1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marupurupu ziada yanahanikiza magazetini

8 Oktoba 2012

Mjadala kuhusu marupurupu wanayopokea wanasiasa kwa shughuli za ziada , ziara ya kansela Angela Merkel Ugiriki na mvutano kati ya Uturuki na Syria ni miongoni mwa mada zilizo hanikiza magazetini .

https://p.dw.com/p/16MBc
Peer Steinbrück akicheza damaPicha: picture-alliance/dpa/dpaweb

Sudi:

Mjadala kuhusu marupurupu wanayopokea wanasiasa kwa shughuli za ziada wanazofanya,ziara ya kansela Angela Merkel nchini Ugiriki na mvutano kati ya Uturuki na Syria ni miongoni mwa mada zilizo hanikiza magazetini hii leo.Kurasa za magazeti zimefunguliwa na Oummilkheir.

Tuanzie lakini na madai ya kuachwa wazi marupurupu ziada wanayopokea baadhi ya wanasiasa kwa shughuli wanazofanya mbali na vikao vya bunge.Mgombea kiti cha kansela kutoka chama cha upinzani cha SPD ndie aliyeingia midomoni .Gazeti la "Neue Osnabrücker Zeitung" linaandika:

Oummil:

Yadhihirika kana kwamba hotuba anazotoa Peer Steinbrück zinaambatana na sheria.Hata hivyo hali hiyo sio sababu inayomfanya mgombea huyo wa kiti cha kansela , kutoka chama cha SPD asilaumiwe.Masuala chungu nzima mtu anaweza kujiuliza kwa mfano inakwenda kwendaje chama cha SPD ambacho daima kimekuwa kikihoji kwamba mishahara mikubwa mikubwa ya mameneja si jambo la haki,lakini Steinbrück kwa kuhutubia mara tatu tu alipwe marupurupu ambayo yanapindukia mshahara wa mwaka mzima wa mfanyakazi wa dukani?Hata kama anapozitoa hotuba hizo hendi kinyume na sheria,lakini kuna kile kinachojulikana kama maadili ambayo yanabidi yazingatiwe.

Sudi:

Gazeti la "Rhein-Zeitung" linahisi wanaomkosoa Steinbrück wanamhusudu tu.Gazeti linaendelea kuandika:

Oummil:

Kijicho labda ndio sababu ya kupamba moto mjadala huo.Peer Steinbrück ni mwanasiasa ambae ujuzi wake unatakiwa na wengi kinyume na wabunge wengine.Kosa likowapi hapo? Hakuna anaeweza kuhakikisha kwamba mwanasiasa huyo wa SPD amejiachia "kununuliwa" na wana uchumi na kufichua maoni yake.Aste aste jamani! Kampeni za uchaguzi zinaonyesha kuanza mapema safari hii."

Sudi:

Mada ya pili magazetini inahusiana na mgogoro wa kiuchumi wa Ugiriki na ziara atakayofanya kesho kansela Angela Merkel nchini humo.Gazeti la "Bild-Zeitung" linaandika:

Oummil:

Kimsingi wagiriki wangebidi wabebe mabango yenye picha za Angela Merkel na kupepea bendera ya Ujerumani majiani,kansela atakapofika ziarani nchini humo.Kwasababu hakuna nchi yoyote inayoipatia Ugiriki fedha nyingi na dhamana kama Ujerumani.Badala ya kushukuria,wagiriki wanapiga makelele majiani na kuikaripia Ujerumani.Kansela wa Ujerumani hawezi kuwapatia chengine wagiriki isipokuwa kuwaambia ukweli hata kama ni mchungu.Nao ni kwamba Athens itapatiwa misaada zaidi ya fedha tu ikiwa itatekeleza ahadi ilizotoa za kufunga mkaja.Atakaeridhia wagiriki washushe pumzi,hawezi kuwakatalia wareno na Hispania kufanya hivyo hivyo.Hapo lakini mpango mzima wa kuinusuru sarafu ya Euro utaingia matatani.

Sudi

Mada yetu ya mwisho magazetini inahusu vita vya Syria vinavyotishia kutapakaa hadi Uturuki.Gazeti la "Mitteldeutsche Zeitung" linaandika"

Oummil:

Kung'olewa madarakani Assad ungekuwa ufumbuzi wa mzozo huo.Jamii yake ndio inayodhibiti hali ya maisha nchini Syria.Fursa ya kupanda daraja anaipata mtu wa jamii hiyo tu.Yaani waumini wa madhehebu ya Alawi.Wasunni ndio jamii kubwa nchini humo,wakifuatwa na wakurd na jamii ndogo ndogo za Armenia,Assyra na Arama ambao ni wakristo.Bila ya kuwasahau wakimbizi milioni moja wa kipalastina na wengine laki mbili wa Iraq.Kila wakati ambapo mapambano dhidi ya utawala wa Assad yatachukua sura ya vita vya wenyewe kwa wenyewe ndipo masuala ya kikabila na kidini nayo yatakapozidi kutangulizwa mbele.Vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoongozwa na wasunni havitalenga pekee dhidi ya utawala wa Assad.Kila upande utataka kujiimarisha.Hili si tena vuguvugu la mageuzi la nchi za kiarabu-litageuka vita vya koo.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Abdul-rahman