1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi ya wahudumu wa afya Kenya yatisha - Wauguzi

Mohammed Khelef
9 Februari 2024

Chama cha Wauguzi cha Kenya kinasema visa vya mashambulizi dhidi ya wahudumu wa afya vinaongezeka, baada ya kundi la watu kuivamia hospitali moja na kuwashambulia wahudumu na kuvuruga huduma kwenye hospitali hiyo.

https://p.dw.com/p/4cEKn
Wanafunzi wa masuala ya afya wakiandamana nchini Kenya.
Wanafunzi wa masuala ya afya wakiandamana nchini Kenya.Picha: Patrick Meinhardt/AFP

Ikiwaunga mkono wauguzi hao, serikali ya Kaunti ya Nakuru imesema baadhi ya viongozi wanaingiza siasa katika masuala ya afya.

"Hii hospitali ya Naivasha imekuwa na shida nyingi, sio kitambo kuna mtu alitoka mjini akaja kuwapiga watu risasi hapa. Haitakubalika kwamba watu wanakuja hapa kuwatishia wagonjwa na wahudumu wetu wa afya,” alisema Samuel Mwaura, katibu wa serikali ya Kaunti hiyo.

Soma zaidi: Watu 15 wafariki kwenye ajali ya barabarani Kenya

Tukio la karibuni zaidi lilitokea kwenye Hospitali ya Naivasha katika Kaunti ya Nakuru magharibi mwa Kenya, ambapo mama mmoja alipodai kumpoteza mtoto wake wa miezi minane kwa uzembe wa wahudumu wa afya.

“Hawanishughulikii, wananiacha tu hapa na mtoto, ninawaambia mtoto anapumua vibaya, hawashughuliki. Halafu wakasema eti masaa yameisha, wakatoka wakaenda.” Alieleza mama huyo aitwaye Beth Njoroge.

Ilibidi maafisa wa usalama waitwe ili kutuliza hali baada ya vurugu kuibuka kutokana na tuhuma hizo na watu kadhaa kujeruhiwa.

Mzozo wa umiliki wa hospitali

Hayo  yanajiri huku mgogoro ukitokota kati ya hospitali ya kibinafsi ya War Memorial ilioko Nakuru na serikali ya kaunti ya Nakuru, kuhusu umiliki wa hospitali hiyo.

Matibabu hutatizika pale wahudumu wasipokuwa salama.
Matibabu hutatizika pale wahudumu wasipokuwa salama.Picha: Brian Ongoro/AFP

Wamiliki wa hospitali ya kibinafsi ya War Memorial waliwasilisha kesi mahakamani baada ya wafanyakazi na wahudumu wote wa afya kuzuiwa kuingia kwenye hospitali hiyo.  

Soma zaidi: Nakuru yapandishwa hadhi na kuwa jiji, lakini nini maana yake?

Serikali ya kaunti inadai kwamba muda wa umiliki wa ardhi ya hospitali hiyo ambayo ilikuwa imekodishwa ulizidishwa kwa njia isiyo halali na wanataka hospitali hiyo ihamishwe kwa umma.

Lakini uongozi wa hospitali hiyo umeyakana madai hayo na kusema serikali ya kaunti imeshindwa kutoa ushahidi wowote unaodhihirishwa madai yao.

Wakili wa Hospitali ya War Memorial, Chomba Kamau, ameilezea Mahakama ya Ardhi mjini Nakuru kwamba, “Polisi hawajatekeleza amri ya mahakama ya kuwaruhusu madaktari na wauguzi kuingia hospitalini humo na kuendelea na huduma zao kama kawaida.”

Mzozo huo umeendelea kuwaacha wagonjwa katika hali mbaya.

Uhaba wa usalama kwa wahudumu wa afya

Mwezi uliopita, daktari mmoja aitwaye Laban Lang’at aliwawa katika Hospitali Kuu ya Nakuru, muda mchache baada ya kukamilisha muda wake wa kazi na mwili wake kutupwa kwenye mtaro wa maji ndani ya hospitali hiyo.

Maafisa wa afya nchini Kenya.
Maafisa wa afya nchini Kenya.Picha: Robert Bonet/NurPhoto/picture alliance

Ingawa uchunguzi wa kifo cha daktari huyo unaendelea kwa kuwashirikisha maafisa wa upelelezi kutoka jijini Nairobi, wengi wanahoji ikiwa kuna usalama wa wahudumu wa afya kwenye maeneo yao ya kazi, ikizingatiwa kwamba wanahudumu usiku na mchana.

Soma zaidi: Wahudumu wa afya Nakuru walalamikia mazingira duni ya kazi

“Wauguzi tulionao tunajua wanafanya kazi kwa kujitolea. Kuna upungufu mkubwa wa wahudumu wa afya nchini,” alieleza Benard Njoroge, mwenyekiti wa Chama cha Wauguzi nchini Kenya.

Chama hicho kinaitaka serikali kuwahakikishia wahudumu wa afya mazingira bora ya kazi, ili pia kuwapa nafasi nzuri ya kuwashughulikia wagonjwa ipasavyo.

Imetayarishwa na Wakio Mbogho/DW Nakuru