1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yazidi kuendelea Yemen

Admin.WagnerD8 Mei 2015

Ndege za kivita za ushirika wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia leo zimefanya mashambulizi mapya ya anga dhidi ya ngome ya wanamgambo wa kihuthi, baada ya wahuthi hao kuishambulia Saudi Arabia.

https://p.dw.com/p/1FN2X
Yemen Aden Houthis
Picha: picture-alliance/AP Photo/Wael Qubady

Saudi Arabia pamoja na washirika wake imefanya mashambulizi ya anga katika ngome ya wanamgambo wa kishia, saa kadhaa baada ya kupendekeza kusitisha mashambulizi ili kutoa nafasi ya usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Saudi Arabia la Saudi Press Agency, mashambulizi hayo yamelenga zaidi vituo vya udhibiti. Ikiwamo pamoja na jengo la mawasiliano, kiwanda cha kutengeneza mabomu ya kutegwa ardhini pamoja na ngome nyengine za waasi ikijumuisha jimbo la Saada lilioko kaskazini mwa Yemen. Jimbo ambalo linapakana na Saudi Arabia.

Saudi Arabia ambayo imekuwa ikiongoza mashambulizi ya anga kwa majuma 6 sasa, ilitoa onyo la adhabu kali dhidi ya waasi wakihuthi kwa kushambulia maeneo ya mpakani mwa Saudi Arabia.

USA Saudi Arabien Kerry bei Adel al-Jubeir
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, John Kerry na mwenzake wa Saudia, Adel al-JubeirPicha: picture-alliance/dpa/AP Photo/A. Harnik

Onyo hilo la Saudi Arabia lilitoka masaa mawili tu baada ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry, kuwasisitiza waasi wa kihuthi kukubali pendekezo la Saudi Arabia la kusitisha mapigano kwa siku tano ili kuwezesha usambazaji wa misaada ya kibinadamu.

"Usalama wa Saudi Arabia ndio kipau mbele kwa jeshi la ushirika pamoja na jeshi la Saudi Arabia. Waasi wakihuthi sasa wamechupa mkapa,." amesema msemaji mkuu wa jeshi la ushirika jenerali Ahmed al-Assiri.

Athari za mashambulizi

Umoja wa Mataifa umeiomba tena Saudi Arabia kusitisha mashambulizi nchini Yemen, ambayo hadi sasa yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 1,400 na kuwajeruhi karibu watu 6,000 wengi wao wakiwa ni raia.

Ismail Ould Cheikh Ahmed
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa , Ould Cheikh AhmedPicha: AFP/Getty Images/Z. Dosso

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Ould Cheikh Ahmed amewasili leo Saudi Arabia, kwa lengo la kuanzisha tena mazungumzo ya amani baina ya pande hizo mbili.

Kwa mujibu wa Shirika la habarii la Yemen la Saba linalodhibitiwa na Wahuthi, watu 13 wameuwawa ikiwamo wanawake na watoto baada ya kijiji kilichopo kaskazini mwa jimbo la Hajja kuripuliwa kwa mabomu.

Wakati huo huo ndege za kivita za jeshi la ushirika zimewashambulia waasi wa kihuthi usiku wa kuamkia leo, katika bandari ya mji wa Aden ambapo mapambano na washirika wa rais Hadi wa Yemen bado yanaendelea.