemo msichana mmoja wakati wananchi wengine watano wameuwawa katika mashambulizi katikati ya mji wa Homs.

Rami Abdel Rahman wa shirika hilo la haki za binaadamu ameliambia shirika la habari la AFP kwamba vikosi vya serikali vimekuwa vikituma wanajeshi zaidi na vinajiandaa kuuvamia mji huo ambapo kuna mamia ya wapiganaji waasi wa Jeshi Huru la Syria.

Kwa mujibu wa shirika hilo lenye makao yake makuu nchini Uingereza, vikosi hivyo vya serikali vimekuwa vikitumia silaha nzito za mizinga na helikopta za kivita katika kuushambulia mji wa Al-Haffe.

Mpatanishi wa kimataifa, Kofi Annan.

Mpatanishi wa kimataifa, Kofi Annan.

Jana wanaharakati wamesema wanahofia kutatokea mauaji makubwa iwapo vikosi hivyo vitaweza kuingia katika mji huo wenye upinzani dhidi ya serikali.

Mji wa Al-Haffe unaonekana kuwa wa mkakati kutokana na ukaribu wake na mji alikozaliwa Assad wa Qardaha. Vikosi vya serikali pia vimezidisha mashambulizi leo hii kwa mji wa kati wa Holms na viunga vyake kwa kuyasakama maeneo ya upinzani ambapo hali imeelezwa kuwa ya kutisha na ya maafa.

Inasemekana kwamba raia 400 wamekwama kwenye shule moja, wakiwemo wanawake na watoto katika kitongoji cha Jourat al- Shia ambapo licha ya kuwa hakuna wapiganaji kitongoji hicho kinaendelea kushambuliwa.

Ufaransa leo hii imeungana na Marekani katika kuelezea wasi wasi wake kwamba vikosi vya utawala wa Syria vinapanga kufanya mauaji mapya makubwa wakati vikiendelea kuushambulia mji wa Al-Haffe.

Serikali ya Marekani ilielezea wasiwasi wake kwamba utawala wa Assad ulikuwa unapanga mauaji mapya ya kinyama kufuatia yale ya watu 55 wiki iliopita katika mji wa Al-Kubeir na yale ya watu 108 yaliofanyika karibu na Houla hapo Mei 25 na 26.

Maandamano dhidi ya Assad katika mji wa Idilib.

Maandamano dhidi ya Assad katika mji wa Idilib.

Ahmad Fawzi msemaji wa mjumbe wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, kwa suala la Syria anasema Bwana Annan ana wasi wasi sana kuhusiana na mashambulizi ya karibuni katika mkoa wa Homs na pia taarifa za matumizi ya vifaru, mizinga na helikopta katika mji wa Haffa.

Wakati huo huo, mjumbe wa usuluhishi wa kimataifa, Kofi Annan, anataraji mkutano muhimu kuzungumzia mzozo huo wa Syria utafanyika hivi karibuni.

Annan aliyesimamia mpango unaoyumba wa vipengele sita wenye nia ya kukomesha umwagaji damu nchini Syria anataka kuwakutanisha viongozi wa dunia na wale wa kanda kumshinikiza kiongozi wa Syria.

Msemaji wake, Fawzi, amewaambia waandishi wa habari leo hii kwamba tarehe, mahala na orodha ya washiriki bado ni mambo ambayo hayakuamuliwa.

Annan alithibitisha kufuatia mkutano wa faragha wa Baraza la Usalama la Umojawa Mataifa wiki iliopita kwamba kunafanyika mazungumzo juu ya kuanzisha kundi la mawasiliano kushughulikia mzozo wa Syria.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia Annan anataka nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, yaani Marekani, Uingereza,Ufaransa,Urusina China, zikiwemo katika kundi hilo sanjari na Iran,Uturuki, Saudi Arabia, Qatar na nchi nyenginezo.

Urusi ambayo ni mongoni mwa marafiki wa mwisho waliosalia wa Rais Bashar al-Assad imesema inazialika nchi hizo katika mkutano wa kimataifa juu ya Syria.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/DPA/RTR
Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 12.06.2012
 • Maneno muhimu Syria, Latakia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15Css
 • Tarehe 12.06.2012
 • Maneno muhimu Syria, Latakia
 • Shirikisha wengine Tuma Facebook Google+
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo http://p.dw.com/p/15Css

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com